Dar es Salaam. Marekani imetaja sababu nne
ambazo zimemfanya Rais Barrack Obama kuijumuisha Tanzania katika ziara
yake ya bara la Afrika.
Rais Obama amepanga kulitembelea bara la Afrika
kuanzia Juni 26 hadi Julai 3, mwaka huu na atazitembelea pia Senegal na
Afrika Kusini.
Kiongozi huyo wa Marekani ambaye baba yake mzazi
ni mzaliwa wa Kenya, anatarajiwa kuwasili nchini Julai Mosi kwa ziara ya
siku tatu. Atakuwa Rais wa tatu wa Marekani kuitembelea Tanzania baada
ya Bill Clinton mwaka 2000 na George Bush mwaka 2008.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Balozi wa Marekani, Alfonso Lenhardt alisema sababu ya kwanza ya
Obama kuja Tanzania ni kutokana na kuwa mfano wa utawala bora,
demokrasia na ushirikishaji wa watu wake wakati wa kufanya uamuzi
unaogusa maisha yao ya kila siku.
Alisema kuwa Tanzania ni nchi ya mfano linapokuja
suala la uongozi bora na ndiyo maana imekuwa na amani na utulivu kwa
muda mrefu ikilinganishwa na nchi nyingi za Kusini mwa Jangwa la Sahara.
“Nchi nyingi za Afrika zinazoizunguka Tanzania
zimekuwa na matatizo ya vita vya wenyewe na hata ukosefu wa utawala
bora,” alisema Balozi Lenhardt ingawa alidokeza kuwa katika siku za
karibuni imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali kutokana na
matukio ya uvunjifu wa amani.
Balozi Lenhardt alisema sababu nyingine
inayomfanya Rais Obama kuja Tanzania ni kutokana na jitihada za Serikali
ya Marekani kutengeneza mazingira mazuri ya uwekezaji na kasi ya ukuaji
wa uchumi.
“Rais Obama anakuja kuunga mkono juhudi za
Watanzania katika kutengeneza mazuri ya uwekezaji lakini bila kusahau
kuwa kasi ya ukuaji wa uchumi wa Tanzania imeivutia Serikali ya
Marekani,” alisema.
Balozi Lenhardt alitaja sababu nyingine inayomleta
Rais Obama kuwa ni kuisaidia Tanzania kuendeleza fursa mbalimbali za
kujiletea maendeleo.
Alisema uendelezaji huo wa fursa una lengo la kuisaidia Serikali ya Tanzania kukabiliana na tatizo la umaskini.
Alisema Marekani ni moja ya nchi zinazoongoza kwa
kutoa fedha nyingi za misaada na akisema kwa mfano, mwaka 2012 pekee
ilitoa Dola 750 milioni.
Aidha, alisema nchi yake imekuwa ikitoa misaada
mingi kupitia Shirika la Millenium Challenge (MCC), ambayo imejikita
zaidi katika kusaidia sekta za umeme, maji na miundombinu.
Alisema Tanzania inaunga mkono jitihada za Serikali
kujitosheleza kwa chakula na inafadhili Mkakati wa Kukuza Kilimo Kusini
mwa Tanzania (SAGCOT).
“Tunaunga mkono mpango wa SAGCOT kupitia Mfuko wa
Rais wa Marekani unaoitwa `Feed the Future’ lengo likiwa kuifanya
Tanzania kupiga hatua katika kilimo,” alisema balozi huyo.
Sababu nyingine ya ujio wa Obama ni kuhimiza haja
ya Afrika kutayarisha viongozi wa kizazi kijacho. Ameanzisha programu ya
kuandaa viongozi wa kizazi inayoitwa `Young African Leaders Initiative’
na Watanzania watatu, Modesta Lilian Mahiga, Masoud Salim Mohamed na
Malula Hassan Nkanyemka walishiriki katika mpango huo na kukutana na
kiongozi huyo mwaka 2010.
“Rais Obama anataka kusaidia kuandaa viongozi wa kizazi kijacho wa Afrika kusimamia vizuri rasilimali za nchi,” alisema.
Tishio la China
Akizungumzia ushindani na China kuhusiana na fursa
za kuwekeza na kuvuna rasilimali za Afrika, Balozi Leinhardt alisema
hawana tatizo lolote na hilo kwani dhamira ya Marekani ni kusaidia
Tanzania kupiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi.
Rais wa China, Xi Jinping aliitembelea Tanzania
Machi mwaka huu na ujio wa Obama umetafsiriwa na baadhi ya watu kuwa ni
ushindani wa mataifa hayo mawili katika kusaka na kunufaika na
rasilimali za Afrika.
Balozi Lenhardt alieleza imani yao ni kuwa China
inadumisha urafiki na Tanzania kwa nia ya kuisaidia kuendelea... “Sisi
hatuna shida na China, kwani tunaamini wako kwa ajili ya kusaidia.
Ilimradi tu wawe na dhamira safi katika kuwasaidia.”
Alipoulizwa kama ziara ya Rais Obama ina lengo la
kusaka fursa ya kuvuna rasilimali za Tanzania, balozi huyo aliwataka
Watanzania kuacha kuwa na wasiwasi wa kuporwa rasilimali zao.
“Watanzania ni watu wapole na wakarimu ila mna
tatizo moja la kuhofia kila jambo. Kila kitu mnachofanyiwa mnaona kuna
baya linakuja. Sisi tuna nia njema ya kuwasaidia kuendelea.”
source:mwananchi
source:mwananchi
No comments:
Post a Comment