Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi.
Rais mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi,
amesema demokrasia ya vyama vingi ni lazima ikwepe chuki, uhasama na
badala yake ihimize ushindani wa nguvu ya sera kutokana na ushawishi wa
kisera bila ya kumwaga damu nchini.
Mzee Mwinyi alitoa matamshi hayo jana
wakati akifunga rasmi kampeni za CCM katika mkutano wa hadhara
uliofanyika katika kijiji cha Mapape, Mkoa Kusini Pemba.
Alisema mwanasiasa ambaye si mufilisi wa
hoja hawezi kutamani na kuutumia mfumo huo kinyume na misingi ya upendo,
umoja na mshikamano wa kitaifa hivyo ni lazima jamii ianze kuwaepuka na
kuwa na tahadhari na wanasiasa wa aina hiyo.
Akihutubia mamia ya wananchi, Mzee Mwinyi
alisisitiza kuwa enzi ya utawala wake ndipo mfumo wa vyama vingi
ulipoingia na kwamba hakuelekeza uwe mfumo wa mapigano, uhasama na chuki
bali serikali yake ilikusudia kuwapo ushindani wa sera na nguvu ya
hoja.
Aidha, alisema demokrasia ya vyama vingi
isipotoshwe na wanasiasa ili kuibadili Tanzania kuwa uwanja wa mapigano
na machafuko na badala yake akasema kila chama cha siasa kitambue kina
wajibu na ulazima wa kuheshimu sheria za nchi.
Alisema si haki litokee kundi moja
kulizungumzia jingine na badala yake kila mtu apate fursa ya kutoa
mawazo yake ipi ni namna bora itakayoliongoza Taifa kwa misingi ya
usawa, haki na demokaria ya kweli.
Akimnadi mgombea wa CCM jimbo la Chambani
Mattar Sarahan Said aliwataka wananchi wa jimbo hilo kumchagua mgombea
huyo kwa kuwa anatokana katika chama kinachofuata miiko, umoja na
kwamba mgombea huyo ni bora kuliko wa vyama vingine vya siasa.
“Nimekuja kwa unyenyekevu na staha , kila
mmoja atambue hilo , umoja siku zote si shari bali ni hiari ya mtu
binafsi, msikubali kuitupa fanaka ya ustawi wa Taifa letu la sasa na
lijalo ” alisisitiza Mzee Mwinyi.
Aliwataka wananchi wa jimbo la Chumbani
kumchagua kwa kura nyingi Mattar ili awe mbunge wao kwasababu ni kijana
hodari na mwepesi katika kupambanua mambo mema na kukataa mabaya.
Wagombea wa ubunge katika uchaguzi mdogo
jimbo la Chambani kisiwani Pemba ni pamoja na Mattar (CCM), Said Miraji
Abdallah (ADC), Yussuf Salum Hussein (CUF) na Sitti Usi Shaib (Chadema).
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment