WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, June 29, 2013

Kiwango changu bado juu

 

Juma Kaseja Juma  

Kigoma. Kipa aliyefunguliwa mlango kuondoka Mtaa wa Msimbazi, Juma Kaseja amesema taarifa za kutemwa kwake anazisikia kwenye vyombo vya habari tu, na kwamba hata kama ni kweli hazijamshtua kwa vile anaamini kiwango chake bado kimesimama kwenye mstari.
Kwa zaidi ya wiki sasa, vyombo vya habari vimekuwa vikiandika taarifa zilizokosa maelezo ya kina kuhusu kutemwa kipa huyo namba moja wa Simba na nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars.
Kaseja ambaye kwa sasa yuko Kigoma kwa ajili ya mapumziko, alisema anafahamu kuwa mkataba wake na Simba ulishakwisha tangu baada ya kumalizika kwa msimu uliopita, hivyo yeye ni mchezaji huru.
“Nasikia tu nimetemwa Simba, lakini kweli sijapata barua na hata kama ningejulisha, nisingeshangaa kwa sababu mkataba wangu na Simba ulishamalizika,” alisema Kaseja.
Mlinda mlango hiyo mwenye rekodi ya pekee nchini, alisema hana ugomvi na uongozi wa Simba pamoja na kutomjulisha kama hawatamwongezea mkataba.
“Sijawahi hata siku moja kujulishwa kuwa sitaongezewa mkataba mpya baada ya kumalizika uliotangulia. Hakuna kiongozi aliyeniambia lolote zaidi ya kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba sitakiwi,” alisema Kaseja.
“Kwa sasa siwezi kuzungumza mengi kwa vile sina haki hiyo kwa sasa, muda utafika nitaongea. Napumzika huku pia nikiendelea kufanya mazoezi kwa sababu soka ndiyo ajira yangu,” aliongeza Kaseja.
Kaseja aliyeidakia Simba kwa miaka tisa mfulilizo tangu mwaka 2003, hakuwa tayari kuweka bayana mwelekeo wake kama uamuzi wa kutemwa Simba utabaki palepale.
Alisema: “Siwezi kusema lolote kwa sasa, ila muda ukifika nitaweka wazi mambo yangu. Naamini bado nina uwezo na kamwe sitakata tamaa hata kama nitaondoka Simba.”
Tangu kutangaza kutemwa kwa Kaseja zaidi ya wiki moja iliyopita, taarifa za ndani kutoka Simba zinadai kuwa uamuzi huo umezaa mgogoro chinichini baina ya viongozi.
Ingawa Mwenyekiti wa Simba Aden Rage, aliwahi kukaririwa akisema kipa huyo hatavaa jezi za Msimbazi msimu ujao, viongozi wenzake wanapinga uamuzi huo.
Kaseja aliwahi kulalamikiwa na mashabiki wa Simba mwishoni mwa msimu uliopita wakimtuhumu kucheza chini ya kiwango hali iliyosababisha kufungwa mabao ya kizembe.
Mbali na kudaiwa kushuka kiwango, kuna taarifa pia kuwa Simba imeamua kuachana na kipa huyo kutokana na kudai dau kubwa ili kusaini mkataba mpya baada ya ule wa awali kumalizika

source: mwananchi

Wengi wamtakia Mandela afya njema


ak 0631a










MAMIA ya watu wanaendelea kukusanyika nje ya hospitali alikolazwa Nelson Mandela mjini Pretoria Afrika Kusini. Inaarifiwa Mandela bado yuko hali mahututi.
Wamekuwa wakimuimbia nyimbo na kumuombea nje ya hospitali. Wengine wamekusanyika katika iliyokuwa makaazi ya Mandela mtaani Soweto.
Watu wana wasiwasi kuhusu hali y mandela lakini pia wanataka kuonyesha wanavyojivunia kiongozi wao ambaye wanamuona kama baba wa taifa lao.
Mandela , rais wa kwanza mweusi Afrika Kusini, anaugua maradhi ya Mapafu.
Mamia ya wananchi walikesha kwa maombi maombi nje ya makaazi ya zamani ya aliyekuwa rais wa taifa hilo Nelson mtaani Soweto.
Rais Jacob Zuma amesema kuwa afya ya shujaa huyo aliyepigana dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini humo inaendelea kuimarika.
Mandela aliye na umri wa miaka 94 amekuwa hospitalini akiuguwa ugonjwa wa maambukizi ya mapafu.
Awali mwanawe wa kike, Makaziwe alisema afya ya babake inaendelea kuwa njema.
Aidha Makaziwe amevikashifu vyombo vya habari kwa kukita kambi nje ya hospitali alikolazwa shujaa huyo akisema wanahabari wanapaswa kumheshimu babaake.
Rais Jacob Zuma alisema Alhamisi kuwa hali ya Mandela iliimarika lakini bado yuko hali mahututi.
"leo angalau yuko sawa kidogo kuliko nilivyomwacha jana usiku,'' alisema Rais Zuma baada ya kuongea na madakatari wanaomtibu Mandela.
Bwana Zuma alifutilia mbali safari yake ya Msumbiji ili kumtembelea Mandela hospitalini.
Wakati huohuo mwanawe Mandela Makaziwe alisema Mzee 'bado yupo' na kuwa anaweza kuhisi mtu akimgusa.

Chanzo: bbcswahili

Friday, June 28, 2013

Zuma ana siri nzito ya Mandela


 


Johannesburg. Rais Jacob Zuma anaaminika kuwa na siri nzito ya Rais wa zamani wa nchi hiyo, Nelson Mandela baada ya kufuta safari ya kwenda Maputo, Msumbiji alikokuwa akahudhurie mkutano wa marais wa nchi wanachama wa Ushirikiano wa Maendeleo wa nchi za Kusini mwa Afrika (SADC).

Zuma alivunja safari hiyo baada ya kumtembelea Mandela hospitalini na kumwona afya yake ikiwa imedhoofika, huku akiendelea kusaidiwa kupumua kwa mashine.

Hatua ya Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma kuahirisha safari yake ya Maputo, tayari kumeibua sintofahamu zaidi kuhusu hatima ya afya ya Mandela.

Msemaji wa Rais Zuma, Mac Maharaj alisema kuendelea kuzorota kwa afya ya Mandela ni sababu ya kufutwa kwa safari hiyo.

Hata hivyo, Maharaj akizungumza kwa simu na gazeti hili jana alikataa katakata kuzungumzia undani wa afya ya Mandela, akasema jukumu hilo ni la familia yake na kwamba Ikulu inasaidia tu katika masuala ya jumla yanayohusu afya ya kiongozi huyo.

Familia ya Mandela
Wakati familia ya aliyekuwa mpigania amani na ubaguzi nchini Afrika Kusini, Nelson Mandela wakipeleka mashine ya kuchimbia kaburi katika makaburi ya kifamilia yaliyopo eneo la Qunu, kwa mara ya kwanza, kiongozi huyo amefumbua macho na kurejewa na fahamu.

Taarifa iliyotolewa jana jioni na Ikulu ya Afrika Kusini inasema Rais Zuma alimtembelea Mandela hospitalini mapema jana ambako alipewa taarifa kwamba anaendelea vizuri. “Bado yuko mahututi lakini imara,” ilisema taarifa ya Ikulu na kuongeza:

“Ana nafuu zaidi leo kuliko nilivyomwona jana (juzi) usiku. Timu ya madaktari inaendelea kumtibu.”
Hata hivyo taarifa hiyo ilimnukuu Rais Zuma akilalamikia kile alichosema kuwa ni vyombo vya habari kutoheshimu faragha ya mgonjwa.

Kauli hiyo ya Zuma ilitolewa muda mfupi tangu binti yake Mandela alipovikosoa vyombo vya habari vya nje ya Afrika Kusini, kwamba vinafanya kazi ya kuripoti tukio la ugonjwa wa Mandela katika misingi ya ubaguzi wa rangi.

Akihojiwa na kituo cha televisheni cha SABC jana mchana, Makaziwe alisema kitendo cha vyombo vya Magharibi kuweka kambi nje ya Hospitali ya Medi Clinic alikolazwa baba yake ni kushindwa kuheshimu desturi za Kiafrika.

Mashine yapelekwa makaburini
Mashine hiyo ilipelekwa juzi katika makaburi hayo ambapo ndipo wanapozikwa ndugu wa familia ya mzee Mandela. Hatua hiyo imekuja baada ya mkutano wa pili wa wanandugu wa karibu na Mandela uliofanyika juzi kwenye mji wa Qunu, kabla ya baadaye kufanya mkutano mwingine kati ya wanaukoo wa Mandela na maofisa wa Serikali waliokuwa wakizungumza mambo ya siri.

Mandela amelazwa katika Hospitali ya Moyo ya Medi-Clinic na hali yake ni ya kukatisha matumaini.
Mbali na hali yake hiyo, Shirika la Habari la Afrika Kusini la CBS jana liliripoti pia kuwa, ini na figo za Mandela zinafanya kazi chini ya asilimia 50.

Taarifa zaidi zinasema, kwa sasa maisha ya Nelson Mandela yapo mikononi mwa familia yake ambao ndio wanaoweza kusema aondolewe mashine ya kumsaidia kupumua ama la.

Miongoni mwao ni pamoja na Waziri wa Utumishi wa Umma na Utawala, Lindiwi Sisulu na kiongozi wa Kikabila Phathekile Holomisa, ambaye alisema kwa sasa kiongozi huyo wa zamani anateseka, hivyo kinachotakiwa ni uamuzi wa familia kuzima mashine ya kumsaidia kupumua.

“Kwa sasa Mandela hafurahii chochote kile, kinachoendelea katika ulimwengu wetu, sasa kwa nini familia isiamue tu kumwondolea hii mashine inayomsaidia kupumua?” alisema.

Tayari kanisa lililopo ndani ya kambi moja ya jeshi mjini Pretoria lilisema kwamba litaandaa mwili wa kiongozi huyo atakapofariki dunia, huku mtoto mkubwa wa Mandela, Makaziwe Mandela akisema lolote linaweza kutokea kuanzia sasa.

Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Pretoria, Makaziwe alisema: “Hali aliyokuwa nayo baba, kwa kweli tunasubiri tu lolote kutokea.”

Naye mjukuu wake Ndileka Mandela alisema, kwamba kutokana na hali ya babu yake huyo wanasubiri lolote lile, wakati mjukuu wake mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Zoleka alisema kwamba hali ya babu yake hairidhishi na inaiweka familia katika wakati mgumu.

Wakazi wamzungumzia
Baadhi ya wakazi wa Johannesburg wanasema Zuma ana “siri nzito” kuhusu hatima ya afya ya Mandela (94), ambaye amelazwa katika Hospitali ya Magonjwa ya Moyo, Med Clinic mjini Pretoria ambako mamia ya watu wamekuwa wakifika kwa ajili ya kumwombea na kumtakia afya njema.

Hatua ya Rais Zuma pia ilisababisha kuongezeka idadi ya watu waliojitokeza kwenda kwenye makazi ya kiongozi huyo yaliyopo eneo la Houghton, Mtaa wa Laan 12 jijini Johannesburg tofauti na juzi, kiasi kwamba polisi walilazimika kufunga baadhi ya barabara kuzuia uingiaji huo isipokuwa kwa waandishi wa habari na wakazi wa eneo hilo pekee.

Mzee aliyejitambulisha kuwa rafiki wa karibu wa Mandela, Pathekile Holomisa, aliliambia gazeti hili kuwa: “Kweli tunapita katika kipindi kigumu, muda umefika kwa Madiba kuwa katika hali aliyonayo, kwa bahati mbaya sisi hatuna tunachoweza kufanya.”

“Tunaambiwa kwamba anasaidiwa na mashine kupumua, katika hatua hii Mungu pekee ndiye anayeweza kutuvusha, pengine Zuma ana siri ya afya yake,”alisema Holomisa ambaye alikuwa akilengwa na machozi.

Mkazi mwingine wa Johannesburg, Bono Boya aliliambia gazeti hili kuwa shauku waliyonayo wananchi wengi wa Afrika Kusini ni kumwona Mandela akitimiza umri wa miaka 95 ifikapo Julai 18 mwaka huu.

“Tumeambiwa anapumua kwa mashine, Serikali iziache mashine ziendelee kufanya kazi hadi mwezi ujao, tunatamani afikishe miaka 95 ili tusherehekee siku ya Mandela pamoja naye, baada ya hapo basi wazitoe maana ni kweli kwamba umri wake ni mkubwa sasa,”alisema Boya.

Mtanzania anayeishi Johannesburg, Almasi Maliki aliliambia gazeti hili kuwa: “Hapa South (Afrika Kusini) Mandela ni kama Mungu, ni mtu anayekubalika kwa Wazungu na Waswahili (Waafrika) kwa hiyo akifa tu, kila kitu hapa kitasimama.

Mashada, nyimbo zatawala
Polisi wa Afrika Kusini walilazimika kuondoa baadhi ya mashada ya maua yaliyotapakaa nje ya Hospitali ya Moyo ya Medi-Clinic.

Watu mbalimbali wamekuwa wakiweka mashada ya maua, maputo na kadi za kumtakia nafuu Madiba.
Pia nyimbo za kumwombea Mandela zilitawala katika hospitali hiyo iliyopo eneo la Pretoria, ambapo hata Zuma naye alijitokeza kuimba.

Miongoni mwa ujumbe uliokuwa umetawala katika maua hayo na kadi yalisomeka: “Tunakuombea kwa Mungu...tunakupenda...Mungu akubariki Mandela.”

source: mwananchi

Kaseja atetewa



Kaseja 

Dar es Salaam.  Baadhi ya wadau wa soka, wamekosoa uamuzi wa klabu ya Simba kutangaza kumtema kipa wake namba moja, Juma Kaseja na kusema hatua hiyo imechangiwa na siasa za chuki dhidi ya kipa huyo.

Kwa wiki nzima sasa, suala la Kaseje kutemwa limekuwa gumzo kwenye vyombo vya habari, huku ikielezwa kuwa uamuzi huo umewagawa viongozi wa klabu, kwani baadhi yao wanataka aendelee kubaki.
Rafiki wa karibu wa Kaseje amelitonya gazeti hili jana kuwa, kipa huyo kwa sasa yuko nje ya jiji na kwamba anatarajia kuzungumza kwa mara ya kwanza kuhusu hatima yake Simba Jumapili wiki hii.

Mwenyekiti wa Simba na hata kocha Abdallah Kibadeni walikaririwa wakisema, kipa huyo aliyesajiliwa mwaka 2003 kutoka Moro United hatakuwamo kwenye kikosi hicho msimu ujao.

Kipa wa zamani wa klabu hiyo, Moses Mkandawile ameshutumu uamuzi wa Simba kumtema Kaseja kwani, yeye binafsi anaamini Kaseja ndiye kipa bora kwa sasa Tanzania.

“Huyu ni nahodha wa timu ya Taifa, ikiwa na maana kwamba kiwango chake bado kiko juu. Sasa iweje Simba wamteme kwa madai ya kushuka kiwango? Kweli uamuzi huu unashangaza sana,” alisema Mkandawile.

“Nadhani kuna chuki binafsi kati yake na baadhi ya viongozi ndiyo maana wengine wanapinga Kaseja kutemwa,” alisema zaidi kipa huyo wa zamani.

Aidha, Katibu Mkuu wa zamani TFF, Fred Mwakalebela naye alishangazwa na uamuzi wa Simba kumtema kipa huyo na kusema haukuzingatia uwezo wake, bali chuki kutoka kwa baadhi ya viongozi wake.

Mwakalebela alisema, anaamini Kaseja bado ni kipa mwenye uwezo wa kucheza timu yoyote kwa vile kiwango chake bado kinadai tofauti na mawazo ya watu wengine.

Kwa upande wake, mchezaji wa zamani Yanga  Kitwana Manara alisema walichokifanya kwa Kaseja siyo sahihi hata kama mpira umekwisha anatakiwa apewe heshima yake kama mchezaji aliyeitumikia klabu muda mrefu.

“Huyu ni alama ya mafanikio Simba, alipaswa kupewa heshima kubwa. Kama hawataki kumsajili, basi wangemweka kwenye benchi la ufundi,” alisema Manara.

Kwa upande wake, nyota wa zamani Taifa Stars, Peter Tino alisema masuala ya usajili waachiwe viongozi na benchi la ufundi na kwamba wasisikilize kelele za mashabiki.

“Kaseja ni kipa mzuri mpaka sasa, ana uwezo wa kucheza zaidi tofauti na wengine wanavyodhani. Apewe nafasi nyingine aonyeshe uwezo wake,” alisema Tino.

Kocha Kennedy Mwaisabula ameishauri Simba kufuta mpango wake wa kumtema kipa huyo, kwani bado ana uwezo mkubwa.

Wakati huohuo, klabu ya Yanga imekana taarifa kuwa ina mpango wa kumsajili Juma Kaseja.

Katibu wa Yanga Laurance Mwalusako alisema, wanatambua kuwa Kaseja bado ana uwezo mkubwa langoni, lakini hayuko kwenye mpango wa kumsajili kwa vile wana makipa wazuri. Kaseja aliwahi kucheza Yanga msimu mmoja, mwaka 2009.

source: mwananchi

Madege 8 ya Obama yatua Dar

 


Dar es Salaam. Makachero wa Marekani wameendelea na matayarisho ya mwisho ya ziara ya Rais Barack Obama, ambapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere walikuwa na kazi ya kuunganisha helikopta za doria.

Makachero hao walikuwa wakiunganisha helikopta sita zilizosafirishwa vipande vipande kutoka Marekani, ambapo meli mbili za kivita na ndege moja pia zimewasili.

Rais Obama tayari yuko katika ardhi ya Afrika, ambapo leo anatarajiwa kwenda Afrika Kusini baada ya kumaliza ziara yake ya kwanza Senegal na anatarajiwa kuwasili nchini Jumatatu.

Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa jana na Mwananchi unaonyesha Marekani imeleta helikopta hizo kwa ajili ya ulinzi wa Rais Obama, zikiwemo meli zilizobeba helikopta nyingine mbili na ndege.

Habari zilizopatikana kutoka kwa wafanyakazi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,zinasema kuwa helikopta sita zinaunganishwa katika sehemu ya karakana ya Kikosi cha Anga cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Mpashaji mmoja aliliambia gazeti hili kuwa helikopta hizo zililetwa kama vipande vipande vilivyosafirishwa kama mzigo kwenye meli za kivita zilizotia nanga jijini Dar es Salaam.

“Nilikaribia kwenye eneo la karakana na nikashangaa kuona jinsi jamaa walivyokuwa ‘bize’ wakiunganisha vyuma mbalimbali na kutengeneza helikopta hizo,” aliongeza mpashaji wetu, ambaye alibahatika kusogelea eneo hilo licha ya kuwepo kwa ulinzi mkali.
Inaaminika kuwa helikopta hizo zitakuwa zinasaidia kusafirisha watu na mizigo kutoka kwenye meli za kivita ambazo zimeegeshwa kwenye Kikosi cha Maji cha JWTZ.

Pia helikopta mbili zinaaminika ziko katika meli ambazo zimeegeshwa huko Kigamboni.
Meli za kivita na ndege ya kijeshi

Katika hatua nyingine, meli mbili za kivita ambazo zimetengenezwa kwa teknolojia ya hali ya juu zimeegeshwa Kigamboni.

“Jamaa wana meli kali kwa kweli, mimi nimekuwa askari wa Kikosi cha Maji kwa muda mrefu na kufanya mazoezi na mataifa kadhaa, lakini sijaona meli kama zile

“Wamarekani wanatisha sana. Meli zao zina zana muhimu za kivita. Pia wanafuatilia kila kitu kinachoweza kuhatarisha usalama wao. Hawaamini mtu kabisa wala kudharau chochote,” aliongeza mtoa habari mmoja.
Ndege ya kijeshi

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa kuna ndege ya Jeshi la Marekani lakini imeegeshwa kwenye karakana ya Kikosi cha Anga cha JWTZ.

Ndege hiyo inadaiwa iko nchini tangu mwanzoni mwa wiki hii, ingawa kuna taarifa kuwa zipo ndege nyingine ambazo zimekuwa zikitua na kuruka.

“Ndege nyingi za Wamarekani zinatua nchini kwa kipindi cha wiki mbili sasa, zaidi zinaleta watu, ambao nahisi ni wale wanaohusika na usalama na mizigo.
“Kimsingi kuna mambo mengi yanaendelea hapa uwanja wa ndege. Ila msisahau pia kuna ujio wa marais kutoka sehemu mbalimbali duniani kwa ajili ya mkutano wa Smart Partnership ndiyo maana kuna mengi yanaendelea hapa,” kiliongeza chanzo chetu.
Matapeli waibuka

Kuna habari pia, kuna kundi la watu limeibuka jijini Dar es Salaam ambalo linataka kutapeli wakazi wa jiji kwa kutumia mgongo wa ujio wa Rais wa Marekani, Barack Obama.

Kamishna wa Polisi wa Kanda Maalumu, Suleiman Kova aliliambia gazeti hili kuwa wamepelekewa kesi tatu za majaribio ya watu kupora wengine kwa kutumia mgongo wa Obama.

Ziara ya Rais Obama imesababisha kuongezeka kwa mahitaji ya usafiri na malazi, hali iliyosababisha kuibuka kwa matapeli wanaowalenga watu wenye magari yenye hadhi kwa wageni wa nje.

Pia hali hiyo imechangiwa zaidi kutokana na ugeni wa viongozi wapatao 11 kutoka mataifa mbalimbali duniani, wanaohudhuria mkutano wa Smart Partnership unaoanza leo jijini Dar es Salaam.
Kova alisema kundi hilo limekuwa likiwasiliana na watu wanaomiliki magari ya kifahari ili wakodishe magari yao.

“Matapeli huwa wanajifanya kuwa wanawakilisha Ubalozi wa Marekani na kujifanya wanataka magari ili kubeba watu watakaofuatana na Rais Obama.
Kwa mujibu wa Kova matapeli hao walilenga kutumia ziara ya Rais Obama kufanikisha wizi wa magari, hasa yale ya kifahari.

Kituo cha Mabasi cha Mwenge chasafishwa
Katika hatua nyingine, Manispaa ya Kinondoni ilivunja vibanda vya biashara kwenye Kituo cha Mabasi cha Mwenge.

Operesheni hiyo iliendeshwa kwa ushirikiano wa maofisa wa Manispaa, Askari wa Jiji, Kikosi cha Polisi cha Kutuliza Fujo (FFU).

Watu walioshuhudia tukio hilo wanaeleza kuwa wafanyabiashara ndogondogo walikuwa wakikimbia ovyo huku wakiwa wamebeba bidhaa zao.
Kituo hicho cha Mwenge huwa kina wachuuzi wengi na wengine hufikia hatua ya kuweka vitu chini.
Mkutano wa Smart Partnership

Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue amesema macho na masikio ya dunia nzima kuanzia leo yanahamia jijini Dar es Salaam kutokana na ugeni mkubwa wa marais tisa na ujumbe wa watu 800, kutoka nchi mbalimbali duniani wanaoanza leo mkutano wa majadiliano ya Smart Partnership.

Mkutano wa Smart Partnership unahusu uwekezaji katika sayansi na teknolojia kwa lengo la kujiletea maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Sefue alisema mkutano huo utafunguliwa na Rais Jakaya Kikwete katika Ukumbi wa mikutano wa Kimataifa wa Nyerere jijini Dar es Salaam.
 
“Nchi yetu imepata heshima kubwa, macho na masikio dunia nzima sasa yanaitazama Tanzania, kila mgeni atakuwa balozi wetu wa kuitangaza nchini yetu huko ughaibuni,” alisema Sefue

Marais watakaohudhuria katika majadiliano hayo na nchi zao kwenye mabano ni Yoweri Museveni (Uganda), Uhuru Kenyatta (Kenya), Boni Yayi (Benin), Ali Omar Bongo (Gabon), Ikililou Dhoinine (Comoro), Ernest Koroma (Sierra Leone) na Blaise Compaore (Burkina Faso).

Viongozi wengine ni Mfalme Mswati II (Swaziland) na Mahinda Rajapaska (Sri Lanka), ambao wametua nchini tayari ya mkutano huo.

Imeandikwa na Beatrice Moses, Patricia Kimelemeta na Ramadhani Kaminyonge

source:mwamanchi

Thursday, June 27, 2013

Neno La Leo: Julius Nyerere Na Ushirikina Wetu....!


9 8fa48

Ndugu zangu,

 Asubuhi ya leo hapa Iringa nilishangaa kuona makundi ya watu yakitokea maeneo ya Kihesa kuelekea katikati ya mji.

Nilipouliza nikaambiwa wanakwenda kwenye maombi. Ndio, Alhamisi asubuhi, watu wanafunga safari kwenda kwenye maombi. Nimeambiwa maombi hayo ni ya siku kadhaa. Ni siku kadhaa za watu kutokufanya kazi.

 Na wengi ni watu wazima, na zaidi wanawake. Kwa kuwaangalia,

kuna wenye kwenda kuombewa kwa hofu ya kuwa wamerogwa, au wanahofia wasije wakarogwa.  Ni hofu ya ushirikina. Na wengi wanaumwa kisaikolojia. Kuna wenye kujihisi wamerogwa, ama , wanaishi na wachawi kama majirani. Hawa wako gizani kwenye wengine tunachokiona ni nuru.

 Inanikumbusha kisa cha Julius Nyerere na mwandishi wa Kimagharibi. Miezi ya mwanzo kabisa ya Tanganyika huru, mwaka 1961,  Julius Nyerere alitembelewa na mwandishi wa habari kijana wa Kimagharibi. Mwandishi yule alimwuliza Julius Nyerere, Rais kijana kwenye nchi changa  swali lifuatalo;

 “ Mheshimiwa Rais, unadhani kwa sasa ni kitu gani kimetawala fikra za watu unaowaongoza kwa maana ya Watanganyika ?”

 Julius Nyerere alitulia kidogo, kisha akajibu;
 “ Kwa kweli kilicho mbele kabisa kwenye fikra za watu wangu ni ushirikina. WaTanganyika wengi wanafikiri sana juu ya mambo ya kishirikina, hasa zaidi watu wa vijijini”.

 Miaka mingi ikapita, na kabla ya Julius Nyerere hajang’atuka uongozi, mwandishi yule alirudi tena Tanzania. Akakutana na Julius Nyerere. Akamwuliza swali lile lile la mwaka 1961, akitaka kujua Watanzania wa sasa ni kitu gani kilicho mbele kwenye fikra zao.

 Julius Nyerere hakuchukua muda mrefu kutoa jibu. Alisema;“ Ooh! Kwa sasa hali ni mbaya zaidi. Watanzania wa sasa  wanafikiri zaidi mambo ya ushirikina, na sasa si vijijini tu, hata watu wa mijini nao wanatanguliza sana mambo ya ushirikina kwenye fikra zao!”

 Ndio, msafara ule niliowaona leo asubuhi wakitokea Kihesa na kwingineko ni WaTanzania wa mijini!

Ni Neno La Leo.
 Maggid Mjengwa

Ya Arusha na tuendako kama taifa




MWAKA 1976 nilikuwa mtoto wa miaka kumi tu. Hata hivyo, nilikuwa na uelewa wa kujua baadhi ya mambo, likiwemo tukio la kule Soweto, Afrika Kusini, yalipotokea mauaji makubwa, ya kutisha na ya kusikitisha ya watoto wengi wa shule. Ilikuwa ni Juni 16, 1976.

Mauaji yale yamepelekea Juni 16 kufanywa kuwa Siku ya Mtoto wa Afrika. Mwaka 1976 sikuweza kufikiri kuwa tukio kama lile la Soweto lingeweza kutokea katika nchi niliyozaliwa. Juzi hapa, siku moja kabla ya Juni 16, tumepokea habari ya mauaji ya kutisha kwenye viwanja vya Soweto, Arusha.

Kuna watoto wamekufa pia. Na picha za watoto waliojeruhiwa, tumeziona magazetini na kwenye runinga. Kama alivyotamka AGP Said Mwema, kilichotokea Arusha kinaashiria vitendo vya ugaidi. Hivyo basi, vilaaniwe na wote wenye mapenzi mema na nchi yetu.
Huu ni wakati pia wa kushikamana kama Watanzania, bila kujali tofauti zetu za kiitikadi na kiimani. Maana, hapa tulipo ni vigumu pia kujua hasa, kama taifa, adui wetu ni nani na anatoka wapi! Tuviachie na tuvipe ushirikiano vyombo vya mamlaka ili vifanye uchunguzi wa kina juu ya kilichotokea Arusha. Vifanye hivyo ili vije na ukweli wa kilichotokea, na hivyo kutupunguzia hofu ya ugaidi kwa raia wa nchi hii na hata wageni wa kutoka mataifa ya nje.

Nchi yetu hii imekuwa na sifa ya kuwa na amani na utulivu. Hakuna shaka yoyote kwamba sisi Watanzania kwa ujumla wetu, ni watu wenye kupenda amani. Tusikubali wachache wapandikize mbegu za chuki miongoni mwetu, na hata kufikia hatua ya kuvuruga amani yetu. Kutufanya tuishi kwa hofu na hata kuhofia kukusanyika kwa pamoja kwenye sherehe zetu za harusi na nyinginezo.

Wanadamu kwa kawaida, ni viumbe wenye kutegemeana. Nimepata kuandika kuhusu Mwanafalsafa Jean- Paul Sartre aliyepata kusema: “Hell is the other people.” Kwamba jehanam ni wale wengine. Anataka pia tukubaliane kuwa pepo yaweza kuwa ni wale wengine.
Kwa hakika kabisa, tofauti ya mwanadamu na mnyama iko kwenye kufikiri. Mnyama anaongozwa na hisia, lakini mwanadamu anapaswa aongozwe na kufikiri. Ndiyo maana ng’ombe anaweza kumpanda mama yake. Ni hisia tu zitakazoongoza tendo lake.

Kwa hiyo, mwanadamu kwenye mambo ya msingi, hapaswi kabisa kuongozwa na hisia, ikiwamo ushabiki. Anapaswa kufikiri, na zaidi kufikiri kwa bidii. Vinginevyo, ni ukweli kuwa kijamii, mwanadamu anaweza kuwa kiumbe anayeishi kwenye uhusiano wa kirafiki na kiadui na wenzake.

Na katika hilo la uadui, wanadamu, kama ilivyo kwa wanyama, wanaweza kushindania na hata kugombania vingi; iwe fedha, mashamba, mapenzi na hata kivuli cha mti. Ndiyo, unaweza kabisa kuwakuta wanadamu wawili wanagombania kivuli cha mti, kwamba nani mwenye haki ya kukaa kivulini.

Wanaweza kugombana hadi akatokea mwendawazimu atakayekuja kuukata na huo mti wenyewe. Wanadamu hao watabaki wakitazamana juani. Mara nyingi, migogoro husababishwa na kugombania kisichotosha. Hivyo, lililo la msingi ni kutambua kuwa wanadamu tunategemeana.

Kwamba panapo kushindania jambo, mwanadamu, tofauti na mnyama, anapaswa kufikiri sana. Atangulize kwanza hekima na busara. Kwenye mgogoro wowote ule, mwanadamu ayape mazungumzo nafasi ya pekee katika kufikia muafaka, na si vurugu au mapigano.

Kwenye mgogoro, na kwenye kuitafuta amani, panakosekana mazungumzo, basi, ina maana ya uwepo wa mazingira ya kuvunjika kwa amani. Wanadamu sisi tumekuwa wepesi sana wa kunyosheana vidole na hata kuhukumiana pasipo kudadisi ili kuujua ukweli.

Na hapa nawaletea leo kisa cha wanandoa waliokaa miaka mingi bila kupata mtoto. Wakaamua wamfuge paka nyumbani. Naye paka huyo wakampenda sana kama mtoto wa kumzaa. Paka naye aliwapenda sana bwana na bibi nyumbani.

Ikatokea mke yule akapata mimba na hata kuzaa salama mtoto. Ikawa kama miujiza. Furaha nyumbani ikaongezeka. Siku moja bwana na bibi walimwacha mtoto wao amelala kitandani. Nao wakaenda zao kuwasabahi jamaa na marafiki.

Walipokaribia nyumba yao wakati wakirudi nyumbani, wakashtuka sana. Walimwona paka wao nje ya mlango akiwa na kipande cha nyama mdomoni. Sura yake ilitapakaa damu pia. Wote wawili wakachukua muchi wa kutwangia nafaka.

Kwa hasira wakamtwanga paka yule kichwani. Alikufa papo hapo! Walipoingia chumbani, wakamkuta mtoto wao amelala salama kitandani. Kando kuna nyoka mkubwa aina ya chatu. Nyoka amekufa baada ya kujeruhiwa kwenye mapambano na paka. ‘Hell is the other people!’ Jehanam ni wale wengine. Lakini hata pepo yaweza pia kuwa ni ya wale wengine. Nahitimisha.

Mandela kama Nyerere

 
Baba wa Taifa la Afrika Kusini,Mzee Nelson Mandela

Ule usemi kuwa “duniani wawili wawili” huenda ukawa na ukweli kama tutaangalia mazingira ya ugonjwa na kifo cha  Baba wa Taifa la Tanzania, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, na mazingira ya kuugua na hali aliyo nayo hivi sasa, Baba wa Taifa la Afrika Kusini isiyo na ubaguzi, mzee Nelson Mandela maarufu kama Madiba.
Mpaka sasa mazingira yanaonyesha kufanana kwa kiwango kikubwa katika maeneo mengi, mbali na ukweli kwamba wawili hawa ni viongozi mashuhuri waliolijengea jina bara la Afrika na kulifanya liheshimike katika anga za kimataifa, kwa namna kila mmoja wao alivyotoa uongozi wa mfano kabla na baada ya kustaafu kwao kwa hiari, japokuwa wangeweza kuendelea kuziongoza nchi zao.

Mwalimu Nyerere alilazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas jijini London nchini Uingereza  kwa ugonjwa wa saratani ya damu tangu Septemba 24 mwaka 1999 na kufariki dunia Oktoba 14 mwaka huo, siku 22 baada ya kulazwa.
Kwa upande wake, Mandela ambaye anapigania uhai wake, alilazwa tangu Juni 8, mwaka huu katika Hospitali ya Medi-Clinic, iliyo katika Jiji la Pretoria ikiwa ni siku ya 20 kufikia leo.

Kadri matibabu ya  Mwalimu yalivyokuwa yakiendelea na hali yake ilivyokuwa ikibadilika na kuwa mbaya kiasi cha kuwekewa mashine ya kumsaidia kupumua, Ikulu ya Tanzania  kupitia kwa aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa na mwandishi wake wa habari, Geoffrey Nkurlu, walikuwa wakitoa taarifa kwa umma kuujulisha maendeleo ya ugonjwa kwa ujumla.

Hivyo ndivyo inavyofanyika hivi sasa kueleza maendeleo yote ya ugonjwa wa mzee Mandela na hali ya kuwekewa mashine za kumsaidia kupumua kupitia kwa Rais Jacob Zumma au kwa msemaji wake.

Kwa muda wote wa ugonjwa wa Mwalimu Nyerere hadi kifo chake, umma wa Watanzania ulishiriki kumwombea kupitia kwenye makanisa, misikiti na sehemu zingine ili apone, na umma ulifuatilia kwa shauku kujua habari za maendeleo yake.

Hali hiyo inafanana na hali ilivyo nchini Afrika Kusini ambako wananchi wa nchi hiyo wamefanya ibada mbalimbali za kumuombea Mzee Mandela ili apone, huku wakipeleka kadi na maua ya kumtakia afya njema hospitalini na salamu za kumtakia afya njema kupitia kwenye vyombo vya habari.

Siyo kwamba habari za kuugua kwa Mwalimu Nyerere zilifuatiliwa na Watanzania pekee, bali ulimwengu wote kwa ujumla wakiwamo marais wa mataifa makubwa ambao baadhi kama Rais mstaafu wa Marekani, Bill Clinton, walijitolea kusaidia matibabu yake katika hospitali bora za Marekani.

Hali hiyo pia inatokea hivi sasa kutokana na dunia nzima wakiwamo viongozi wa nchi na serikali wakiwamo wastaafu kufuatilia kwa karibu hali ya Mzee Mandela tangu alipoanza kuugua.

Wakati bara zima likiendelea kumuombea Mandela aliyeko hospitalini wakati huu, liko pia kwenye ugeni mzito wa rais Barack Obama wa Marekani ambaye ataitembelea vile vile nchi hiyo katika ziara ya kikazi iliyoanzia nchini Senegal jana usiku na kutarajiwa kuwasili Afrika Kusini kesho na baadaye Tanzania Jumatatu ijayo.

Kama gazeti la Independence lilivyoeleza katika tolea lake la hivi karibuni kuwa, huenda ziara ya Obama katika nchi hiyo, pengine na bara la Afrika kwa ujumla, ikamezwa na hali mbaya ya kiafya aliyonayo Mzee Mandela.

HALI ILIVYO AFRIKA KUSINI
Wakati Mandela akiwa mahututi, wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini Afrika Kusini, wameanza kuandika jumbe mbalimbali za kukata tamaa juu ya uhai wake kwenye kuta za hospitali ambako amelazwa.

Baadhi ya jumbe hizo ni pamoja na ile uliotundikwa kwenye shingo ya kikatuni ambacho kimelazwa kwenye kitanda huku kitanda kilicholala kikatuni kikiwa kimezungukwa kwa mashada ya maua kuashiria hakuna uhai tena kwa kiongozi huyo.

Ujumbe huo unasomeka hivi: “Asante kwa yote uliyotutendea kwa ajili ya nchi yetu.”

Ujumbe wote unaashiria kutokuwa na uhakika wa kuwa naye tena kiongozi huyo huku nyingi zinazodaiwa kuandikwa na watoto zinaeleza kuwa “siku zote utakuwa hadithi ya kweli kwetu na babu kwetu sisi sote. Tata Mandela umegusa maisha yetu, tunakupenda pia njia hiyo uliyoendea ni yetu sisi sote.”

Nyumbani kwa Mandela jijini Johannesburg, vyombo vya habari kutoka kila kona ya dunia vimepiga kambi vikisubiri habari yoyote kuhusu jabali hilo lililopigana na siasa za ubaguzi wa rangu na kutumikia jela kwa miaka 27 chini ya utawala wa makaburu.

Maua yametanda nje ya nyumba yake, huku ujumbe mbalimbali ukiwa umeandikwa kwenye mawe, mwingi ukimtakia kila la kheri.

Hata hivyo, wananchi wengi katika viunga vya Johannesburg wanaamini kuwa serikali inawaficha kuhusu ukweli hasa wa afya ya Mandela. Wengi waliohojiwa na waandishi wa habari wanaamini kuwa Mandela amekwisha kufa.

Wanaamini kuwa ama serikali inataka Mandela afikishe umri wa miaka 95 mwezi ujao, au wanataka kupisha kwanza ziara ya Obama.

Kwingineko duniani, watu mbalimbali wamekuwa wakimuombea uzima kiongozi huyo humo huku macho yote ya wananchi yakiwa kwa kiongozi wa taifa hilo, Rais Jocob Zuma, kuweka wazi juu ya hali yake.

Tangu Jumapili iliyopita, afya yake ilipozidi kudhoofu vyombo vya habari duniani vimekuwa vikizunguka katika Hospitali ya Medi-Clinic mjini Pretoria ili kujua ukweli wa hali yake.

ASKOFU MKUU AMWOMBEA MANDELA
Askofu Mkuu, Thabo Makgoba, nchini humo, alimuombea Mandela sala ya mwisho ya amani baada ya kumtembelea hospitalini hapo na kuona hali yake hairidhishi.

Katika maombi hayo, Askofu Makgoba aliomba pamoja na mke wake kiongozi huyo, Graca Machel.
 
CHANZO: NIPASHE