Katibu
Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad ametangaza
kushirikiana na Rais mstaafu wa Awamu ya Sita Zanzibar, Dk Amani Abeid
Karume kuhakikisha Zanzibar inapata mamlaka yake kamili.
Tamko hilo amelitoa wakati akihutubia
mkutano wa hadhara uliokuwa umebeba agenda ya kujadili mabadiliko ya
Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliofanyika kwenye uwanja
wa Kibandamaiti na kuhudhuriwa na wanachama wa CUF toka mikoa mitatu ya
Unguja.
Maalim Seif alisema mbali na Dk Karume
kazi hiyo pia itaendelea kufanywa na kamati ya maridhiano inayoongozwa
na Mwenyekiti wake Waziri wa zamani wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Hassan Nassor Moyo na Makamu wake Abubakari Khamis Bakari
wakiwemo wajumbe wanne.
Wajumbe hao ni pamoja na mjasiriamali Eddy
Riyami, mwakilishi wa Jimbo la Mji Mkongwe (CUF) Ismail Jussa Ladhu,
Aliyekuwa Waziri wa SMZ Mansour YusuF Himid, Mkurugenzi wa Uenezi na
Mawasiliano ya Umma wa CUF Salum Bimani.
Maalim Seif aliwaeleza wanachi kuwa Dk
Karume na Kamati hiyo hawatarudi nyuma hadi pale Taifa la Zanzibar
litakapopata uwakiklishi katika Umoja wa Mataifa na kuwa dola yenye
mamlaka kamili kama lilivyokuwa kabla ya Aprili 26,1964.
“Madai haya si ya Seif, Karume, Jussa,
Moyo au Eddy, ni sauti ya Wazanzibari wote bila kujali itikadi zao za
kisiasa, kwanini tusiwe na mamlaka yetu kamili, kudai haki ni wajibu
uliohimizwa na Mungu hivyo hatutakatishwa tamaa,”alisema Maalim Seif.
Alisema kwa upande wake yuko imara katika
kuitetea nchi yake na kwamba dola ya Zanzibar ni kongwe kuliko
Tanganyika, Malawi, Kongo, Rwanda, Uganda, Kenya na Burundi iliokuwa na
mabalozi wake katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.
Alisema kabla ya kukatwa kwa mipaka na
wakoloni mwaka 1884/1885 huko Berlin, Zanzibar ilikuwa ni Taifa kamili
lakini baada ya kukatwa kwa mipaka hiyo ikabakishiwa visiwa vya Pemba na
Unguja pamoja na maili kumi katika masafa ya usawa wa mwambao wa Pwani.
“Nitaendelea kushirikiana na Dk Karume,
Wazanzibari na kamati ya maridhiano hadi pale mamlaka kamili
yatakapopatikana, mimi ndiye Maalim Seif, nishazoea kufungwa, kutukanwa,
kunyanyaswa hivyo hakuna ninalolihofia katika kuipigania
Zanzibar,”alisema huku akishangiliwa na wananchi.
Akiizungumzia Tume ya Katiba ya Jaji
Joseph Warioba alisema ni muhimu kwa rasimu ijayo ya katiba mpya mambo
kadhaa aliyoyataja yakazingatiwa ili kuipa haki Zanzibar ya kuwa na
madaraka yake kamili ambayo yataisaidia kujijenga kiuchumi na kimataifa.
Akionekana kutia shaka ya wananchi wengi
kutopewa vitambulisho vya ukaazi na kuandikishwa kwenye daftari la
kudumu la wapiga kura, alimtaka Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein
kuwa mkweli na kutimiza ahadi yake ya kumpa kila Mzanzibari kupata haki
yake.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment