Na Maggid Mjengwa,
MABADILIKO makubwa yamefanyika katika nchi yetu kwa mujibu wa Rasimu ya Katiba Mpya iliyozinduliwa wiki hii.
Haya ni mabadiliko makubwa kuwahi
kufanyika tangu mwaka 1977. Ni mwaka ambao Katiba ya Jamhuri ya Muungano
ya Tanzania ilifanyiwa marekebisho makubwa. Mwaka huo wa 1977
yalifanyika mabadiliko makubwa pia kwenye uongozi wa Chama cha Mapinduzi
(CCM) na hata ndani ya mfumo wa uongozi wa Serikali.
Naam, katika dunia hii, mabadiliko ya
kijamii hupelekea mabadiliko ya kisiasa. Na Wanasholojia wanasema zipo
sababu mbili zenye kupelekea mabadiliko hayo. Sababu za ndani ya jamii
husika (endogenous) na sababu za nje ya jamii (exogenous).
Kwa upande wetu, tunaona kwamba sababu za ndani na za nje, kwa pamoja, zimesukuma
kwenye kufikia hatua hii ya kufanyika mabadiliko haya makubwa ya Katiba.
Na kwa jamii yetu kwa upana wake, ina
sababu za msingi za kuyafurahia mabadiliko haya, maana, ni sawa na
mwanadamu aliyepewa kikombe chenye nusu ujazo wa maziwa.
Utafahamu kama amefurahia au
amechukizwa kwa namna atakavyochagua kukielezea kikombe kile anayekiona
ni ‘kikombe nusu cha maziwa’ anaonyesha kutoridhika, na anayekiona ni
‘kikombe kilichobaki nusu tu kujaa’ huyo amekifurahia na anaonyesha
matumaini kuwa iko siku kitajaa. Inahusu kuwa na matarajio chanya
(optimism) na kuwa na matarajio hasi (pessimism).
Binafsi, nichukue fursa hii
kuwapongeza Wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kazi yao njema
iliyotufikisha kwenye hatua hii ya kuwepo kwa Rasimu ya kwanza ya
Katiba. Lakini, mwingine wa kupongezwa kwa ujasiri wake mkubwa wa
kiuongozi, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Historia itamkumbuka Rais Kikwete kwa
ujasiri wake wa kuachana na fikra za ukale na kuwa tayari, kwa mara ya
kwanza katika historia ya nchi hii, kukaa meza moja na makundi yote,
wakiwemo wapinzani wa chama chake kujadili mustakabali wa nchi yetu.
Maana, hili la Katiba halihusu
mustakabali wa chama cha siasa, bali mustakabali wa nchi yetu. Vyama vya
siasa vinakuja na kuondoka, lakini nchi yetu itabaki pale pale. Leo
unaweza kuwa kiongozi wa chama fulani, lakini, mtoto wako au mjukuu
wako, akaja kuwa mwanachama au kiongozi wa chama tofauti na chako.
Kwa ujasiri wa kuongoza mchakato huu
wa Katiba, na kimsingi mabadiliko makubwa kwa maslahi ya taifa, Rais
Kikwete anatupitisha kwenye ‘Jakaya-stroika’ ya kwetu wenyewe, maana,
kimsingi, mabadiliko mengi makubwa ya kimfumo, kiuchumi na kijamii,
yanakuja kufuatia Katiba Mpya inayokuja.
Na katika dunia ya sasa, hakuna
anayeweza kuyazuia mabadiliko yanayotokana na msukumo wa ndani ya jamii.
Kwa mfano, Urusi ya zamani kule, Mikhael Gorbachev alipoanzisha mageuzi
makubwa ya kisiasa, kiuchumi na kijamii katika Urusi, watu wake
hawakuamini walichokiona.
Gorbachev aliuona wakati uliobadilika.
Mabadiliko yale makubwa ya kimfumo kule Urusi yalipata majina mawili.
Perestroika na Glasnot. Perestroika ina maana ya ujenzi mpya wakati
Glasnot ni uwazi.
Kabla ya mageuzi yale makubwa, Urusi
ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la kuwepo na fikra za ukale na kukosekana
kwa uwazi. Jamii ilijawa hofu, mambo mengi yalikuwa ya kufichaficha.
Kulikuwa na usiri mkubwa!
Lakini, ndani ya kufichwa huko,
kulikuwa na harufu ya uoza mkubwa. Gorbachev, daima atakumbukwa kwa
kvunja ukimya na kuifanya Urusi kuwa nchi ya kisasa kama inavyoonekana
sasa.
Na kwa hakika, ‘kuzaliwa’ kwa Katiba
Mpya yetu, ni sawa na Taifa letu kujivua gamba. Maana, kujivua gamba
huku kama taifa, kunapaswa kuendane na kuanza kubadili mifumo yetu ya
kifikra. Tuanze sasa kufikiri juu ya malengo ya taifa, kwa maana ya
ndoto za taifa letu badala ya kutanguliza sana malengo ya vyama vyetu au
zaidi malengo binafsi ya vyeo na mamlaka.
Nchi yetu ni kama nyumba kongwe.
Tuendelee kwa umoja wetu kuifanya kazi ya kuikarabati upya nyumba yetu.
Ipate mwonekano mpya. Kuikarabati upya nyumba kongwe, huweza pia
kupelekea kuibomoa nyumba yenyewe.
Kutakuwa na fito na vipande vya
matofali vya kurudishia. Kutahitajika fito na matofali mapya pia. Ndiyo,
fito na matofali mengine yatakuwa ni ya kutupa tu, na ni lazima
yatupwe, basi. Na hapo utakuwa umeikarabati upya nyumba yako.
Maana, katika jamii, mabadiliko
yanapaswa yaendane pia na fikra mpya. Na jamii huingiwa na mashaka na
kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao
hawataki kabisa kuwaruhusu wengine kushiriki uongozi wa nchi.
Watu ambao bado miongoni mwao
wanaamini kwamba tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni
uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa. Sasa,
katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za
kiwendawazimu tu!
Nchi yetu inapita sasa katika kipindi
kigumu tangu tupate Uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na
hususan viongozi wa kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya
jazba, chuki na visasi. Hayo matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye
kuambukiza kwa haraka.
Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na
visasi vitawale siasa zetu. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna
mtu, kikundi au chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii
kuliko wengine wote.
Na kwa mwanadamu, lililo kubwa ni
uwepo wa matumaini. Na imani ya wananchi kwa taifa na viongozi wao, ni
shina la matumaini yao. Inakuwaje basi mwananchi anapokosa imani na
taifa, na hata kwa kiongozi? Katiba yetu iwe chachu ya kurudisha mioyo
ya uzalendo kwa taifa letu.
Mungu Ibariki Tanzania. ( Makala haya yamechapwa kwenye Raia Mwema wiki jana)
source:mjengwa blog
No comments:
Post a Comment