WAKATI Tume ya Mabadiliko ya Katiba
(maarufu Tume ya Warioba) inaundwa, wapo watu walioamini maoni yao
yatachukuliwa na tume hiyo, hususan kama maoni hayo yatakuwa ni ya wengi.
Watu waliamini hivyo kwa sababu
waliambiwa tume hiyo ni ya “kukusanya maoni” ilhali kiuhalisia tume hiyo ilikuwa
ni ya ‘kusikiliza’ tu maoni lakini ikiwa haina mfumo wenye kuilazimisha tume
kuchukua maoni ya wananchi wengi.
Kimsingi muda wote ambao wananchi
waliutumia kutoa maoni, Tume ilikuwa inawasikiliza tu lakini yenyewe ikiwa ni
uamuzi wa mwisho wa ‘maoni gani’ ni muhimu na yapi yanafaa kuingizwa kwenye
Katiba.
Watu hawa wengi waliotoa maoni yao
katika sehemu mbalimbali za nchi yetu walifanya hivyo wakiamini kuwa wanaweza
kuishawishi tume kuchukua maoni yao. Watu hawa wengi walikwishasahu kuwa Tume
ya Warioba kimsingi ni tume ya kusikiliza maoni tu na kutoa mapendekezo.
Kwa kawaida mapendekezo yanayotolewa na
tume yanapaswa kuwa yale yenye kuakisi matakwa ya wengi. Tume ya Warioba hata
hivyo, haikutakiwa kutoa mapendekezo yake kutokana na kuona matakwa ya wengi.
Iliundwa kusikiliza tu maoni na kutoa mapendekezo yake bila kujali maoni ya
wananchi yalikuwaje.
Hii haitakuwa mara ya kwanza kwa tume
ya maoni Tanzania kutokujali maoni ya wananchi wengi na badala yake kutoa
mapendekezo kinyume cha maoni ya wananchi hao. Wengi wetu tunakumbuka tume ya
Jaji Nyalali iliyopita na kuwauliza wananchi kama turudi kwenye mfumo wa vyama
vingi au tuendelee kuwa katika chama kimoja.
Kwa wanaokumbuka tume ile baada ya
kufanya kazi yake ilikuta kuwa wananchi waliotoa maoni asilimia 80 walitaka
tuendelee kuwa chini ya chama kimoja huku asilimia 20 tu walitaka tuingie
kwenye vyama vingi. Waliotaka chama kimoja wengi walitaka demokrasia yake
iboreshwe na kusimamiwa vizuri zaidi. Hata hivyo, tume katika hekima yake na
‘ugenius’ wake (ikiwa imejaa wasomi mahiri wa sheria) ikaamua ‘kupendekeza’
kuwa Tanzania iingie kwenye mfumo wa vyama vingi.
Kimsingi tume ile ilienda kinyume
kabisa cha matakwa ya wananchi. Mara nyingi umesikia watu wakinukuu Katiba na
kusema kuwa “madaraka ya kutawala yatatoka kwa wananchi”. Ukisikiliza vizuri
unaweza ukafikiria inasemwa “madaraka ya kutawala yatatoka kwa wananchi wasomi”.
Kilichotokea ni kuwa mfumo wa vyama
vingi uliingizwa tena nchini si kwa sababu wananchi wengi waliutaka bali kwa
sababu kundi la wasomi waliamini kuwa ndio njia pekee ya kuboresha demokrasia.
Ulipofika uchaguzi wa 1995, CCM ikashinda kiti cha urais kwa asilimia 61.8;
uchaguzi wa 2000 CCM ikashinda urais kwa asilimia 71.7; mwaka 2005 CCM
ikashinda kwa asilimia 80.2 na mwaka 2010 CCM ikashinda 62.8.
Na ukiangalia kwenye viti vya ubunge
bado CCM inashikilia karibu asilimia 80 hivi. Je, inawezekana matokeo haya
yanaakisi matakwa ya wananchi ya kutaka nchi iwe kwenye chama kimoja? Je, kwa
kupendekeza mfumo wa vyama vingi kinyume cha matakwa ya wananchi Tume ndio
imewapa wananchi, yote yanayotokea leo katika siasa?
Kwamba pamoja na kutawala kwake vibaya,
ufisadi na sera mbovu zilizoshindwa bado CCM inapendwa na wananchi wengi? Kama
hili ni kweli na likaendelea kuwa kweli kwa chaguzi kadhaa zijazo siyo kwamba
CCM itaendelea kushinda?
Fikiria uchaguzi mdogo ujao wiki hii.
Ukisikiliza lugha za kisiasa na mwitikio wa wananchi unaweza ukaamini kuwa CCM
haiwezi kushinda hata kura moja. Lakini kama tulivyoona sehemu mbalimbali
nchini CCM bado ina wapenzi wengi sana. Je, wapo watakaoshangaa wakisikia kuwa
baadhi ya viti vya udiwani vitakavyogombaniwa vikaendelea kuwa CCM au
kunyang’anywa kutoka upinzani? Mimi siwezi kushangaa.
Ninachozungumzia hata hivyo ni hili la
Tume ya Warioba kuweka mapendekezo kwenye rasimu yake ya Katiba huku ikiweka
wazi kuwa ilichopendekeza siyo maoni ya wananchi bali maoni ya tume yenyewe.
Kwa watu waliopata kumsikiliza Warioba wakati wa uzinduzi (sijui kwa nini watu
wanazindua rasimu!) alizungumza na kutuonesha kuwa yeye na wenzake ndio
walikuwa na maoni bora zaidi kuliko ya wananchi. Naomba nirejee baadhi ya kauli
zake mbele ya Makamu wa Rais.
Kuhusu
haki za binadamu wananchi walitaka haki hizi ziimarishwe na kusiwe na vikwazo
visivyo vya lazima. Tume imependekeza mabadiliko katika baadhi ya haki za
binadamu kwa madhumuni ya kuziimarisha. Moja ya mabadiliko hayo ni kuhusu uhuru
wa mwananchi kushiriki shughuli za umma. Tume inapendekeza kwamba vikwazo
vilivyowekwa kuzuia mgombea huru viondolewe. Kwa maana nyingine Tume inapendekeza
mgombea binafsi aruhusiwe.
Swali: Kuna mtu anajua ni
asilimia ngapi ya wananchi walitaka wagombea huru waruhusiwe katika nafasi zote
kama tume ilivyopendekeza?
Tume
pia, inapendekeza haki mpya ziingizwe kwenye Katiba ikiwa ni pamoja na haki ya
wafanyakazi, haki ya mtoto, haki za watu wenye ulemavu, haki za wanawake, haki
za wazee, haki za makundi madogo katika jamii, haki ya elimu na kujifunza, haki
ya kupata habari, haki na uhuru wa habari na vyombo vya habari na kadhalika.
Swali: Tume inapata wapi
madaraka ya “kutengeneza” haki mpya? Hili limenishangaza kwa sababu tume imejaa
wasomi na watu ambao kwa kila kipimo wanapaswa kujua zaidi. Lakini katika
‘ugenius’ wao huo ndugu zetu wameamua kutengeneza ‘haki’ mpya? Je, ni wananchi
waliotaka hizi ‘haki’ mpya ziingizwe? Na Katiba haiingizii haki ‘mpya’
inatakiwa ‘kutambua’ uwepo wa haki hizo. Kwa mfano, haki ya kuishi haitolewi na
Katiba bali Katiba inatambua tu.
Mgombea
wa nafasi ya Rais atatangazwa kuwa mshindi iwapo atakuwa amepata kura zaidi ya
asilimia hamsini ya kura zote zilizopigwa.
Swali: Haya ndio matakwa ya
wananchi au ndio maoni ya Tume? Kama ni maoni ya Tume wananchi wao walitaka
nini?
Angalia na hili;
Kuhusu
Bunge kutakuwa na wabunge wa aina mbili. Kutakuwa na wabunge wa kuchaguliwa na wabunge
watano wa kuteuliwa na Rais kuwakilisha watu wenye ulemavu. Kila Jimbo la
Uchaguzi litakuwa na wabunge wawili mmoja mwanamke na mwingine mwanamume.
Hoja: Nina uhakika kuna ‘magenius’
waliokaa kwenye Tume wakaona kuwa hili ni wazo bora kabisa! Sasa najiuliza,
hivi ni kweli wananchi wengi waliotoa maoni walitaka kila jimbo ‘LAZIMA’ liwe
na mbunge mwanamke na mwanamume? Hivi kuwa kwao watu wa jinsia moja ama
tofauti, kunahakikishia vipi kuwa watakuwa ni wawakilishi wazuri wa wananchi?
Au wanataka kuwa na takwimu tu zinazoonesha ‘gender parity’?
Kama lengo ni huo usawa wa kijinsia kwa
nini waishie kwenye wabunge tu? Kila kata iwe na diwani mwanamke na mwanamume;
kila kijiji kiwe na viongozi wanawake na wanaume; na kwenda mbali zaidi
‘magenius’ wetu wangeweka kuwa ni lazima Rais wa Muungano ateue mgombea mwenza
wa jinsi tofauti – hii itaonesha usawa. Lakini wasiishie hapo; Majaji ni lazima
wateuliwa kwa kuangalia jinsi zao, na teuzi nyingine zote!
Lakini pia itabidi tuhoji kwa nini
‘jinsi’ (ama jinsia wengi wanavyopenda kuita) ndio iwe kigezo kikubwa hivyo?
Kwa nini wasiangalie na dini au rangi ya watu? Au hata makabila yao? Si lengo
ni kuonesha usawa? Kwani usawa wa watu uko katika jinsia zao au katika utu wao?
Nina hoja nyingi sana ninapoangalia
rasimu hii. Hitimisho langu ni rahisi kulielewa tu. Rasimu hii imetoka kwa Tume
na haikutoka kwa wananchi. Sasa, nina uhakika kuna watu wanasema wanaponisoma –
sasa kama ina mambo mazuri hivi ambayo tumekuwa tukiyalalamikia hata kama
hayakutolewa na wananchi si ni bora kweli kweli na wote tuikubali rasimu hii?
Kwamba, kama wasomi wameona mawazo yao ni mazuri sana na yanafaa kwa Taifa
zima, kwa nini tusikubali tu?
Jibu langu ni hili katika swali: Kama
Katiba inaakisi mawazo ya wajumbe wa tume na wasomi walioulizwa, je bado
tunaweza kusema ni Katiba kutoka kwa wananchi? Je, ni kweli kama mawazo ya
wananchi hayakuchukuliwa kwa kiwango kinachoonesha ukuu wao (supremacy of the
people) bado Katiba itakuwa ni ya wananchi? Lakini swali kubwa ni hili; kama
mfumo wa kuandika Katiba mpya ya wananchi hauwahakikishii wananchi hao kuwa
mawazo yao yatazingatiwa, kweli wananchi wana sababu ya kukubali Katiba hiyo?
Jibu langu ni hapana. Sijui la kwako.
Kama kuna mengine katika rasimu hii
nitaendelea na mada hii wiki ijayo, In shaa Allah
Source
;www.raiamwema.co.tz: Lula wa Ndali Mwananzela
No comments:
Post a Comment