Na Calvin Kiwia
Dar es Salaam. Taifa Stars leo ina kazi moja tu ya kutimiza dhamira ya miaka mingi kucheza fainali za Kombe la Dunia. Dhamira hiyo itafunguka zaidi kwa kuifunga Ivory Coast leo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam katika mchezo wa kusaka safari ya Brazil mwaka 2014.
Ni lazima ishinde mechi zake mbili za mwisho, ikianzia na hii ya leo dhidi ya vinara kwenye kundi lao, kisha ikisafiri kwenda Gambia nako wakapate ushindi. Lakini bado haitatosha, kwani wakati Stars ikisaka pointi sita katika mechi mbili, itaomba pia Morocco waifunge Ivory Coast katika mchezo wa mwisho. Hakuna linaloshindikana.
Akizungumzia pambano hilo jana, Kocha wa Stars Kim Poulsen alisema kulingana na maandalizi waliyofanya kabla ya mchezo huo, ni matarajio yake watacheza vizuri na kuhakikisha ushindi unapatikana.
“Kama mwalimu, nafikiri nimeifanya kazi yangu kwa asilimia 100. Matarajio yangu ni wachezaji watafanya yale yote niliyowapa kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri,”
“Najua tunacheza na timu ngumu na bora kwa bara la Afrika. Lakini hatupaswi kuwaogopa ingawa tunatakiwa kucheza kwa uangalifu mkubwa kwa kushambulia pamoja na kujilinda kikamilifu.”
Kim alieleza kuwa wanatakiwa kuwa makini zaidi katika dakika za mwanzo, kwani iwapo wataruhusu bao la mapema linaweza kuwachanganya vijana wake na kuwatoa mchezoni.
Aidha, amesema kukosekana kwa wachezaji watatu beki Aggrey Morris aliyelimwa kadi nyekundu mechi ya Morocco, Mrisho Ngassa anayemiliki kadi mbili za njano pamoja na John Bocco aliye majeruhi hakuwezi kuathiri timu hiyo kwani tayari amejazia wachezaji wengine.
“Nafasi ya Aggrey Morris atacheza Cannavaro (Nadir Haroub). Pia, natarajia kumchezesha Kazimoto (Mwinyi) katika nafasi ya Ngassa (Mrisho).” alieleza kocha huyo
Katika mazoezi ya Stars, Kim alikuwa akiwasisitiza wachezaji wake kutumia vizuri mipira ya kona pamoja faulo kujipatia mabao huku akimpa Kazimoto jukumu la kupiga mipira hiyo na kuwataka mabeki Cannavaro pamoja na Erasto Nyoni kuhakikisha wanatumia vizuri urefu na uzoefu wao kufunga mabao ya vichwa.
WACHEZAJI
Nahodha na kipa wa Stars, Juma Kaseja alisema
baada ya kumalizika kwa programu ya mazoezi Uwanja wa Taifa jijini Dar
es Salaam kuwa wamejifua vya kutosha na kuahidi kupigana hadi tone la
mwisho kuhakikisha wanashinda pambano hilo.
“Kwa upande wetu, nafikiri tumejifua vya kutosha. Kwa ujumla mchezo hautakuwa rahisi kwetu. Ivory Coast ni timu bora katika Bara la Afrika ina wachezaji wengi wanaocheza soka Ulaya,”
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi kuja kutusapoti. Naamini tuko vizuri na mwalimu ametupa mbinu nyingi. Tunawaahidi tutapambana hadi tone la mwisho kuhakikisha tunapata matokeo mazuri.” alisema Kaseja.
Beki Shomari Kapombe alisema: “Nafikiri tuko sawa kimwili na kiakili. Tunajua umuhimu wa mchezo huo. Kwa hiyo nafikiri hatuwezi kuzembea hata dakika moja. Kocha ametuelekeza mbinu nyingi za kuwamaliza Ivory Coast katika mazoezi. Nadhani kilichobaki ni kuzifanyia kazi,”
“Mashabiki wajitokeze kwa wingi, waje kufurahi. Tunawaahidi kuwa tutacheza vizuri pamoja na kuwapa furaha ya ushindi.
Beki wa kati Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema: “Mchezo utakuwa mgumu ingawa tumejipanga kwa hilo. Kama wachezaji tumejizatiti kwa hilo ingawa dua za Watanzania pia ni muhimu katika kufanikisha ushindi wetu.
Stars inashika nafasi ya pili kwenye kundi C ambalo linaongozwa na Ivory Coast yenye pointi 10, huku Morocco ikishika nafasi tatu na pointi 5, Gambia inakuruza mkia ikiwa na pointi moja.
KIKOSI
Kikosi kinaweza kuanza hivi: Juma Kaseja, Erasto Nyoni, Shomari Kapombe, Nadir Haroub, Kelvin Yondan, Frank Domayo, Amri Kiemba, Salum Abubakari, Thomas Ulimwengu, Mwinyi Kazimoto na Mbwana Samatta.
source:mwananchi
No comments:
Post a Comment