Na Ndyesu Florian
Kwa hakika sielewi ni mdudu gani huyu ambaye
atakuwa amewaingilia kiasi cha kuwasumbua vichwani wawakilishi wetu
hawa wa wananchi kama maana ya wabunge.
Kwa baadhi ya wabunge hasa wale ambao siku zote ni makini, wanaotimiza wajibu wao ipasavyo, naomba mnivumilie niseme.
Siku zote nimekuwa nikijiuliza na kutafakari, hivi dawa ya vurumai hizi zote ambazo zimetokea bungeni kule Dodoma ni ipi?
Nimefika mahali nikafikiri kuwa ingefaa siku moja
uongozi wa Bunge uagize wataalamu wa afya wafike mahali hapo, wawapime
akili wabunge wetu ili tuone kama wapo wenye kasoro, wasaidiwe.
Mifano ipo mingi ya matukio mengi ambayo
yanaonyesha kasoro miongoni mwa wabunge wetu, kiasi cha kumfanya mtu
makini ajiulize, kulikoni katika chombo hiki?
Nianzie kidogo kwenye vurumai zilizotokea bungeni mjini Dodoma siku ya Alhamisi, Mei 30, 2013.
Tofauti na nyakati nyingine ambako wahusika
walikuwa wabunge wa chama tawala, CCM dhidi ya wale wa upinzani, safari
ni baina ya wabunge wa upinzani.
Vurumai hizo ziliwahusisha wabunge wa Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) dhidi ya wale wa CUF wakati ule wa
hotuba ya kambi ya upinzani kwenye mjadala wa Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe.
Ni muda mfupi baada ya kumaliza wajibu wake wa kuwasilisha hotuba yake ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2013/14.
Akiwasilisha hoja za upinzani, Hezekiah Wenje,
Mbunge wa Nyamagana (Chadema) akawakera wenzake wa CUF kwa maneno ambayo
si vizuri kuyarejea hapa.
Bila subira, wabunge wa CUF wakaanza kujibu
mapigo, tena kwa maneno makali, kauli nzito ambazo licha ya Naibu Spika,
Job Ndugai kujaribu kuwatuliza haikuwa, ndipo mkutano wa Bunge
ukavunjika, Bunge likaahirishwa kwa muda.
Ndugai akalifikisha suala hilo kwenye Kamati ya
Uongozi ya Bunge ambayo jioni ikatoa karipio kwa pande hizo mbili, jambo
ambalo hata hivyo halikusaidia kumaliza msuguano huo na Bunge
likaahirishwa kwa mara ya pili.
Mlolongo huu wa matukio hayo kwa mara nyingine umetia doa au
chumvi katika kidonda kibichi cha sifa mbaya ambayo chombo hiki au
mhimili huu wa dola tayari umekuwa nayo.
Niseme wazi kwamba siku zote ni uungwana kwa mtu
kuomba radhi, ndiyo maana ninakubaliana na hatua ambayo viongozi
waandamizi wa vyama hivyo wamechukua.
Kauli za Freeman Mbowe (Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni) kwamba waliwaumiza CUF na yule wa CUF, Rashid Alli
Abdallah, mnadhimu wa chama hicho, aliposema kwamba walighafirika kwa
lugha isiyofaa, zote zimesikika, sina shaka kwamba zimekubalika.
Hata hivyo, hili la kuomba radhi kwa viongozi hao
baada ya vurumai hizo na maji kumwagika, kwa mara nyingine zimetoa picha
mbaya kwa chombo hiki.
Kauli hizi ndizo zinazotuacha wanajamii na hasa
wafuatiliaji wa karibu wa mijadala ndani ya Bunge letu tukiwa na maswali
mengi ambayo ni zaidi ya majibu. Yote haya yanatia doa uadilifu wa
chombo hiki.
Ninajiuliza, picha hii inayotolewa na wabunge wetu inawafanya Watanzania wakiamini tena chombo hiki?
Wawakilishi wetu hao kila mmoja tangu aingie humo mwaka 2010 anaufahamu vizuri wajibu wake katika kuitumikia jamii?
Zile semina elekezi walizopewa mwaka 2010 baada ya
kuchaguliwa au kuteuliwa kwa viti maalumu au kuteuliwa na Rais,
zimewasaidia kiasi gani.
Ina maana kuwa wamezisahau haraka kanuni hizo zinazosimamia chombo hiki au hata mchezo huo wanaoucheza?
Mbunge wetu anazifahamu vizuri kanuni, taratibu zote, ni kwa kiasi gani anajitahidi katika kuzitimiza au kuziishi?
Pia, wajibu wa spika au kiti chake katika kusimamia kanuni hizi na hata nidhamu katika Bunge unaheshimiwa kwa kiasi gani?
Kama hauheshimiwi, wabunge wetu wote wanataka
kutuonyesha kuwa wamekwenda katika jumba hilo la kifahari, lakini bila
kujua vizuri wajibu wao?
Ni kweli kwamba mbunge wetu anaweza kufanya chochote kile anacholipenda, tena bila kujali athari zake mbele ya jamii?
Pia, ni picha gani inayotolewa na wabunge wetu
mbele ya jamii kila wanapoamua kushambuliana, kutukana au kutoleana
maneno makali, kejeli na mambo kama hayo?
Wabunge wetu wamesahau kuwa wanaonekana laivu
mbele ya runinga au vyombo vingine ambavyo vinaonyesha mijadala ya Bunge
inayoendelea Dodoma?
Maswali machache hayana budi kujibiwa na wabunge wetu kwa sasa.
Hata hivyo, ninapojaribu kutafuta majibu ya
maswali haya ninakwama na matokeo yake ninapokutana na tatizo la msingi
la umakini na uthabiti wa kiti cha spika.
Ninajiuliza, hivi kweli kiti kinapwaya, nini
sababu za kupwaya kwake, ni kanuni au taratibu zote zinazotungwa
kusimamia chombo hiki zimeshindikana kutelekezwa au kufuatiliwa?
Huenda ziliandaliwa kanuni hizi bila kujiuliza maswali ya endapo zinatimiza azma iliyokusudiwa.
Tatizo la msingi ninaloliona ni utoto uliofichwa
kwenye ushabiki wa kisiasa uliojengwa na kuendekezwa mno na wabunge
wetu. Huo ndiyo unaosababisha vurumai kama hizi za kawaida kule Dodoma,
zinazochekewa zikaachwa zipite.
Wasiwasi wangu ni kuwa wengi wa wabunge wetu
hawajitambui kwamba ajira zao hudumu kwa miaka mitano na kwamba mkataba
wao na waajiri wao, wapigakura unamalizika baada ya muda huo.
Huenda jukumu la msingi la kutunga sheria ambalo
Bunge letu linafanya, pia lile la kuisimamia Serikali halionekani
machoni mwa wabunge wetu wengi.
Matokeo yake, kila wanapopata nafasi basi hulipuka wapendavyo.
Nimshauri Ndugai au uongozi wa Bunge watambue
wajibu wao wasichoke kwamba wanaandamwa mno na vyombo vya habari kila
wanapokunjua makucha, husemwa.
Kama kanuni zipo, hazisimamiwi, hatua hazichukuliwi, ruhusa za wabunge kuacha vikao zimezidi, wengi huonekana mitaani wakiranda, wakihubiri siasa, kufanya mikutano ya hadhara wakati Bunge likiendelea. Kiti cha spika kichukue hatua, siyo kukaa kimya..
source: mwananchi
Kama kanuni zipo, hazisimamiwi, hatua hazichukuliwi, ruhusa za wabunge kuacha vikao zimezidi, wengi huonekana mitaani wakiranda, wakihubiri siasa, kufanya mikutano ya hadhara wakati Bunge likiendelea. Kiti cha spika kichukue hatua, siyo kukaa kimya..
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment