Bunge la
Katiba limeanza kujadili Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba katika sura ya
kwanza na sura ya sita ambayo kwa kiasi kikubwa inahusu Muundo wa
Muungano.
Sura hizi
mbili, ndizo ambazo zinaelezwa kuwa ni roho ya mjadala wa Katiba katika
Bunge hilo Maalumu kwa kuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, imependekeza
Muundo wa Muungano wa serikali tatu katika sura hizo na ibara nyingi
katika rasimu inayojadiliwa, zinajengwa kwa muundo huo wa Muungano.(Hudugu Ng'amilo)
Wakati
akiwasilisha Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba bungeni Jaji, Joseph Warioba
alitoa sababu nyingi za tume kufikia kukubali mapendekezo ya wananchi
kuhusu serikali tatu.
Miongoni
mwa sababu kubwa ni pamoja na sasa Muungano kubadilika kuwa ni wa
serikali mbili na nchi mbili, Muungano ambao siyo ule ulioachwa na
waasisi Hayati Julius Nyerere na Abeid Karume wa serikali mbili nchi
moja.
Nchi
mbili ndani ya Muungano, zimetokana na Mabadiliko ya Kumi ya Katiba ya
Zanzibar ya Mwaka 1984, ambayo yalifanyika mwaka 2010.
Katika
mabadiliko hayo yaliyopo katika sehemu ya kwanza tu ya Katiba ya
Zanzibar yanasema Zanzibar ni nchi ambayo eneo la mipaka yake ni eneo
lote la Visiwa vya Unguja na Pemba pamoja visiwa vidogo vilivyoizunguka
na bahari yake ambavyo kabla ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar
ikiitwa Jamuhuri ya Watu wa Zanzibar.
Zanzibar ni sehemu ya Muungano
Namba
mbili katika katiba hiyo sehemu ya kwanza, inaeleza kuwa Zanzibar ni
miongoni mwa nchi mbili zilizounda Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Sehemu ya
pili(a) inaeleza kuwa , kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za
Serikali, Rais anaweza kuigawa Zanzibar katika mikoa, wilaya na maeneo
mengineyo kwa kufuata utaratibu uliowekwa na sheria iliyototungwa na
Baraza la Wawakilishi.
Katiba ya
Zanzibar pia imebadili masharti ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano
inayosema Sheria za Muungano zinazotungwa na Bunge la Jamhuri, zitume
sehemu zote, lakini kwa sasa Zanzibar ili Sheria ya Muungano itumike ni
lazima ipelekwe Baraza la Wawakilishi.
"Maana yake ni kuwa, Katiba ya Zanzibar ipo juu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano," anasema Jaji Warioba.
Kutokana
na utata huu, Mjumbe wa Bunge la Katiba, Hamad Yusuph Masauni alifanya
mahojiano na gazeti hili na kueleza ifuatavyo;Swali: mababadiliko ya
Katiba ya Zanzibar ya mwaka 2010, yanatajwa kuwa moja ya mambo ambayo
yamechangia sana mapendekezo ya Serikali tatu, je nini maoni yako?
Jibu: Ni
kweli kuwa yamefanyika mabadiliko hayo, lakini kwa ufahamu wangu mimi
nadhani Zanzibar hawajavunja Katiba, kwani kusema tu Zanzibar pia Katiba
ya Zanzibar kumpa Mamlaka Rais kuigawa katika mikoa na wilaya siyo
kosa.
Swali:
lakini jambo hili linatajwa kuwa nyeti kwani kwa kiasi kikubwa licha ya
matatizo mengine, inaonekana ndilo limebariki uwepo wa serikali tatu.
Jibu:
Hapana. Kwanza naomba ieleweke Suala la Tawala za mikoa siyo la Muungano
hivyo, haimzuii Rais wa Zanzibar kugawa mikoa na wilaya kwani jambo
hili si la Muungano.
Swali: Unadhani ni kwa nini Zanzibar imefikia kufanya mabadiliko haya makubwa ya Katiba yake?
Jibu:
Mimi sioni kama kuna tatizo, lakini kwa kuwa sasa tunatengeneza Katiba
ya Muungano ni vyema tukafanya marekebisho kama tunataka kulifanya suala
la tawala wa mikoa liwe la Muungano.
Swali:
Masauni wewe ni mbunge wa Jamhuri wa Jimbo la Kikwajuni Zanzibar. Hivi
sasa kuna mjadala mzito juu ya Muundo wa Serikali nini maoni yako?
Jibu: Mimi naunga mkono msimamo wa chama changu na wananchi wa jimbo langu kuendelea na muundo wa serikali mbili.
Swali:
Lakini muundo huu unaonekana kulalamikiwa na Wazanzibari wengi kutokana
na hoja kuwa Tanganyika imevaa koti ya Muungano na fedha nyingi
zinaendesha Maendeleo ya Tanganyika badala ya Zanzibar.
Jibu: Ni
kweli kuna madai hayo, lakini naamini changamoto hizi zitapatiwa
ufumbuzi kama ambavyo aliahidi Rais Jakaya Kikwete alipokuja kuzindua
bunge.
Swali:
Lakini hata baada ya bunge kuzinduliwa na kutolewa ahadi hizo na Rais
Wazanzibari na hata wanaounga mkono mfumo wa Serikali tatu, wanasema
hata katika bunge hilo bado kunaonyesha Zanzibar kumezwa. Nini Maoni
yako?
Jibu:
Hayo ni madai ya wanasiasa wachache ambao wana malengo ya kushika dola
kama mfumo wa Serikali tatu, ukipita lakini mimi binafsi naamini
Zanzibar haijamezwa bungeni kwanza katika kamati zote kama Mzanzibari
siyo mwenyekiti basi ni makamu.Swali: Je, wewe binafsi kwa mtazamo wako
unaona ni Muundo wa Serikali ngapi unafaa na je, wananchi wa jimbo lako
watakuelewa kwa kutetea msimamo wa chama chako?
Jibu:
Mimi naunga mkono serikali mbili na hakika nikirudi na serikali tatu
wananchi wangu hawatakubali sio kwa sababu jimbo langu wana ccm ni wengi
lakini wana hoja.
Swali:
Baraza la Wawakilishi limetajwa pia kupendekeza muundo wa serikali tatu,
hasa kutokana na hoja yao, kutaka Zanzibar yenye Mamlaka, Tanganyika
yenye Mamlaka na kujulikana Mamlaka ya Muungano.
Jibu:Binafsi siwezi kuzungumzia maoni ya wawakilishi lakini nadhani tatizo ni tafsiri tu zinachanganya watu.
Swali:
Unadhani sasa Bunge hili la Katiba linaweza kusaidia kuondoa matatizo ya
Zanzibar na hata Tanganyika katika mfumo wa Muungano uliopo?
Jibu:
Ndio kwani Bunge hili lina jukumu kubwa la kutunga sheria ambazo ndizo
zitakuwa kuu kwa pande zote na kuondoa kero za muda mrefu kwa kila
upande.
Swali: Nini hofu yako katika Muundo wa serikali tatu?
Jibu:
Hakuhitaji mtu kuwa ya PhD kujua kuwa serikali tatu zitaua muungano
wetu, hofu yangu mimi bila Serikali mbili muungano unakwenda kufa.
Swali: Nini maoni yako ya jumla kuhusu Bunge Maalumu la Katiba?
Jibu:
Mimi wito wangu kwa wajumbe,tutengeneze Katiba hii kwa maslahi ya
wananchi na sio masilahi yetu. Hakuna wananchi ambao wanataka vurugu
zitokee katika Bunge hili hata baada ya kupitishwa mapendekezo ya
Katiba.
Mussa Juma ni mwandishi wa mwananchi.0754296503.
No comments:
Post a Comment