Na Maggid Mjengwa,
NAHOFIA, kuwa Watanzania tumejikita
kwenye ndoto ya utajiri wa gesi na mafuta na kusahau kilimo chetu.
Hivyo, ni hatari kwa uchumi wetu.
Tunafikiria utajiri wa gesi na mafuta
kana kwamba katika dunia hii ni sisi tu Watanzania ndio wenye utajiri wa
akiba ya gesi na mafuta. Hatujui, kuwa katika dunia hii kuna nchi
zilizo akiba hizo za mafuta na gesi lakini bado uchumi wao hauwafanyi
watu wao wawe ni wenye neema tu. Nao wanafikiria pia kwenye vyanzo
vingine vya kuinua uchumi wao ikiwamo kilimo.
Naam, Mwanafalsafa David Hume alipata
kusema; “Mbegu yako imekomaa leo, yangu itakomaa kesho. Ni jambo la
manufaa kwetu sote kama nitalima pamoja nawe leo, na wewe unisaidie
kulima kesho. Siwezi kuwa na urafiki nawe
kama naona kuwa hujengi urafiki nami.
Msimu utapita, nasi tusipoaminiana na kushirikiana, basi, sote tutakula
hasara.” – David Hume.
Kuna wakati nilisafiri kwenda
Finland. Kule nilishangazwa sana kuona matrekta mengi yamepangana kwenye
shamba moja. Nilimwuliza mwenyeji wangu; kulikoni?
Nilijibiwa kuwa huo ni utamaduni wa
wakulima wa nchi ile. Kila mwaka huwa na mashindano ya kulima kwa
matekta. Wakulima wa eneo moja huenda kwenye shamba la mwenzao na
kufanya mashindano hayo; wanaangalia ni nani amewazidi wenzake katika
kunyosha mistari, kulima kwa kasi, na kadhalika.
Ni katika nchi ile ya Finland
nikaelewa, kuwa utamaduni huo ulianza tangu zama za kilimo cha kutumia
farasi. Matrekta yalipoingia katika kilimo, ilitokea kwa mkulima mmoja
akamwuliza mwenzake; “Je, trekta lako ni sawa na nguvu za farasi
wangapi? Ni katika mazingira hayo, hata kipimo cha nguvu za farasi
kikaanza kutumika; horse power, ina maana ya nguvu ya farasi, inatumika hata leo katika kupima nguvu za mashine mbalimbali.
Nitazungumzia umuhimu wa mtaji wa
kijamii ( social capital) na ari ya kiraia ( civil courage) ili kuweza
kuinua uchumi wa mtu mmoja mmoja na hatimaye kuinua uchumi wa nchi. Ili
jamii na nchi kwa ujumla iendelee kiuchumi inahitaji kuwa na mtaji huu
muhimu. Kukua kwa ushirikiano wa kijamii katika shughuli mbalimbali, iwe
za huzuni au sherehe, ni mfano wa kuwapo kwa msingi mzuri wa mtaji wa
kijamii.
Dhana hii ya mtaji wa kijamii na ari
ya kiraia huenda ni ngeni kwa baadhi yetu. Hata hivyo, ni kitu ambacho
tunakishuhudia kila kukicha. Tunaona vikundi mbalimbali vya kijamii
vikiongezeka. Leo tuna mifano ya jumuiya za kuzikana, tuna jumuiya za
kukopeshana na nyingine nyingi.
Tuchukue mfano huu wa jumuiya zenye
kushirikiana katika sherehe, mathalan, harusi. Siku hizi ukitembelea
kumbi za starehe si ajabu ukakutana na watu walio katika kikao cha
kamati ya maandalizi ya harusi. Ni kamati hizi zenye kupanga mikakati
ya kufanikisha harusi. Wakati mwingine hupanga hata kile kinachoitwa
“harusi ya kufa mtu!”.
Kamati ya maandalizi ya harusi
itakutana hata mara mbili kwa mwezi. Na mara nyingi hukutana kwenye
kumbi za starehe baada ya saa za kazi. Kamati itapanga mikakati ya
kufanikisha harusi huku wajumbe wengine wa kamati wakinywa bia. Na hata
wakifanikisha harusi, watakutana tena kama kamati maalumu kwa “kuvunja”
kamati. Watakula, watakunywa, watasaza. Fungu la kufanya hayo hupangwa
pia kwenye bajeti ya harusi!
Wakati wenzetu kule Finland
wanashindana katika shughuli za maendeleo, sisi, pamoja na umasikini
wetu, bado tunashindana kwenye kufanya harusi za anasa kubwa! Tunatumia
mamilioni ya shilingi kufanya harusi za “kufa watu” wakati kuna watu
nchi hii wanaokufa kwa umasikini. Wanakufa kwa vile barabara za kutoka
vijijini kwao hadi ziliko hospitali za wilaya hazipitiki! Kuna watu
wanakufa kwa kukosa fedha za kununulia madawa kwa magonjwa yao. Mjadala
huu utaendelea...
0754 678 252, http://mjengwablog.com
No comments:
Post a Comment