Rais wa Afrika kusini Jacob Zuma, amesema kuwa nchi yote inazidi kumwombea Mzee Nelson Mandela ili apate afueni haraka.
Rais huyo wa zamani amelazwa
hospitalini Pretoria, ambako anatibiwa maambukizi ya mapafu. Na Rais
Jacob Zuma anasema kuwa Nelson Mandela yuko katika hali mbaya sana
ingawa madaktari wameweza kudhibiti hali yake.
Katika taarifa yake Bw. Zuma amesema kuwa japokuwa Mandela ameathirika sana madaktari wanaomshughulikia wanafanya kazi nzuri.
Rais huyo mstaafu wa Afrika Kusini, amelazwa hospitalini kwa siku ya tano leo ambako anapokea matibabu ya ugonjwa wa mapafu.
Duru kutoka kwa ofisi ya rais Jacob
Zuma, zinasema kuwa Mandela mwenye umri wa miaka 94, yuko katika hali
mbaya ingawa imeweza kudhibitiwa.
Jamaa zake pamoja na aliyekuwa mkewe Winnie Madikizela-Mandela, walimtembelea hospitalini Jumatatu
Mwanawe Mandela Zenani (Mandela-Dlamini), pia alirejea kutoka nchini Argentina, ambako yeye ni balozi.
Serikali imekuwa ikisema kuwa hali ya Mandela inatia wasiwasi ingawa madaktari wameweza kuidhibiti.
Amekuwa katika chumba ya wagonjwa mahututi tangu kulazwa hospitalini Jumamosi kwa mara ya tatu mwaka huu.
Mwezi Disemba , bwana Mandela alilazwa hospitalini kwa siku 18 baada ya kupata maradhi ya mapafu,
Kumekuwa na taarifa za simanzi kwa
mara ya kwanza huku familia yake ikikusanyika kando yake, baadhi ya watu
wakisema kuwa ni muda wamwache Mandela aende zake.
Bwana Mandela, mwenye umri wa miaka
94, alipelekwa hospitalini mapema Jumamosi , ikiwa ni mara ya tatu
kulazwa hospitalini mwaka huu.
Kwa mujibu wa duru za urais, Mandela
amekuwa akiugua kwa muda mjini Johannesburg baada ya kukumbwa tena na
ugonjwa wa mapafu. Msemaji wa serikali Mac Maharaj amesema kuwa maafisa
katika hospitali wanataka kudhibiti idadi ya watu wanaozuru hospitali
hiyo ili wampunguzie bwana Mandela usumbufu.
Alilazwa hospitalini baada ya hali yake kuwa mbaya zaidi mnamo Jumamosi.
Kwa mujibu wa taarifa za urais, Rais
President Jacob Zuma, amerejelea wito wake kwa watu nchini Afrika Kusini
kumuombea Madiba wakati huu anapougua.
Lakini mwandishi wa BBC mjini
Pretoria, Karen Allen, anasema kuwa kuna matumaini madogo kuwa Mandela
aliyeongoza vita dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi, huenda akapona.
Anasema kuwa wengi walipata matumani
baada ya bintiye Mandela Zindzi, kusema kuwa babake yuko salama na kuwa
anaendelea kupata nafuu.
Mkewe Mandela Graca Machel, alifutilia mbali, ziara yake mjini London Jumamosi ili kuwa kando ya mumewe.
Mandela alikuwa Rais wa Afrika Kusini kati ya mwaka 1994 hadi 1999.
Alifungwa jela miaka 27 na anaaminika
kuwahi kuugua ugonjwa wa mapafu alipokuwa akifanyishwa kazi ngumu katika
machimbo ya mawe akiwa jela.
Chanzo: bbcswahili
No comments:
Post a Comment