WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Wednesday, June 26, 2013

SHIVJI : Serikali tatu zitakuwa tegemezi,dhaifu

 
 


Rasimu ya Katiba Mpya inaendelea kuibua mambo na hisia mpya. Safari hii aliyevunja ukimya ni Mhadhiri mstaafu na mwanasheria maarufu nchini, Profesa Isaa Shivji.

Profesa Shivji anazungumzia sehemu muhimu ambazo zimegusa makundi mbalimbali katika rasimu hiyo, kama vile muundo wa Muungano, ambapo anasema ule wa Serikali tatu unaopendekezwa ni tegemezi na dhaifu.

Anasema mfumo huo, haujawekewa nguvu ya kikatiba ya kuulinda na kuupa mamlaka thabiti.
Shivji ambaye alikuwa anaagwa kama Mwenyekiti wa Kigoda cha Mwalimu Nyerere, anasema muundo huo mpya unaweza kusababisha kuzuka kwa migogoro mingi na mikubwa itakayovunja Muungano.

 “Huu muundo ingekuwa sahihi zaidi kama mtu atauita kuwa muundo wa dola tatu badala ya Serikali tatu kama rasimu inavyoeleza, kwa sababu tunaona Serikali zote tatu zina mihimili mikuu mitatu ya dola – Bunge, Mahakama na Serikali,” anasema.

Anaonya kuwa iwapo Rasimu hiyo itakubaliwa bila mabadiliko makubwa, itasababisha kuvunjika kwa Muungano.

Angalizo la Prof. Shivji, limekwishatolewa na Chama cha Mapinduzi ambacho kinaendelea kushikilia sera yake ya Serikali mbili na makundi mengine mbalimbali. Hata hivyo, yapo makundi mengine, kikiwamo Chama cha Demokrasia na Maendelo ambayo yamefurahishwa na muundo unaopendekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.

Akifafanua hoja yake, Profesa Shivji anabainisha kuwa rasimu hiyo imekosa maelezo ya wazi na thabiti kuhusu ukuu wa Katiba ya Muungano, juu ya Katiba nyingine za washirika wa Muungano.

“Hali hii itasababisha migongano na kutoelewana kati ya mamlaka za washirika wa Muungano na mamlaka ya Jamhuri ya Muungano.

Anasema Ibara 8, ya rasimu hiyo inayozungumzia ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano inaeleza kuwa “ukuu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano utakuwa katika mambo ya Muungano tu na si vinginevyo”.

“Ukisoma rasimu hii ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika Ibara ya 8(1) inasema na hapa nitanukuu: “Bila ya kuathiri masharti ya Katiba za washirika wa Muungano kwa mambo yasiyo ya Muungano, Katiba hii itakuwa sheria kuu katika Jamhuri ya Muungano”.

Kwa hiyo Ibara hii inaeleza kuwa Katiba inayopendekezwa haitakuwa na nguvu za kisheria juu ya Katiba za washirika wa Muungano,” alisema Shivji.
Anasema Katiba zote za nchi zinazofuata muundo wa shirikisho kama unaopendekezwa na Tume, zikiwemo za Marekani na Australia, zina vipengele vinavyoeleza wazi kuwa katiba ya shirikisho ni sheria kuu juu ya katiba za washirika ambayo inaondoa mianya ya kuibuka kwa migongano kati ya mamlaka za shirikisho na washirika wao.

“Nadhani masharti mengi ya Rasimu na muundo wake mzima ni matokeo ya mivutano mikali katika Tume,” anasema na kuongeza:

“Bahati mbaya hatuna mwenendo wa majadiliano ya Tume wala taarifa yao rasmi, … lakini usomaji wangu wa awali unaniambia kwamba Rasimu hii ni maelewano (compromise), na sio mapatano, au mwafaka, kwa maana ya consensus.”

Anasema katika maelewano pande zinazokinzana hatimaye hukubali kwa shingo upande ili kutokukwamisha uamuzi ambapo pande zote zinapata kidogo na kupoteza kidogo, na kila upande huwa na mkakati wake wa kupata zaidi katika duru ya pili.
Anaongeza kuwa vile vile, maelewano hayo ya pande mbili kamwe hayawezi kuwa kwa moyo safi.

“Maelewano au compromise, yanazaa uamuzi legelege, mapatano au consensus, kwa upande mwingine, ni maafikiano yanayofikiwa baada ya mjadala mrefu, kila mmoja akilenga kuthibitisha hoja yake na kwa njia hii kusadikisha wenzake kwamba hoja yake ni sahihi. Baada ya kufikia uamuzi wa mwafaka, kila mmoja anatoka akiwa ameridhika na amefurahi. Katika compromise, kila mmoja anatoka amenuna,” anasema.

Profesa Shivji anasema Rasimu ya Katiba inasema hati ya Makubaliano ya Muungano iliyorejewa katika ibara ndogo ya (1), ndio msingi mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Katiba kwa kadri itakavyorekebishwa, itakuwa ni mwendelezo wa makubaliano hayo.

“Ukiangalia kwa jicho la kisheria,  ukisema hati ndio msingi, maana yake ni kwamba hati bado inaendelea kuwa na nguvu ya kisheria na ndio sheria kuu inayotawala Katiba…. Lakini hati iliweka Serikali mbili; sasa iweje rasimu inayozungumzia Serikali tatu iwe na msingi ambao ulijengeka kwenye Serikali mbili?” anahoji.

Anaongeza kuwa huenda Tume hiyo iliyosheheni wanasheria wazoefu na waliobobea, walijua na kuelewa walichokuwa wanaandika na haiwezekani walikosea au kuteleza, isipokuwa walichokifanya ilikuwa ni ‘kusalimu amri’ na ‘kuelewana’ ili  mambo yaendelee.

“Ndivyo tulivyopata ibara legelege ambayo kisheria haina kichwa wala mkia, ibara kama hii isiyoeleweka inashusha hadhi ya Katiba. Inawezekana kabisa kwamba ibara hii isiwe na madhara makubwa kwa sababu majaji wenye busara hawatatia maanani sharti kama hili. Lakini unaweza kupata jaji ambaye anaegemea zaidi kwenye ufundi na kuitafsiri ibara hii kama ilivyo, na madhara yake yanaweza kuwa makubwa.

Eneo la washirika
Katika mfano mwingine aliouita mzito zaidi, alisema ni kuhusu mipaka ya madaraka ambapo eneo la utawala wa Serikali ya Shirikisho limetajwa kuwa ‘eneo lote la Tanzania Bara ikijumuisha sehemu yake ya bahari na eneo lote la Zanzibar ikijumuisha sehemu yake ya bahari, wakati eneo la utawala wa Serikali ya Bara na Serikali ya Zanzibar halikutajwa.

Anasema pande mbili za Muungano zimewahi kutofautiana kuhusu eneo lao la bahari, hasa kwa sababu inadhaniwa kwamba bahari inayopakana na maeneo ya Tanganyika na Zanzibar ina mafuta na rasilimali nyingine.

Anasema ukimya wa Rasimu juu ya kueleza kwa uwazi mipaka ya utawala wa Washirika ni wa ajabu kwa sababu huwezi kuzungumzia utawala wa mamlaka yoyote yale bila kubaini mipaka yake, anabainisha kuwa ukimya huo unaweza kuzaa migogoro.

Profesa Shivji anasema magwiji wa Katiba wanaafiki kwamba mfumo wa shirikisho una angalau sifa kadhaa –mwananchi anatawaliwa na serikali mbili, yaani serikali ya shirikisho na serikali ya mshirika; na kuna mgawanyo wa madaraka miongoni mwa serikali, na katiba/sheria zao zina hadhi sawa; na kuwa Katiba ya Shirikisho ni Sheria Kuu (supreme law).

Je, Rasimu inakidhi sifa hizi? Kwa maoni yangu, kwa kiasi kikubwa kila mwananchi wa pande zote mbili atatawaliwa na Serikali mbili; Wabara watatawaliwa na Serikali ya Shirikisho na Serikali ya Bara, Wazanzibari watatawaliwa na Serikali ya Shirikisho na serikali ya Zanzibar. Pia kuna mgawanyo wa madaraka kati ya serikali tatu,” anasema.

Anasema kwa msingi huo, washirika, yaani Bara na Zanzibar watakuwa na hadhi sawa  lakini akasema sifa inayotatanisha ni ya mwisho, ile inayosema Katiba ya Shirikisho ni Sheria Kuu.

Akielezea dhana ya Ukuu wa Katiba Shivji anasema ni sheria zote, madaraka, majukumu na mamlaka yanatokana na Katiba, na Katiba ndio chanzo cha uhalali wa utawala.

Anaongeza kuwa Katiba yenyewe inapata mamlaka yake kutoka kwa wananchi katika ujumla wao. Ndiyo maana, katika msamiati wa kawaida, tunasema katiba ni sheria mama.

“Nikitumia msamiati huo kwa katiba ya shirikisho, naweza nikasema kwamba katiba ya shirikisho ndio mama na baba wa shirikisho. Katiba na sheria za washirika, ingawa zina mamlaka kamili katika maeneo yao, zinatokana na katiba ya shirikisho na zinapata uhai wao wa kisheria kwa mujibu wa katiba ya shirikisho.

Anasema kwa kawaida ukitaka shirikisho liwe imara na liwe na nguvu, basi hakuna budi Washirika wakubali kutambua na kutii masharti ya Katiba ya Shirikisho vinginevyo shirikisho litayumba na kutakuwa na migogoro kutokana na vipengele vya katiba na sheria na vitendo vya vyombo vya washirika kukinzana na kugongana kila mara.

Ukuu wa Katiba

Akisisitiza juu ya ukuu wa katiba, Shivji anasema Ibara ya 61(4) inasema ‘Washirika wa Muungano watatekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii na Katiba zao”.

“Wanasema ‘Kuzingatia’ sio kubanwa; Kiingereza chake ni ‘to take account of’, ‘to bear in mind’. Hii ina maana unaweza ukazingatia masharti ya Katiba ya Shirikisho, na baada ya hapo ukatenda kinyume chake, lakini hata hivyo utakuwa hujavunja Katiba” anasema.

Anasema hii inaeleweka zaidi ukisoma ibara ndogo inayofuata inayotaka Washirika kutekeleza majukumu yao kwa masuala yasiyo ya Muungano ‘kwa mujibu’ wa masharti ya katiba zao.

“‘Kwa mujibu inaleta maana ya kubanwa, huwezi ukakiuka. Kwa hivyo, masharti ya Katiba ya Shirikisho yanakushawishi; masharti ya Katiba ya Mshirika yanakushurutisha.”

Anaielezea Ibara 109 (5) kuwa inasema ‘bila ya kuathiri’ kutumika kwa Katiba ya Tanzania Bara na Katiba ya Zanzibar, Katiba hii itakuwa na nguvu ya sheria katika Jamhuri ya Muungano kwa mambo yanayohusu Muungano na endapo sheria nyingine yoyote itakiuka masharti yaliyomo katika Katiba hii, basi sheria hiyo nyingine, kwa kiasi kinachokiuka Katiba hii, itakuwa batili.

“Kuna dhana mbili zilizotumika katika kipengele hiki: ‘mambo yanayohusu’ (Muungano) na ‘sheria’. Bila shaka ‘mambo yanayohusu Muungano’ ni dhana pana zaidi kuliko ‘mambo ya Muungano’. Mambo ya Muungano ni yale saba yaliyotajwa katika nyongeza…Mambo yanayohusu Muungano ni hayo saba pamoja na yale yote yaliyozungumziwa katika Katiba ya Shirikisho,” anasema

Anaongeza kuwa kwa mantiki hiyo hiyo, neno ‘sheria’ haliwezi likawa na maana pana zaidi ya sheria inayohusu mambo ya Muungano inayotungwa na Bunge la Shirikisho kwa mujibu wa ibara 109.

Kwa hivyo, ukuu wa Katiba ya Shirikisho unaozungumziwa katika ibara hii ni juu ya shughuli za Muungano tu, na kuwa sheria yoyote juu ya mambo yanayohusu Muungano ikikiuka masharti ya Katiba ya Shirikisho, sheria hiyo ni batili. Lakini hii haihusu katiba na sheria za Washirika.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment