Tume ya Mabadiliko ya Katiba nchini
Tanzania, imependekeza wawepo wagombea huru katika ngazi za uchaguzi
mbalimbali nchini humo. Hayo ni miongoni mwa mapendekezo yaliyotangazwa
jijini Dar es salaam na Mwenyeketi wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Jaji
Joseph Warioba wakati wa uzinduzi wa Rasimu ya Kwanza ya Katiba Mpya.
Jaji Warioba amesema pia wapo wananchi
waliopendekeza kwamba, wagombea huru waruhusiwe kugombea nafasi zote
isipokuwa nafasi ya urais. Jaji Warioba amesema tume ilipitia maoni hayo
na kupendekeza kwamba, wagombea huru waruhusiwe kugombea nafasi zote
kuanzia ngazi ya Mwenyekiti wa Mtaa hadi nafasi ya Urais.
Kadhalika Jaji Warioba amesema, Tume
pia imependekeza kwamba, mgombea yeyote wa urais ili athibitike kuwa ni
mshindi atalazimika kupata zaidi ya asilimia hamsini ya kura, na kwamba
endapo mgombea hatafanikiwa kupata asilimia hamsini uchaguzi utarudiwa
kwa kuangalia wagombea wawili waliopata kura nyingi.
Mapendekezo mengine yaliyotangazwa na Tume ni pamoja na kuwepo kwa serikali tatu yaani ya Bara,Zanzibar na ile ya Shirikisho.
Pia tume imependekeza kuwa, Bunge la
Muungano liwe na jumla ya Wabunge 75, hamsini kutoka Bara, ishirini
kutoka visiwani na watano wateuliwe na Rais kutoka makundi maalum ya
walemavu.
Mapendekezo mengine ya Tume ya
Mabadiliko ya Katiba ni pamoja na Rais kubakia na madaraka yake ya
uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu, lakini uteuzi wa ngazi za chini
uachiwe Tume ya Utumishi.
Imeeleza kwamba, Rais mara baada ya
kufanya uteuzi wa viongozi wa ngazi za juu wakiwemo, mawaziri, manaibu
waziri, jaji mkuu na naibu jaji mkuu, viongozi hao watalazimika
kuthibitishwa na Bunge.
Chanzo:bbcswahili
No comments:
Post a Comment