WAKATI mwingine unafikiria vitu vimefika pabaya; halafu vinaharibika
kabisa! Ni sawa sawa na uone gari lako linapasuka tairi na unajitahidi
kwa ufundi wote kuliegesha pembeni na unajua hili ni baya lakini
unashukuru Mungu kuwa angalau ni tairi tu utabadilisha.
Unapoegesha gari na kuanza kutoa tairi la akiba na jeki kabla
hujatulia rejeta ya gari inaanza kuchemka na moto unalipuka kwenye
injini na kabla hujafanya lolote moto unalipuka na kuanza kuteketeza
gari lako.
Ukiwa umekaa chini unasikitika maana hata kujaribu kuzima huna nafasi
simu yako inaita na unaambiwa mtoto wako kagongwa na gari amekimbizwa
hospitali! Kwenye Kiingereza wanasema when you think things are bad, they get worse!
Suala la udini Tanzania tumelizungumza na kufika mahali kujua kuwa
tuko pabaya. Tumeshuhudia kauli za ajabu na za kichochezi, hadi
tumefika tunagombea nani achinje na nani asichinje huku wengine
wakitaka Mahakama ya Kadhi iingizwe kwenye Katiba na wengine wakipinga.
Wakati hatujatulia tunaona video za kina Ilunga na wengine wakichochea
mauaji ya viongozi na waumini wa Kikristu.
Tukiwa bado tunatafakari hayo na tukiwa hatujatulia katika suala la
kuchinja na masuala mengine yenye harufu zote udini, Profesa Ibrahim
Lipumba mmoja wasomi mashuhuri wa Tanzania akaja na lake jipya.
Akizungumza kwenye Msikiti wa Idrissa Kariakoo jijini Dar es Salaam,
Prof. Lipumba amesikika akisema kuwa chama chake kilifanya kampeni ya
kidini ili kumsaidia Rais Jakaya Kikwete – Muislamu mwenzao ili asije
akaangushwa. Bila kumung’unya maneno Prof. Lipumba ambaye ni Mwenyekiti
wa Taifa wa Chama cha Wananchi (Wakiislamu?) amesema kuwa pamoja na
kuwa uchaguzi wa 2010 kutokuwa huru na wa haki yeye na wenzie ilibidi
watumie mbinu za ziada ili kuokoa “jahazi”.
Pamoja na kauli hiyo Prof. Lipumba ameonekana akiwagawa Watanzania
kwa misingi ya kidini upande mmoja wakiwepo Waislamu ambao licha ya
kumsaidia Kikwete kuupata urais hawakupata matunda yoyote hadi hivi
sasa na upande wa pili ni “wenzetu” ambao ni wazi akimaanisha ni
Wakristu. Prof. Lipumba akizungumzia hili amesema kuwa “Kwa hiyo kama
Waislamu tunataka kupata haki zetu, kama tunataka kuishi kama raia wa
daraja la kwanza katika nchi yetu, lazima tujipange kuelekea Uchaguzi
Mkuu wa 2015; na sisi tuanze kujipanga kwa sababu wenzetu wameanza
kujipanga, vinginevyo tutaendelea kubaki masikini na raia wa daraja la
nne katika nchi yetu wenyewe”
Prof. Lipumba amesema mengi sana kwenye hadhara ile kiasi kwamba
maswali makini yanahitaji kuulizwa ama kuhusu usomi wake na hekima
ambayo watu walitarajia kuwa nayo au amesema vile kwa sababu anajua
sasa hivi njia ya kutokea ni hii ya udini. Kwa mtu ambaye ametumikia
serikali (kama mshauri wa Rais) na kama mmoja wa wasomi kauli zake
ambazo nyingi zinaonesha dalili ya ujinga (siyo tusi) ni wazi ile imani
ambayo watu walikuwa nayo kuwa Prof. Lipumba ni msomi inabidi
kuangaliwa upya.
Ni usomi gani unaoweza kumfanya mtu kuwa mbaguzi wa wazi ambaye
anaiangalia jamii anayotaka kuiongoza kwa misingi ya “sisi dhidi ya
wao”? Hivi alipogombea urais mara nne alikuwa anataka kuwa Rais wa
Waislamu ili awape Waislamu maendeleo? Wakristu na wale wasio na imani
hizi mbili wangeishi vipi katika Tanzania chini ya Lipumba ambaye Sheikh
Basaleh akimtambulisha alimtambulisha kama “Rais mtarajiwa”? Kweli
Wakristu wanaweza kuwa salama chini ya mtu kama Lipumba?
Lakini pia inabidi twende mbali zaidi na kuhoji kama Lipumba anaweza
“kuweka imani yake mbele” kama alivyopongezwa na Sheikh Basaleh mara
baada ya Uchaguzi Mkuu (kwa kauli yake mwenyewe) je, anaweza kukiongoza
chama cha siasa ambacho ni cha kitaifa ambamo ndani yake wamo
Wakristu? Je, inawezekana ndani ya CUF Mwenyekiti Lipumba na Katibu Mkuu
Maalim Seif (wote Waislamu) Wakristu wanaweza kuwa na haki yoyote sawa
au wanaonekana kama watu ambao wanachukuliwa kama ishara tu ya kitaifa
lakini chama kwa kweli ni cha Waislamu chenye kupigania harakati za
Waislamu?
Sasa binafsi sina tatizo kabisa na Lipumba kama Muislamu kuzungumzia
mambo ya Uislamu – kwangu haijalishi sana; lakini shida inakuja kuwa
kiongozi wa umma anaposimama na kuzungumza lugha ya kuligawa taifa
jinsi alivyofanya Lipumba kweli anaweza kuaminika? Inawezekana ni kweli
Watanzania walitambua huu mwelekeo wa Lipumba ndio maana walimkataa
mara nne na tena mara ya nne walimkataa vibaya zaidi?
Lakini swali ambalo linabakia ni jinsi gani Lipumba anaweza kuendelea
kuwa mwenyekiti wa chama cha siasa wakati Mwenyekiti wake anapigania
maslahi ya kidini kwa kupitia chama chake akithibitisha kuwa CUF
ilifanya hivyo mwaka 2010? Sheria ya vyama vya siasa inakataza kabisa
vyama kuundwa kwa maslahi ya kupigania dini au maslahi ya kidini.
Kwamba CUF kimefanya hivi na Lipumba amethibitisha swali kubwa
linabakia – Je, Msajili wa Vyama vya Siasa ana ujasiri wa kufanya
lolote?
Kama Lwakatare kwa maneno ya video ameweza kushtakiwa na kunyimwa
dhamana kwa sababu ameoneka na akipanga njama – wengine walisema ugaidi
– je, Lipumba ambaye ameonekana akithibitisha kuwa chama chake ni
chama cha kupigania haki za Waislamu na hili liko wazi kwenye video na
yeye mwenyewe hajakanusha je, John Tendwa ana uwezo wa kusema lolote au
ataumauma maneno ya kutaka “kuletewa malalamiko rasmi”?
Ninapoacha maswali haya na mengine nabakia kujiuliza tunafikiri
tumefika pabaya je, inaweza kuwa mbaya zaidi ya hivi? Muda utajibu
source: raia mwema: Lula wa Ndali Mwananzela
No comments:
Post a Comment