KWA
kweli nilishitushwa na ukali wa mjadala ulioibuka bungeni na nje ya
Bunge baada ya Mbunge wa Nyamagana (CHADEMA), Ezekiah Wenje, hivi
karibuni, kukihusisha Chama cha Wananchi (CUF) na ushoga kutokana na
chama hicho kuwamo katika kundi la vyama vya kiliberali, ambamo
mwelekeo wa sehemu kubwa ya vyama katika kundi hilo ni kuunga mkono
ushoga.
Mabishano yaliyokuwapo bungeni yalikuwa makali kiasi kwamba ilibidi
Naibu Spika, Job Ndugai, afanye uamuzi wa kuahirisha kikao cha Bunge.
Naambiwa mjadala uliendelea kuwa mkali kwenye viwanja vya Bunge baina
ya wabunge wa vyama hivyo viwili.
Nimeshuhudia wabunge wakiitana majina ya ajabu bungeni. Majuzi tu hapa
mbunge mmoja wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Peter Serukamba, naye
alitukana ndani ya ukumbi huo wa Bunge lakini ukali na hamaki
iliyokuwapo haikukaribia hata nusu ya mjadala huu wa ushoga.
Nimejiuliza maswali mengi lakini moja kubwa ambalo ni je; ushoga ni
uovu au tatizo kubwa zaidi kuliko ufisadi? Je, chama kutetea au
kutotetea mashoga kuna athari zozote kwa taifa letu?
Mojawapo ya matatizo makuu ya jamii nyingi duniani kuhusiana na
masuala ya ushoga ni kukataa kuyajadili hadharani. Hili limekuwa ni
suala la marufuku na matokeo yake watu wengi hata hawafahamu
wanachokichukia au wanachokikubali na badala yake wanashikilia tu
misimamo yao kwa kusingizia dini au mila na desturi.
Na sababu za kidini na kimaadili zimetumika mara nyingi tu kwenye
unyanyasaji wa makundi fulani ya watu. Enzi ya ubaguzi wa rangi nchini
Afrika Kusini na kwingineko duniani ambako watu weusi walitendewa
vibaya kuliko hata wanyama, dini ilitumika kutetea unyama huo.
Kwenye mafunzo ya dini ya makaburu, wayahudi na wabaguzi wengine, watu
wanafundishwa watu weusi ni zao la mtoto wa Nabii Nuhu aliyeitwa Ham
anayedaiwa kumchungulia baba yake akiwa utupu.
Kwamba baada ya baba yake kugundua, alimlaani na kuanzia hapo akawa
mweusi na asili ya mtu mweusi ikaanzia hapo. Hii maana yake ni kwamba
watu weusi ni waliolaaniwa na Mwenyezi Mungu.
Kwa Kaburu aliyepitia mafunzo hayo ya dini, huwezi kumweleza kitu
kuhusu mtu mweusi na akaelewa. Hata hivyo, ukisoma maandishi tofauti
tofauti ya biblia na sayansi, haileti mantiki kwa mtu kutoa laana ya
kumfanya mtu atoke kuwa mzungu na au mhindi na awe mchina au mwarabu.
Biashara ya utumwa iliendeshwa pia kwa propaganda hizi. Mtu alikuwa ni
mchungaji, shekhe au padri lakini alikuwa na watumwa wake. Na wala
hakuona kosa lake kwa sababu alifunzwa kwamba mtu mweusi ni laana tupu.
Kadhia hii ya mashoga imewakuta pia wanawake. Wapo waliokuwa wakisema
wanawake hawana haki zozote kwa sababu ndiyo waliosababisha Adamu ale
tunda na kusababisha hasira ya Mwenyezi Mungu kwa wanadamu.
Ilifikia wakati, kwenye kitabu cha biblia, mwandishi anaandika kwamba
katika mkutano fulani wa kidini, wanaume kadhaa walihudhuria. Wanawake
hawakuwa chochote wala lolote. Hawakufaa hata kuhesabiwa.
Katika mojawapo ya hekaya za Wagiriki nilizowahi kusoma, inadaiwa kuna
kipindi Wagiriki walikuwa wanaoana wanaume kwa wanaume kwa sababu
walihisi mwanamke ni kiumbe cha chini mno kuwa na uhusiano nacho. Ni
afadhali uoe mwanamume mwenzako kuliko mwanamke.
Na ukichunguza, utaambiwa hizo zilikuwa mila na desturi zao au mapokeo ya kidini.
Kimsingi, sababu zote hizo zilizotumika kuwanyanyasa na kuwatenga
watumwa, wanawake na watu weusi siku za nyuma na hata leo, ndiyo
hizohizo zinazotumika dhidi ya mashoga kwenye kizazi hiki.
Hoja yangu kubwa ya leo ni kwamba mapokeo ya kimila au kidini kuhusu
jambo lolote si lazima yawe sahihi na watu hawatakiwi kuwa wagumu
kubadilika kwa sababu ya kulinda mapokeo hayo.
Wiki iliyopita, katika mijadala iliyokuwapo katika mitandao ya
kijamii, mtu mmoja alinishambulia kwa msimamo wangu wa kutaka mashoga
wasinyanyaswe au kutendwa kama wanyama. Alishutumu kwamba mimi napenda
sana umagharibi.
Jina lake alikuwa anaitwa Alphonce Godfrey. Nikamuuliza maswali mawili
tu; kama yeye hapendi umagharibi, mbona jina lake ni la kimagharibi?
Pili, hivi watetezi wote wa haki za wanawake ni wanawake?
Au unapotetea haki za wanyama ni lazima na wewe uwe mbwa au tembo?
Nafikiri watu wengi wameshindwa kutetea haki za mashoga kwa hofu ya
kuonekana ni mashoga.
Wikiendi iliyopita, nimesoma makala moja katika gazeti moja la hapa
nchini ambapo shoga mmoja wa kiume amelalamika kwamba anavamiwa na
vijana nyumbani kwake na kubakwa mara kwa mara.
Hakuna anayemsaidia kwa vile yeye ni shoga. Akienda polisi, anawekwa
katika mahabusu ya kiume kwa vile yeye ni mwanamume. Matokeo yake
anabakwa na mahabusu wenzake. Kwa sasa ameathirika na Ukimwi, lakini
wabakaji hawajui na wanaendelea tu.
Vitendo hivi vya wanasiasa na watu wenye ushawishi kwenye jamii yetu
kupaniki kwa sababu tu wameambiwa wana uhusiano na ushoga vinaongeza
ugumu wa maisha ya wenzetu hawa.
Na kutumia ushoga kama silaha ya kumshinda mpinzani wako kisiasa
katika nchi ambayo uelewa wa mambo ni mdogo kama Tanzania nayo pia ni
makosa.
Kuna wanaoamini kwamba mashoga wanazaliwa kuwa hivyo. Ni masuala ya
homoni na jenetiki ndiyo yanayosababisha hivyo. Sawa sawa na mtu
kuzaliwa kuwa albino. Kama unatetea maalbino wasiuawe, huna haki ya
kumshutumu anayetetea mashoga.
Madaktari wanasema ushoga unatokana na mazingira anayokulia mtu. Kama
ambavyo hakuna mtu anayezaliwa teja, mwizi, jambazi, mlevi au
mwasherati, ndivyo hivyo anavyozaliwa shoga.
Kama tunaishi na familia zetu na walevi, majambazi, mateja na mafisadi
wengine, tunashindwaje kuishi kwa namna hiyohiyo na mashoga?
Maisha yetu yana unafiki mbaya sana. Kuna watu ambao wanafahamika
kwamba ni mafisadi, walevi, waasherati, wauaji na wahaini lakini
wanasali kila wiki, wanachaguliwa kuwa viongozi na michango yao
inapokewa misikitini na makanisani.
Hebu fikiria itakuaje siku ambapo shoga ataingia kanisani au msikitini
na kuomba kuchaguliwa kuwa kiongozi au kutoa mchango wa kutaka kujenga
chochote? Nina imani watu wataihama nyumba hiyo ya ibada.
Mashoga na ushoga vimeishi na mwanadamu kwa miaka mingi, mingi sana.
Hautaondoka kwa sababu mimi na wewe tunachukia. Hautaondoka kwa sababu
tukiitwa mashoga tunataka kukunja ngumi na kutoa ngeu.
Katika ngazi ya familia, tuwakuze watoto wetu kimaadili na kidini.
Viongozi wa dini, wafanye kazi zao kwenye nyumba za ibada na nje ya
hapo.
Kinachobaki, tumwachie Mwenyezi Mungu. Mwisho wa siku yeye ndiye atakayetuhukumu sote… Mashoga na Wasio Mashoga
source: Raia Mwema: Ezekiel Kamwaga
No comments:
Post a Comment