WIKI hii nitakamilisha (kwa muda)
mjadala unaohusu matukio yaliyoikumba sekta ya elimu hivi karibuni, lakini
wakati wote najua kwamba masuala ya elimu siku zote yataibuka katika safu hii
kwani hayaishi na kwa jinsi tunavyoyashughulikia yanaelekea yataendelea kujitokeza
kwa ukali zaidi.
Ni kweli kwamba sakata la hivi karibuni
la sehemu moja ya utawala kutangaza kwamba watoto wa shule wameshindwa vibaya
na sehemu nyingine kuamua kubadilisha taratibu za kupima matokeo ili washinde
ni dalili za ugonjwa na sio ugonjwa wenyewe.
Ugonjwa wetu ni mkubwa kuliko
tunachokiona na tunachokizungumza kwa jazba na sauti kali, na huu ni ugonjwa
ambao anayetaka kuufuatilia kwa makini ataugundua katika kila medani ya maisha
yetu. Iwe ni elimu, au kilimo, au viwanda, au afya, au maendeleo vijijini, au
hata michezo, tumekuwa ni watu wa kutafuta urahisi wa majibu katika hali ngumu.
Kwa kufanya mabadiliko katika utaratibu
wa kupima matokeo watawala wetu wanataka tuamini (na wao nadhani wanaamini)
kwamba elimu yetu haina tatizo, ni elimu bora kabisa, na kwa hiyo hatuna sababu
ya kuhamanika wala kuchukua hatua zozote za dharura. Hawa ndio akina Pangloss
niliowahi kuwasuta katika safu hii.
Sote tunajua, hata kama baadhi yetu
wangependa kujifanya wamesahau, kwamba tafiti mbalimbali zimetuonyesha kwamba
watoto wetu katika shule nyingi hawafundishwi (na hawajifunzi) kwa kiwango
kinachotakiwa, na kwamba wengi wao wamekutwa wakiwa nyuma kwa miaka mitano au
sita ya darasa walimokutwa.
Sasa tunashangaa nini tunapoambiwa
kwamba watoto wa aina hiyo, wanapofika hatua ya kutahiniwa, wanafanya vibaya?
Tungetakiwa tushangae kama tungeambiwa kwamba wamefaulu. Wanaoshangaa kwa haki
ni wale wazazi wanaokwenda shuleni kuwaaambia walimu wa watoto wao kwamba
haiwerzekani kwamba watoto wao wamepasi kwa sababu wao (wazazi) wanajua kwamba
watoto hao hawajui kitu na hawawezi kufaulu.
Tumeambiwa mara kadhaa kwamba
anayeficha ugonjwa ataumbuliwa na kilio, lakini tumeamua kuwa mabingwa wa
kuficha magonjwa yetu, tena magonjwa ya hatari kama hili la ujinga. Kwa hatua
za “fasta-fasta” zilizochukuliwa majuzi, hili la elimu ni kama limekwisha,
tutalisahau hadi utakapotokea mlipuko mwingine. Na utakapotokea tutachukua
hatua nyingine za “fasta-fasta” huku tukijua (au tukitakiwa kujua) kwamba
“fasta-fasta” ya awali haikutusaidia.
Tumekuwa watu wa hivyo; hatuna
mustakabali wa pamoja kwa sababu kila mmoja wetu anajijengea mustakabali wake,
yeye na familia yake. Inaelekea sote tunaelewa umuhimu wa elimu bora kwa watoto
wetu, na ndiyo maana kwamba tunawekeza fedha nyingi katika kuwasomesha katika
shule tunazoziona kama shule bora, mara nyingi kwa sababu watoto wakienda huko
wanafanywa kuzungumza kimombo kuliko wazazi wao, na kwetu hiyo ndiyo elimu!
Tatizo ni kwamba ni wachache wetu
wanaoweza kumudu shule hizo za gharama kubwa, na watoto walio wengi wanaendelea
kusoma katika shule ambazo siyo tu haziwafanyi wazungumze ung’eng’e bali hawana
lolote wanalojifunza, hata kusoma, kuandika na kuhesabu kwa kiwango cha msingi
tu. Na hawa ndio Watanzania wa kesho!
Nilikwishakulisema hili, lakini nitalirejea,
wakati hawa wazungumzaji wa ung’eng’e wasiojua kitu watakapofika madarakani
wakichukua nafasi za wazazi wao waliowasomesha ung’eng’ewa kuwasaidia kuzidi
kuiuza nchi, wenzao wasiosoma ung’eng’e wala kitu kingine chochote watawagomea,
na kutatokea vita. Kutakuwa na matabaka yasiyovumilika na katika hali kama hiyo
hapatakalika.
Ni kweli kwamba wengi wa watawala
wanapochukua uamuzi wa kijinga kama huu wa kubadilisha vipimo vya mitihani
wanawapeleka watoto wao kusoma katika shule ambazo wazazi wa kawaida
hawazimudu. Kwa maana hiyo hawa ni wazazi wasio kuwa na uchungu na shule
wanazoziamulia. Kwa nini wajali wakati watoto wao wanasoma kwingine?
Hebu tuambizane tena: hakuna jambo
muhimu kwa watoto wetu kama elimu bora katika kuwafanya wawe binadamu bora na
raia wema. Mifano inajionyesha yenyewe. Watoto wa matajiri na wakuu wa serikali
na watoto wa masikini na ambao wazazi wao hawakuwa na vyeo serikalini
wamejikuta wote ni sawa kwa sababu walisoma shule zinazofanana na walipata
elimu inayofanana.
Huo ulikuwa ni wakati ambapo wazazi
waliokuwa serikalini walifanya muamuzi wa wa kuzifanya shule za umma zitoe
elimu iliyokuwa bora kwa kiasi kilichowezekana, na watoto wao walisoma katika
shule hizo.
Huu ulikuwa ni wakati ambapo wazazi
wenye uwezo, au vyeo serikalini, waliwaondoa watoto wao kutoka shule binafsi na
kuwaingiza katika shule za umma kwa sababu walikuwa na imani na shule za umma
kuliko shule binafsi.
Kwa jinsi hii watoto walio wengi wa
Taifa hili walikuzwa katika mazingira ya udugu. Leo hii hili halipo tena, na
huko tuendako, kama si kesho ni kesho kutwa, gharama zake zitakuwa kubwa mno.
Ningependa kutoa ushauri kwamba tuache
mtindo wa kupaukia masuala, tuachane na mtindo wa kuendesha kila kitu kwa
dharura. Kama ninavyosema kila mara, hakuna mahali pengine tunakokwenda, kwani
hapa ni kwetu, tumefika, na tunatakiwa tujenge maskani yetu ya kudumu hapa.
Kama hiyo ni kweli, tunatakiwa tuketi
chini kama Taifa la watu wenye akili, tutafakari suala la elimu kwa mapana na
marefu, historia yetu katika medani hii; tuangalie tulipokosea ni wapi na nini
tulitakiwa tufanye; tuwaangalie wenzetu waliofanikiwa na tujifunze kutoka kwao.
Jambo la kwanza la kuwekeza katika
kutafuta ufumbuzi wa matatizo yetu katika medani ya elimu ni tafakuri pevu, na
wala si fedha. Umakini, fedha zitahitajika, lakini jambo la kwanza, jambo la
msingi, jambo la awali kabisa, ni fikra zitakazotuelekeza jinsi ya kuenenda na
jinsi ya kuwekeza fedha zetu kwa busara.
Tukiishakuelewana ni nini tunataka
kufanya, ndipo tutakapoweza kuangalia rasilimali kiasi gani tuwekeze katika
elimu ya watoto wa Taifa hili. Tunaweza kukopa kwa niaba yao, na hawatakuwa na
kinyongo wakija kujua kwamba madeni wanayotakiwa kuyalipa ni fedha zilizowapa
elimu sawa na watoto wa Korea na Singapore.
Tunaweza kuzithamanisha rasilimali zetu
na utajiri tunaoambiwa kwamba tunao, kama ni dhahabu, gesi, mafuta, misitu na
utajiri mwingine na sehemu maridhawa ya fedha zinazotokana na rasilimali hizo
ikawekezwa katika elimu ya watoto wetu.
Yapo mambo mengi ambayo tunaweza
kufanya, mambo ambayo tunatakiwa kuyafanya, ili kulinusuru Taifa hili dhidi ya
janga la ujinga. Jambo moja ambalo najua kwa hakika hatutakiwi kulifanya ni
kuendelea jinsi tunavyofanya mambo yetu, hovyo hovyo.
Source:
www.raiamwema.co.tz: Jenerali
Ulimwengu
No comments:
Post a Comment