WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, March 15, 2015

PENGO ATOFAUTIANA NA MAASKOFU


Dar es Salaam: Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo amesema waumini hawana budi kusoma vizuri na kuelewa Katiba Inayopendekezwa ili wakati ukifika, wafanbye uamuzi kwa hiari na utashi wao wakati wa kupiga Kura ya Maoni.

Ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku mbili baada ya Jukwaa la Wakristo kutoa tamko linalowataka waumini kujitokeza kwa wingi kujiandikisha kwenye Daftari la Wapigakura, kushiriki kikamilifu kwenye shughuli zote za elimu ya Katiba Inayopendekezwa na kupiga kura ya "hapana" kuikataa Katiba Inayopendekezwa.
Lakini jana, Kardinali Pengo alisema kuisoma na kuielewa katiba hiyo ndiyo wajibu wa msingi ambao Wakristo wanao kwa sasa ili kupiga kura inayostahili wakati ukifika. Kuhusu maaskofu kuagiza waumini waikatae Katiba Inayopendekezwa, Kardinali Pengo alisema wao wakiwa viongozi wa watu, hawana mamlaka wala uwezo huo, bali wenye uwezo ni wananchi wenyewe.
Hata hivyo, Kardinali Pengo alitaka tamko hilo lisambazwe kwenye parokia na vigango vyote vya Jimbo Kuu la Dar es Salaam ili waumini wasomewe, wauelewe kwanza, ili hatimaye waweze kufanya uamuzi sahihi wakielewa ni nini wanachokitakiwa kukifanya.
Changamoto za familia

Katika hatua nyingine, Kardinali Pengo pia alizungumzia changamoto za wanandoa, ikiwamo tabia ya kuchepukia nje ya ndoa ambayo alisema inasababisha amani kutoweka ndani ya familia.

Akizungumza katika ibada ya Kwaresima kwa Wanawake Wakatoliki Tanzania (Wawata) jana, Kardinali Pengo alisema akina mama wengi kwa sasa, hususan katika ndoa wamekuwa wakisaliti ndoa na baadaye kuwatupia lawama watoto wao juu ya tabia walizoanzisha wenyewe.

Katika mahubiri yake aliyoyatoa katika Kanisa la Mt. Joseph Dar es Salaam, mbali na changamoto sugu za kifamilia, Kardinali Pengo alijikita katika kuangalia aina sita za malezi kwa watoto na athari za utandawazi kwenye jamii.

"Wapo wanawake ambao kwa sasa wanaendekeza michepuko kwenye familia na wamekuwa hawana hofu ya Mungu wakati wote. Kuna wengine ambao wanavaa mavazi ya mabinti wakisema wanakwenda na wakati," alisema.

"Wanawakemea watoto wao wakati wao wanaendekeza tabia chafu, wakiulizwa wanasema eti wao wameshakuwa watu wazima."

Katika sehemu ya mafundisho yake, mbali na kupungua uaminifu, Kardinali Pengo alizitaja changamoto nyingine alizosema kuwa zimeendelea kuumiza familia ambazo ni tofauti za kiimani, kipato, elimu, kulea watoto nje ya ndoa, kushindwa kudhibiti maadili ya watoto, ushirikina na ufisadi.
Alisema changamoto hizo zinatafuna familia nyingi kwa sasa.

CHANZO: MWANANCHI

Wednesday, March 11, 2015

UNDANI WA AJALI YA IRINGA LEO: BASI LAUA ZAIDI YA ABIRIA 40 BAADA YA KUANGUKIWA NA KONTENA.

Muonekano baada ya kutokea ajali hiyo leo saa 3.30 Jumatano katika kijiji cha Changarawe wilayani Mafinga mkoani Iringa baada ya basi la abiria la kampuni iitwayo Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Dar.
AJALI mbaya ya gari imetokea asubuhi ya leo saa 3.30 Jumatano katika kijiji cha Changarawe wilayani Mafinga mkoani Iringa baada ya basi la abiria la kampuni iitwayo Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Dar kuelekea Mbeya na kusababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia 42 na majeruhi 22.
Habari kutoka eneo la tukio, zinasema ajali hiyo ilitokea wakati lori hilo lililokuwa limepakia kontena, likiwa katika mwendo wa kasi, lilipojaribu kulikwepa shimo lililokuwa katikati ya barabara na lilipotaka kurudi upande wake, ndipo lilipogongana uso kwa uso na basi hilo, linalokadiriwa kuwa na zaidi ya abiria 50 ndani yake.
“Hili lori lilipogongana na basi, kontena lake likaliangukia basi kiasi kwamba abiria wote wamelaliwa, watu wengine wanadaiwa walirushwa katika korongo kufuatia kishindo cha mgongano.
Hali ya kuwaokoa maiti na majeruhi ni ngumu kwa sababu hakuna gesi ya kukatia vyumba hapa Mafinga,” alisema shuhuda mmoja wa ajali hiyo ambaye hakutaja jina lake.
Watu ni wengi eneo la tukio na miongoni mwa viongozi wa serikali ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Juma Masenza.
Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ramadhani Mungi ambaye pia yupo eneo la tukio hivi sasa, amewasiliana na Global na kuahidi kutoa ushirikiano zaidi baadaye kwa vile hivi sasa hekaheka ni nyingi.
Maiti nane watambuliwa
WATU wanane kati ya 42 waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea asubuhi leo katika kijiji cha Changarawe, huko Mafinga wametambuliwa kufuatia zoezi linaloendelea katika hospitali ya Mafinga ambako miili ya marehemu imelazwa.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi ameuambia mtandao huu hivi punde kuwa ajali hiyo iliyohusisha lori aina ya Scania, lenye namba ya usajili T 689 APJ lililokuwa likiendeshwa na Maiga Sebastian na basi la abiria T 338 CBE, ambalo dereva wake alikuwa Baraka Godbless, ilitokea baada ya lori hilo kuliovateki lori lingine la mafuta lililokuwa mbele yake katika mteremko mkali.
“Magari yote mawili yalikuwa yanashuka katika mteremko mkali, lori likitokea Mafinga na basi likitokea Makambako, lori baada ya kuovateki, likaona shimo barabarani, katika kulikwepa akahamia upande wa basi, yakagongana uso kwa uso. Lakini pia kontena lililokuwa kwenye lori, likiwa na vitu vizito, likalilalia basi katikati,” alisema Kamanda.
Akifafanua, alisema katika idadi ya vifo hivyo, watu sita walikuwa wanawake na 36 wanaume, wakiwemo watoto watatu huku majeruhi wakiwa ni 22. Zoezi la kutambua maiti bado linaendelea na kwamba kwa sasa hawezi kutaja majina ya waliotambuliwa.
(HABARI: OJUKU ABRAHAM/GPL)

Tuesday, March 10, 2015

ZITTO KABWE????????

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Zubeir Kabwe.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Zubeir Kabwe, amevuliwa uanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).…
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Zubeir Kabwe.
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) Zitto Zubeir Kabwe, amevuliwa uanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia alikuwa mmoja wa mawakili waliokuwa wakikiwakilisha chama hicho katika kesi hiyo, Tundu Lissu.
Uamuzi huo umechukuliwa muda mfupi baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutupilia mbali ombi lake la kuitaka kuizuia Kamati Kuu ya Chadema kujadili kuhusu ubunge wake, hadi hapo rufaa aliyokuwa ameikata katika Baraza Kuu itakapokuwa imesikilizwa.
Zitto Zubeir Kabwe akiwa na mwanasheria wake, Ndugu Albert Msando.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, ambaye pia alikuwa mmoja wa mawakili waliokuwa wakikiwakilisha chama hicho katika kesi hiyo, Tundu Lissu ndiye aliyetoa tamko la kuvuliwa uanachama kwa Zitto.
Ujumbe aliouandika Zitto Kabwe kupitia mtandao wa Twitter baada ya maamuzi ya mahakama.
“Katiba ya Chadema inasema wazi kuwa mwanachama yeyote atayekipeleka mahakamani, atakuwa amejiondoa uanachama wake endapo atashindwa kesi hiyo, hivyo natangaza rasmi kuwa Zitto Kabwe siyo tena mwanachama wa Chadema,” alisema Lissu.
Zitto Zubeir Kabwe akiongea jambo Bungeni.
Mgogoro kati ya Chadema na Zitto ulianza mwishoni mwa mwaka 2013 baada ya kugundulika kwa nyaraka zilizomhusisha Zitto na wanachama wengine wawili, Dr Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba kwamba walikuwa na nia ya kufanya mapinduzi ya viongozi kwa njia zisizo halali.
Kufuatia jambo hilo, Chadema iliitisha kikao cha Kamati Kuu ili kuwajadili watu hao na kuchukua maamuzi, kilichofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na wajumbe wake wote.
Akiongea na wananchi wa Kigoma Kaskazini.
Wakati kikao hicho kikiendelea na kukiwa na dalili za Zitto na wenzake kutimuliwa, mbunge huyo kijana alikwenda Mahakama Kuu na kuweka zuio la kujadiliwa kwake na Kamati Kuu hadi rufaa yake katika Baraza Kuu la Chadema itakapokuwa imesikilizwa. Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kilikaa Januari 2014.
Katibu Mkuu wa chadema, Dr Wilbrod Slaa (kushoto) akiwa na Zitto Kabwe.
Mahakama ilikubaliana na zuio hilo. Kesi hiyo ilikuwa ikisikilizwa chini ya Jaji Richard Mziray huku Zitto akiwakilishwa na mwanasheria Albert Msando aliyekuwa akishindana na wanasheria watatu wa Chadema, Peter Kibatala, Tundu Lissu na John Mallya. Dr Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba walifukuzwa uanachama na kikao kile cha Kamati Kuu.
Zitto mwenyewe alikuwa hajatoa tamko lolote kuhusiana na hatua hiyo ya chama chake, ambayo hata hivyo, ilitegemewa na wengi.
Dr Kitila Mkumbo akiongea na wanahabari baada ya kutimuliwa Chadema.
Samson Mwigamba.
(HABARI: OJUKU ABRAHAM/GPL)

source: Global Publisher

Monday, March 9, 2015

Yanga si kwa Simba.

  Wapanda nafasi ya tatu, MO aimwagia Sh. milioni 500

Mashabiki wa Simba wakishangilia ushindi baada ya timu yao kuifunga Yanga Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana. Simba ilishinda 1-0. PICHA: TRYPHONE MWEJI
Yanga  imeendelea kuwa mteja wa Simba baada ya jana kukubali kichapo cha bao 1-0 katika mechi ya raundi ya pili iliyopigwa kwenye Uwanja wa Taifa.
 
Ushindi huo wa Simba ni wa pili mfululizo baada ya Desemba mwaka jana Wekundu wa Msimbazi hao kuibamiza mabao 2-0 timu hiyo ya mtaa wa Jangwani na Twiga jijini Dar es Salaam katika mechi ya Nani Mtani Jembe iliyoandaliwa na wadhamini wao wakuu Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha bia ya Kilimanjaro.  
 
Katika mechi ya raundi ya kwanza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) iliyochezwa Oktoba 18, mwaka jana katika uwanja huo, timu hizo zilitoka sare tasa.
 
Matokeo hayo yanaifanya Simba kupanda hadi nafasi ya tatu baada ya kufikisha pointi 26 tano nyuma ya vinara Yanga na nne nyuma ya mabingwa watetezi wa VPL, Azam FC ambao wanashika nafasi ya pili.
 
Bao la Okwi 
Emmanuel Okwi ndiye aliyepeleka kilio Jangwani katika dakika ya 51 baada ya kutupia bao hilo pekee kwa shuti kali akiwa umbali wa takribani mita 27 ambalo lilimshinda kipa wa Yanga, Ali Mustafa 'Barthez'. Okwi alifunga bao hilo kutokana na kupenyezewa pasi murua na Ibrahim Ajibu.
 
Bao hilo ni la tano kwa Okwi msimu huu na ni pili kwa kipa wa Yanga Ali Mustafa 'Barthez' kufungwa VPL msimu huu, pia kipa huyo alifungwa mengine mawili kwenye Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya BDF XI ugenini nchini Botswana.
 
Kabla ya mechi kuanza
Awali katika mechi ya utangulizi iliyozikutanisha Timu B za miamba hiyo, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 5-2 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
 
Baada ya mechi hiyo kumalizika, Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kuingia uwanjani kupasha misuli majira ya saa 9:14 alasiri wakiongozwa na kipa wao, Ivo Mapunda, hata hivyo dakika nne baadaye (saa 9:18) Yanga nao walitinga uwanjani kupasha wakiongozwa na mfungaji bora wa VPL  msimu uliopita, Mrundi Amissi Tambwe.
 
 Robo saa kabla ya mechi kuanza mashabiki wa Yanga waliokuwa wamekaa sehemu ya chini ya jukwaa la VIP C, walianza kuzichapa kavukavu baada ya kutofautiana kuhusu utabiri wa matokeo.
 
Kipa Ivo Mapunda wa Simba alitakiwa na marefa wa mchezo huo kuondoa taulo lake langoni kabla ya mechi kuanza. Taulo hilo limempatia umaarufu mkubwa nchini Kenya wakati akiidakia Gor Mahia. 
 
Katika mechi hiyo, timu zote zilivaa jezi za kampeni maalum ya kupinga mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) ambazo zilikuwa zimeandikwa mbele "imetosha". Kadhalika mechi ilisimama kwa dakika moja kwa kuwakumbuka albino waliokufa kwa mauaji ya ukatili.  
 
Kipindi cha kwanza
Pambano hilo lililoanza kwa timu kusomana, Simba ndiyo waliokuwa wa kwanza kufika langoni mwa Yanga katika dakika ya pili, lakini shuti la Ajibu lilikosa macho baada ya kwenda pembeni kabla ya dakika moja baadaye Ivo kudaka shuti kali la Simon Msuva.
Dakika ya 18, beki wa Simba Juuko Murshid  alifanya kazi ya ziada kwa kuruka juu na kuokoa kwa kichwa krosi ya Msuva iliyokuwa ikielekea kimyani. 
 
Nafasi nzuri zaidi kwa Yanga ilikuwa katika dakika ya 28, Mrwanda alipopewa pasi murua ndani ya 18 na Mrisho Ngasa lakini akapata kigugumizi katika kupiga shuti jambo lililoonekana kumkera Kocha Mkuu Mholanzi Hans van der Pluijm ambaye aliamua kumtoa dakika mbili baadaye na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu.
 
Dakika ya 36, Javu alitoa pasi murua kwa Ngasa ambaye aliachia shuti kali lakini Ivo akawa makini kulicheza.
 
Nafasi nzuri kwa Simba zilikuwa dakika ya pili, tatu, 27, 42 na 44, lakini mashuti ya washambuliaji Emmanuel Okwi na Ajibu hayakuwa na macho huku Ramadhani Singano 'Messi' akishindwa kutumia vema nafasi aliyoipata dakika ya 43 baada ya kukwatuliwa kwa nyuma na Haruna Niyonzima jambo lililomsabishia kadi ya njano.
 
Hadi kipindi cha kwanza kinamalizika hakuna timu iliyoona lango la mwenzake huku Yanga ikipata faulo 9-8, kona 1-1, kuotea 3-1, mashuti 4-4 na njano 3-4 dhidi ya Simba.
 
Kipindi cha pili
Hapakuwa na mabadiliko zaidi ya yale ya Yanga ya kipindi cha kwanza, hata hivyo kasi ya Simba ilionekana dakika ya 51 baada ya Okwi kutupia bao la kwanza kwa shuti kali akiwa umbali wa takribani mita 27 ambalo lilimshinda kipa wa Yanga, Ali Mustafa 'Barthez'. Okwi alifunga bao hilo baada ya kupenyezewa pasi murua na Ajibu.
 
Bao hilo lilipandisha mzuka kwa Kocha Mkuu wa Simba, Mserbia Goran Kopunovic baada ya kucharuka akihamasisha mashabiki wa Simba wasimame kushangilia.
 
Kama Ajibu angeongeza umakini, basi mambo yangezidi kuiendea vibaya Yanga kwani dakika ya 60 akiwa ndani ya 18 alikosa bao la wazi huku dakika tisa baadaye Ivo akifanya kazi ya ziada kwa kucheza shuti la Javu. 
 
Dharau za Niyonzima kupiga mpira na kufunga wakati refa Martin Saanya kutoka Morogoro akiwa ameshapuliza kipenga ziliigharimu Yanga na kuifanya icheze pungufu kuanzia dakika ya 73 baada ya Mnyarwanda huyo kuonyeshwa kadi ya pili ya njano na kutolewa nje, huku pia akienda na kupiga meza ya mwamuzi wa akiba wakati akitoka uwanjani.
 
Dakika ya 75 Ajibu alimpisha Elius Maguri huku Yanga nayo ikifanya mabadiliko katika dakika ya 76 kwa kumtoa Ngasa na kumuingiza Mliberia Sherman Kpah wakati dakika 12 baadaye Simba ikimtoa Abdi Banda na kumuingiza Simon Sserunkuma.
 
Kipenga cha mwisho
Baadhi ya mashabiki wa Jukwaa la VIP C walishindwa kujizuia baada ya kuonekana wakimwaga machozi mara baada ya filimbi ya mwisho ya mwamuzi Saanya. Kadhalika shabiki mmoja wa kike wa Yanga alidondoka na kuzirai kabla ya kukimbizwa hospitali mara baada ya mechi kumalizika. 
 
Nyimbo kuu ya mashabiki wa Simba mara baada ya kipenga cha mwisho, walikuwa wakiimba Jerry Muro, Jerry Muro, Jerry Muro..., ingawa haikufahamika sababu ya kuimba hivyo lakini huenda ni kutokana na tambo alizozitoa msemaji huyo wa Yanga siku moja kabla ya mchezo akisema "Simba si mpinzani tena wa Yanga bali ni mtani tu". 
 
Kauli za makocha
Mara baada ya kumalizika kwa mechi hiyo, Kocha wa Yanga, Pluijm alisema walitengeneza nafasi chache lakini walishindwa kuzitumia, huku pia akifafanua kuwa hata Simba walitengeneza nafasi mbili tu za uhakika kipindi cha pili na kwamba anadhani bahati ya kushinda mechi hiyo ndiyo iliyowabeba.
 
Akizungumzia kitendo cha kumtoa Mrwanda, alisema "Ninamjua Danny (Mrwanda) kitabia, niliamua kumtoa mapema ili asionyeshwe kadi ya pili ya njano.
 
Kwa upande wa Kocha wa Simba, Kopunovic alisema: "Ninawapongeza wachezaji wangu kwa kufuata maelekezo niliyowapa.  Hivi ndivyo Simba inavyopaswa kucheza siku zote.
 
"Bao la Okwi ni gumu, ni mchezaji bora mwenye uwezo wa kufunga  mabao ya aina ile, kwa kweli anastahili pongezi."
 
Naye nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro', alisema tumepambana sana, lakini tumefungwa bao la kushangaza, hatujui limeingiaje. 
 
Naye Niyonzima alisema "ninafikiri ilipangwa na Mungu nitolewe kwa kadi nyekundu". 
 
Kwa ujumla Simba ilipata faulo 12-5 dhidi ya Yanga, kona 0-5, kuotea 0-0, mashuti, 4-3, njano 1-2, nyekundu 0-1 na kunawa mpira 0-1.     Simba: Ivo Mapunda, Kessy Ramadhani, Mohamed Hussein, Hassan Isihaka, Juuko Murshid, Abdi Banda, Ramadhani Singano, Jonas Mkude, Ibrahim Ajibu, Said Ndemla na Emmanuel Okwi.
 
Yanga: Ali Mustafa 'Barthez', Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Nadir Haroub 'Cannavaro', Kelvin Yondani, Said Juma, Simon Msuva, Haruna Niyonzima, Amissi Tambwe, Mrisho Ngasa na Danny Mrwanda.
 
Katika hatua nyingne inadaiwa Mohamed Dewji (Mo) amemwaga kitita Sh. milioni 500 katika klabu hiyo. 
 
Kwingineko
Mtibwa Sugar ikiwa Manungu Turiani ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mbeya City. Bao la Mtibwa lilifingwa na Musa Mgosi dakika ya sita huku la City likifungwa na Themi Felix dakika ya 64. Nayo Mgambo Shooting ilishinda 3-1 dhidi Ndanda FC 
 
CHANZO: NIPASHE

Sunday, March 8, 2015

SIMBA YAICHAPA YANGA LEO UWANJA WA TAIFA!!

Emmanuel Okwi wa Simba (kulia) akikwatuliwa na beki wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' katika mechi baina ya timu hizo leo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Simba ilishinda kwa bao 1-0 lililofungwa na Okwi.
Abdi Banda wa Simba (kulia) akiondoka na mpira huku akikabwa na kiungo Haruna Niyonzima wa Yanga.
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub 'Cannavaro' akizozana jambo na mwamuzi wa mechi ya Yanga na Simba, Martine Saanya.
Kipa wa Yanga, Ally Mustapha 'Barthez' akiudaka mpira huku akishuhudiwa na kiungo wa Simba, Ramadhani Singano (katikati) na beki wa Yanga, Oscar Joshua.
Beki wa Yanga, Mbuyu Twite akiondoa mpira huku akizongwa na Emmanuel Okwi wa Simba.
Mashabiki wa Yanga wakionekana kusisitiza jambo katika mchezo huo wa leo kati ya timu yao dhidi ya Simba.

Wednesday, March 4, 2015

Buriani Kapteni Komba: Nakupigia makofi, nikifuta machozi




HAKUNA ubishi kwamba kifo cha Mbunge wa Mbinga Magharibi na mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kapteni John Damiano Komba ni cha kuhuzunisha.

Ilikuwa ni mshtuko mkubwa kila mahali ziliposikika habari kwamba amefariki ghafla siku hiyo ya Jumamosi, Februari 28, 2015, kwenye Hospitali ya TMJ mjini Dar es Salaam kutokana na ugonjwa wa kisukari na presha.

Ni kama mshumaa uliozimika ghafla katika giza nene. Mshumaa uliotarajiwa kutoa mwanga mkubwa katika kampeni za CCM za Uchaguzi Mkuu wa Rais na wabunge unaotarajiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Tayari katika sherehe za miaka 38 ya CCM mwezi uliopita, Komba aliwaonjesha wapinzani wa CCM aina ya vigongo ambavyo walikuwa watarajie kwenye kampeni za uchaguzi huo.
“Hatunywi sumu, hatujinyongi, CCM mbele kwa mbele…., tumeipenda wenyewe…chaguo letu milele na wavimbe wapasuke watajijua wenyewe….. waache waisome namba, CCM mbele kwa mbele, waacheni waandamane CCM mbele kwa mbele…,” wameambiwa hivyo wapinzani baada ya ‘kugaragazwa’ kwenye uchaguzi wa mitaa na vijiji uliofanyika mwaka huu.
Je, Komba alikuwa mtu wa aina gani? Kama tunavyomjua hakuwa malaika. Alikuwa ni binadamu wa kawaida tu mwenye msimamo wake, mtazamo wake, uamuzi wake, dini yake na chama cha siasa ambacho ni CCM.

Na kama binadamu hakukosa kasoro. Katika usanii Komba hakutaka kushindwa katika jambo lake lolote. Kama unabisha mwulize aliyekuwa mpinzani wake wa jadi, Norbert Chenga wa kikundi cha Muungano, Dar es Salaam ambacho sasa kimetoweka katika ulimwengu wa sanaa.

Yeye na Chenga waliendeshana kweli kweli hasa katika muziki wa taarab. Ilikuwa ni vita ya kunyang’anyana wasanii mahiri na mwenye kisu kikali ndiye mara zote aliyekuwa akishinda na mtu huyo alikuwa ni marehemu.

Mbali ya nguvu ya chama na kipaji cha Komba kuongoza sanaa, umahiri wa TOT dhidi ya Muungano katika taarab ulitokana pia na mkusanyiko wa vipaji vya muziki huo kutoka Zanzibar na kikundi cha JKT na Bima. Kwa mfano, Khadija Kopa na Fatma Dogodogo walikuwa wamechomolewa kutoka katika kikundi mahiri cha taifa cha Culture cha Zanzibar.

Kutoka JKT walitoka wasanii mahiri kama marehemu Mzee Bia Hassan na mtunzi asiye na makeke lakini mkali kweli kweli kwa kutunga, marehemu Ali Mtoto Seif.

Katika vita hiyo ya kukwapua wasanii, kitendo ambacho bila shaka hakitasahaulika ni kile ambacho mwimbaji na mtunzi mahiri wa Muungano, Ally Star ‘alipokiasi’ kikundi cha Muungano kwenda kutamba kwenye jukwaa la TOT siku ya onyesho lenye upinzani mkali kati ya vikundi hivyo viwili kwenye Ukumbi wa Vijana, Dar es Salaam.

Ilikuwa hatari kweli kweli. Fikiria katika upinzani wa kweli wa soka wa enzi za 1960 na 1970 mchezaji tegemeo wa Yanga aibuke ghafla katika benchi la Simba siku ya mechi ya watani hao iliyokuwa na gumzo kubwa. Lakini ilitokea hivyo katika mvutano wa taarab wa TOT na Muungano na sasa imebaki ni historia.

Lakini zaidi ya yote Komba alikuwa ni Mtanzania aliyeipenda nchi yake jinsi inavyoongozwa na CCM na alijitahidi kutumia kipaji chake cha usanii na ushawishi kwenye majukwaa ya siasa kukiongezea chama chake thamani kwa njia ya burudani na majukwaa ya kwao Mbambabay na maeneo mengine.

Tanzania sasa si tena nchi ya chama kimoja. Mzalendo wa kweli unatakiwa uwe shabiki wa chama tawala au upinzani ili kutoa mchango wako katika masuala mbalimbali ya maendeleo.
Komba alichagua kuendelea kuwa shabiki wa CCM mwaka 1992 wakati Tanzania ilipoamua kuwa nchi ya vyama vingi. Kwa sababu hiyo basi, huwezi kumlaumu kwa kutumia kipaji kukisifia CCM na kuvinanga vyama vya upinzani pale alipoona kwa mtazamo wake vinapotoka.
Kapteni Komba amefariki dunia akiwa kipenzi kikubwa cha wanaCCM waliokuwa wanafurahishwa na kipaji chake cha sanaa. Lakini siyo siri kwamba kwenye siasa alijitengenezea maadui kutokana na kauli na misimamo yake mbalimbali.

Yaliyojitokeza katika mitandao ya kijamii baada ya kifo chake yanathibitisha ukweli huo kuwa kuna watu ambao walikuwa hawampendi kabisa kutokana na kauli alizowahi kuzitoa kama mwanaCCM au mwanasiasa.

“.....Kupitia msiba wa Kapteni John Komba ndio nimeanza kuthibitisha chuki kati ya watawala na watawaliwa, hasira kati ya 'wao na sisi', roho mbaya kati ya daraja la chini na daraja la juu.....watu hawana huzuni tena...na kuna watu wanaongea maneno machafu......Nchi haipo salama sana....hasira za matabaka zinaongezeka..,” aliandika mmoja wa wachambuzi wa masuala ya kila siku nchini katika hali ya utani wenye umakini mtandaoni.

“Chuki kati ya watawala na watawaliwa?” “Hasira kati ya wao na sisi?” “Roho mbaya kati ya daraja chini na daraja la juu?” Anachomaanisha mchambuzi huyo hapa kinafikirisha lakini ukweli ni kwamba mambo hayako sawa kisiasa nchini kutokana na kauli za watu baada ya kifo hicho.

Lakini hebu turudi nyuma. Ni mambo gani ambayo marehemu aliwatibua watu wa upande wa pili wa chama chake au wa vyama vya upinzani?

Yanaweza yakawepo mambo kadhaa lakini makubwa yanayojitokeza waziwazi kutokana na jinsi watu wanavyojadili mitandaoni ni matatu.

La kwanza katika orodha ni kauli yake aliyoitoa alipokuwa kwenye Bunge Maalumu la Katiba. Akichangia kwenye Bunge hilo Kapteni Komba alidai kwamba mfumo wa Serikali Tatu ukipitishwa ataingia msituni kudai Serikali mbili.

Hakufafanua lakini kimsingi wengi walivyomuelewa ni kwamba alikuwa anazungumzia kwenda kuanzisha vita katika kudai hizo Serikali mbili alizokuwa anashabikia ambazo ndizo hatimaye zilipitishwa katika mapendekezo ya katiba yaliyopitishwa baada ya wabunge wengi wa upinzani kulisusia bunge hilo.

Wapo waliojitokeza kudai kwamba kauli yake ya kuingia msituni ilikuwa ya hatari ya kuiingiza nchi vitani hivyo kustahili kukemewa.
Je, ilistahili kweli kukemewa? Chama chake, viongozi wa Serikiali wakiwemo wanasheria wake na hata viongozi wa dini zote hawakuiona athari waliokuwa wanaiona wanasiasa wengi wa upinzani ambao walilivalia njuga suala hilo bila mafanikio ya kutaka marehemu kuchukuliwa hatua.

Wapo wanaoamini hadi leo kwamba kauli hiyo ingetolewa na mjumbe wa upinzani angesakamwa.

Suala la pili la marehemu ambalo lilileta ukakasi lilitokea pia kwenye bunge hilo hilo maalum la Katiba alipomwandama aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Marekebisho ya Katiba, Jaji Joseph Warioba. Ilikuwa baada ya kutokea sintofahamu kati ya wajumbe wa CCM na wale wa vyama vya upinzani kupelekea wale wa upinzani kususia vikao.

Kapteni Komba hakumung’unya maneno kueleza jinsi alivyofadhaishwa na Jaji Warioba katika mchakato wake mzima wa kukusanya maoni na mapendekezo yake ya rasimu ya katiba.
Komba alisema kuhusu Waziri Mkuu huyo mstaafu wa Tanzania: “Mimi nasema wazee nyinyi mkistaafu pumzikeni na kama tunawapeni vyeo au nyadhifa mtusaidie kazi, fanya kwa heshima uliojenga huko nyuma. Lakini leo hizi zote vurugu hizi ni warioba. Nashindwa kuvumilia kutosema, mtanisamehe….. vurugu zote hata tungezungumza namna gani , mzee huyu ni chanzo cha vurugu zote….”

Nao uamuzi wa Kapteni Komba wa kumshabikia waziwazi Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa katika mbio za kuwania urais 2015, ulimtenganisha na baadhi ya wanachama wenzake wa CCM waliopo katika kambi za wagombea wengine wa urais.

“Mimi hapa nilipo leo ukiniuliza nani atakuwa rais, mimi nasema Lowasa anafaa kuwa rais. ….Mimi nasema Edward Lowassa anafaa kuwa rais kabisa. Kama chama changu kitampendekeza mimi 100 kwa 1000 kabisa…..” alisema Komba alipohojiwa katika kipindi kimoja cha runinga kuhusu nani anayefaa kuwa Rais 2015.

Jimboni kwake, Komba alikuwa mtetezi mkubwa wa wananchi wake walioko katika mwambao wa Ziwa Nyasa. Mara baada ya kuuvaa ubunge alilalamika sana kuhusu ukosefu wa usafiri wa uhakika wa meli.

Alifikia hata hatua ya kumsifu aliyekuwa Rais wa Kwanza wa nchi jirani ya Malawi, Hayati Kamuzu Banda kwamba ndiye aliyekuwa mbunge wao kwa kuruhusu meli ya nchi hiyo M.V Ilala kufanya shughuli zake pia katika mwambao wa Tanzania wa ziwa hilo kusafirisha abiria na mazao.

Mbali ya kulalamikia usafiri wa meli ambao sasa umeahidiwa utapatiwa ufumbuzi na serikali, Komba amefariki akilalamikia pia tatizo la mawasiliano ya matangazo ya redio za Malawi kuwa na nguvu kuliko matangazo ya redio za Tanzania katika jimbo lake.

Katika mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa kati ya Tanzania na Malawi, Komba alilalamikia uamuzi wa Malawi kusitisha safari za meli ya M.v Ilala katika mwambao wa Tanzania uliokuwa umefanywa na Rais wa zamani wa Malawi, Joyce Banda.

Alimshutumu kwa kuibua upya mzozo wa mpaka wa Ziwa Nyasa na kuwachanganya wananchi wa Mbinga kwa matangazo ya redio za Malawi zinazosikika jimboni mwake.

Komba alisema Rais Joyce Banda alikuwa anazitumia redio zake kupotosha umma kuwa ukanda wa Ziwa Nyasa ni mali yake na wananchi wanaamini hivyo.

Je, Komba alitokea wapi? Ni mwalimu wa shule ya msingi ambaye kipaji chake cha usanii kilivumbuliwa na aliyekuwa kada na CCM na mwenye kipaji cha aina yake ya usanii, hayati Brigedia Jenerali Moses Nnauye. Ndiye aliyemwingiza jeshini na Komba kuanza makeke. ‘CCM Nambari One’ kilikuwa kibao cha kwanza kilichomtoa.

Mwaka 1992 Tanzania ilipoamua kuwa na mfumo wa vyama vingi, Rais Mstaafu Ali Hassan Mwinyi alimshawishi aache jeshi kuunda kikosi cha sanaa ndani ya CCM kilichoitwa Tanzania One Theatre (TOT).

Taifa halitomsahau Komba kwa nyimbo zake za simanzi za maombolezo ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere mwaka 1999.

Aliwahi kuniambia kwamba nyimbo zile alizotunga baada ya kujifungia chumbani aliposikia tu kwamba m Mwalimu amefariki, tofauti na wengi walivyokuwa wakifikiria kwamba zilitungwa wakati Mwalimu bado anauguzwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas, London, Uingereza.

Hakika kifo chake kitawagusa Wamalawi walio wengi na hasa Rais wa zamani wa nchi hiyo, Bakili Muluzi. Komba alikuwa kivutio kikubwa wakati alipopata nafasi ya kumfanyia kampeni Muluzi ili ashinde awamu ya pili ya uongozi wake.

Simulizi za Komba na kundi zima la TOT zilikuwa kubwa hasa vijijini ambako watu walikuwa hawaelewi ni vipi lori kubwa la wasanii hao lilikuwa linatoa muziki mkubwa katika maeneo yao yasiyokuwa na umeme. Ilikuwa kama wanaona uchawi fulani hivi.

Muluzi anakifahamu vyema kipaji cha usanii cha Komba na uzoefu wake wa kushiriki siasa za Tanzania kwani aliweza kummegea mawili matatu yaliyoweza kumuongezea sifa kufanya yeye na chama chake cha UDF kushinda uchaguzi wake wa awamu ya pili kwa kishindo.

Komba aliwahi kuniambia kuwa alifanikiwa kumbadilisha Muluzli kuwa kiongozi wa watu kwa ushauri wake wa kumtaka ajichanganye na watu wa kawaida katika mikutano yake na kuachana na staili iliyokuwapo ya viongozi kuonekana kama ni wafalme wa aina fulani kwa matendo na kauli zao.

Aliniambia kuwa alikuwa ameshibana sana na Muluzi hivyo haikuwa ajabu basi aliporudi nyumbani kuanzisha shule, jina la shule kuitwa Sekondari ya Bakili Muluzi.

Katika juhudi za kutaka muziki wa Tanzania uwe na aina moja ya upigaji, Komba alijaribu kuutangaza mtindo wa Achimenengule ili ufuatwe na bendi zote nchini uwe ni alama ya Tanzania.
Kwa bahati mbaya jambo hilo hakufanikiwa kwani ni bendi chache zilizoitikia hazikufanya hivyo kwa moyo na baadaye kuachna na suala hilo.

Hata hivyo Komba alistahili sifa kwa kujaribu jambo ambalo pengine huko mbele umuhimu wake utaonekana.
Komba alizaliwa Machi 18, 1954. Alisoma shule ya Msingi Lituhi baadaye kujiunga na Sekondari ya Songea kuanzia mwaka 1971 hadi 1974.

Mwaka uliofuata hadi 1976 alijiunga na Chuo cha Ualimu cha Kleruu Iringa na kuhitimu cheti cha ualimu.

Baada hya kujiunga na jeshi, alipata mafunzo ya uafisa wa Jeshi katika chuo cha Maafisa wa Jeshi cha Monduli mwaka 1977 hadi 1978. Ndipo kuanzia mwaka 1992 alipojikita kwenye sanaa na siasa hadi mauti yanamkuta.


Source:www.raiamwema.co.tz

MAOMBOLEZO: Wananchi wamsaidia Nape ujumbe kwa Nyerere


Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye (wa pili kulia) akishirikiana na wanamuziki wa nyimbo za dansi kuimba wimbo maalumu wa kumuaga marehemu John Komba katika Viwanja vya Karimjee juzi. Picha na Venance Nestory 
Dar/Mikoani. Wakati wa kumuaga John Komba, ambaye alikuwa mpiga kampeni mashuhuri wa CCM, kada wa chama hicho, Nape Nnauye aliimba “Neenda baba… msalimie Mwalimu (Julius Nyerere), mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo wakati huu,” bila ya kutaja ikoje, lakini wananchi walioongea na gazeti hili wamemalizia wimbo huo; wanaona hali ya nchi ni mbaya.
Nape, katibu wa itikadi na uenezi na mtoto wa kada maarufu wa CCM, Marehemu Moses Nnauye aliyetunga nyimbo nyingi za uhamasishaji, aliungana na wasanii wa muziki wa dansi kuimba wimbo huo uliotungwa na Komba wakati wa kifo cha Julius Nyerere, ambaye ni mwasisi wa Taifa la Tanzania kwenye Viwanja vya Karimjee juzi.
Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi wa CCM aliongoza kuimba sehemu ya wimbo huo yenye maishairi yasemayo “Kapteni Komba, familia yako umeiacha na nani, chama chako umekiacha na nani. Nenda baba, msalimie Mwalimu, mweleze hali ya Watanzania ilivyo hivi sasa, mweleze hali ya nchi yetu ilivyo hivi sasa hasa wakati huu, msalimie Mzee Kawawa Simba wa Vita”.
Baada ya kuimba sehemu hiyo ya wimbo huo uliotungwa na Komba mwaka 1999 wakati kifo cha Mwalimu Nyerere na ambao umebadilishwa maneno na kupewa jina la “Nani Yule”, waombolezaji mbalimbali walionekana kuguswa hisia zao.
Wakati Nape akiwa amerudi nyuma na kuinamisha kichwa chini, Rais Jakaya Kikwete, Rais wa Serikali ya Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, Spika Anne Makinda, wabunge na viongozi wengine walionekana kububujikwa na machozi.
 Wengi waliohojiwa walielezea kuwa nchi imejaa maovu yanayofanywa na watu wenye dhamana, mamlaka na nyadhifa katika taifa, wakitaja ufisadi, rushwa, ubinafsi, ubadhirifu na hata hali ya kisiasa kuwa mbaya na hivyo hayo ndiyo angeelezwa Mwalimu Nyerere, ambaye aliongoza harakati za uhuru wa Tanganyika na anasifika kwa kupinga maovu hayo kwenye jamii.
“Kwa mtazamo wangu, kama Komba akikutana na Nyerere ningependa amwambie kwamba, Tanzania ya leo inanuka rushwa viongozi wa Serikali hawana maadili, bora angekuwepo yeye,” alisema Gervas Mbaya, mkazi wa Nyegezi wilayani Nyamagana, Mwanza.
Imani Hezron, Mkazi wa Nyakato alisema: “Amwambie Mzee Nyerere kwamba alipoondoka aliacha kilimo kama uti wa mgongo wa taifa, leo si hivyo tena, na taifa halipigani vita kuondoa umasikini ujinga wala maradhi.”
Mkazi mwingine anayeishi Chuo Kikuu cha St Augustine cha Mwanza, Sarah Onesimo, alisema: “Ningependa amwambie Mwalimu Nyerere kuwa Tanzania imechafuka kwa mauaji ya albino... mauaji yanazidi kuongezeka, huku jitihada ya kudhibiti hazionekani na kama angejaliwa kuwepo, pengine yote haya yasingetokea.”
source: mwananchi