Zitto
Kabwe, Mjumbe, BMK
Iwapo
Tanzania ni Shirikisho (Federation) au ni Muungano (Union) ni jambo ambalo
limekuwa likuzua utata kwa miaka mingi. Hivi sasa katika vikao vya Kamati za
Bunge maalumu la Katiba jambo hili limezua mjadala mkubwa ambapo baadhi ya
Wajumbe wanapendekeza kuwa neno Shirikisho litoke kwenye sura ya kwanza ya
Rasimu ya Katiba na wengine wakipendekeza libakie au hata kuweka wazi kabisa
kuwa Tanzania ni Jamhuri ya Shirikisho la Tanganyika na Zanzibar. Maoni haya
yanatokana na misimamo ya wajumbe kuhusu muundo wa Muundo wa Muungano kwa maana
ya idadi ya Serikali. Ni vema dhana hizi kueleweka vizuri ili watumiaji waweze
kuzitumia kwa usahihi. Kwa ufupi tutazame maana ya kila dhana na mifano
mbalimbali duniani. Tutatazama dhana tatu kuu - Muungano (Union), Shirikisho
(Federation) na Jumuiya (Confederation/Community).
Muungano
(Union)
Katika
aina hii ya Nchi kuungana huundwa Taifa moja, Dola moja ndani ya Nchi moja.
Katika muundo huu Serikali za Washirika wa Muungano huachia sehemu kubwa ya
madaraka yao kwa Serikali ya Muungano. Mara nyingi muundo huu hupelekea kuwapo
kwa Serikali moja yenye nguvu ya Muungano na kama Washirika wanabakia na
Serikali zao, basi hubakia na mambo machache sana. Faida ya Muundo huu ni
kwenye uimara wake na sio rahisi kuvunjika. Hasara za muundo huu ni athari ya
moja ya nchi, hasa kama ni ndogo, kumezwa na Mshirika mkubwa. Hapa Afrika Nchi
ya Afrika ya Kusini (Republic of South Africa) inafuata muundo huu wa Muugano
ambapo Serikali ya Muungano ina nguvu na mamlaka mengi kuliko Serikali za
Majimbo yanayounda Jamhuri ya Afrika ya Kusini. Huko Asia mfano mzuri ni Nchi
ya India ambapo japo muundo wake unatoa nguvu kubwa kwa Majimbo kujitawala,
Serikali ya Muungano (Union Government) ina nguvu kubwa zinazoondoa sifa ya
kuitwa Shirikisho. Sio lazima 'Union' kuwa na Serikali moja (Unitary State)
isipokuwa mazingira ya nchi husika ndio yanaweza kuamua. Mfano mzuri hapa ni
ule wa Afrika ya Kusini ambayo ni 'unitary state' yenye Serikali 10, tisa za
Majimbo na Moja ya Muungano.
Shirikisho
(Federation)
Katika
muundo huu Serikali za Washirika hukasimu sehemu ndogo ya madaraka yake kwa
Serikali ya Muungano. Mambo ya kidola (sovereign functions) hufanywa na
Serikali ya Shirikisho na Serikali za Washirika kubakia na mambo yake yenyewe.
Kwa mujibu wa Sheria za kimataifa nchi yenye mfumo wa Shirikisho kuwa ni nchi
moja katika sura ya kimataifa ingawa inawezaonekana ni nchi zaidi ya moja ndani
ya Shirikisho husika. Faida kubwa ya muundo huu ni kuondoa hofu ya mkubwa
kummeza mdogo na ule uhuru wa kujiamulia mambo mengi. Hasara ya muundo huu ni
kujengwa kwa utaifa au hisia za utaifa za Washirika ambazo hatimaye hupelekea
Shirikisho kuvunjika. Hapa Afrika mfano mzuri wa Shirikisho ni nchi ya Ethiopia
ambapo Majimbo yake yanao uwezo hata wa kujitoa katika Shirikisho kikatiba.
Eritrea ilitumia fursa hii na kujitoa kuwa sehemu ya Ethiopia mara baada ya
mapinduzi yaliyomtoa Mengistu Haile Mariam. Ujerumani pia ni Shirikisho
(Federal Republic of Germany au kwa kijerumani BundesRepublik Deutschland)
Jumuiya
(Confederation/Community)
Katika
muundo huu kila Mshirika anakuwa na uhuru wa mambo yake yote isipokuwa tu
kunakuwa na mambo ya uratibu wa pamoja. Aina hii ya Muundo ndio unapaswa kwa
kinachoitwa Muungano wa Mkataba. Faida kubwa ya muundo huu ni kwamba hakuna
kubanana na pale kunapotokea hofu Mshirika hujitoa. Hasara yake imo kwenye
faida yake.Mfano mzuri ni Switzerland na Jumuiya ya Ulaya. Hata Jumuiya ya Afrika
Mashariki pia inaitwa kuitwa ni Muungano wa Mkataba.
Muundo
gani Tanzania?
Tanzania
kuwa Shirikisho au Muungano ni mjadala ambao utaendelea kuwapo licha ya kuamua
kuchagua muundo mmoja wapo. Wakati wa kuandika Katiba ya India mwaka 1947
ubishani huu ulikuwa mkubwa sana pia. Katiba ya India imegawanya mamlaka katika
sehemu tatu - Mambo ya Muungano, Mambo ya Washirika na Mambo ya pamoja
(concurrent). Wajumbe wa Bunge la Katiba la India wanaotaka Shirikisho
walipinga muundo huo na kukataa 'Washirika kuwa ombaomba kwa Serikali ya
Muungano'. Hata hivyo ubishi huo ulimalizwa na Mwanasheria mahiri wa India
bwana B M Ambedkar kwa kusema 'tunataka Serikali imara ya Muungano na yenye
nguvu iwezekanvyo' na alifunga mjadala kwa kusema 'Muungano wa Washirika unatakiwa
zaidi kuliko Shirikisho la Washirika'. Hivi ndivyo ilivyo India ambapo pamoja
kwamba ni Shirikisho lakini ni 'Unitary'. Vile vile Jamhuri ya Afrika ya Kusini
ina muundo sawa sawa na nchi ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani lakini
wakati Ujerumani ni Shirikisho, Afrika Kusini ni Muungano (Unitary).
Watanzania
hatupaswi kuiga isipokuwa kujifunza kwa nchi nyingine. Hivyo muundo gani unafaa
ni uamuzi wetu wenyewe. Hata hivyo uamuzi huo ni lazima ujibu vigezo fulani
fulani. Vigezo vikubwa ni viwili; Je, Muundo tunaoutaka utajibu kero
(malalamiko) za Muungano wa sasa? Je, Muundo tunaoutaka utajibu hofu za
Muungano kuvunjika. Muundo utakaojibu hofu hizo ndio utakaotufaa. Tanzania
inaweza kuwa na Muundo wa Muungano wenye Serikali tatu ama Muundo wa Shirikisho
wenye Serikali mbili, ama kinyume chake. Idadi ya Serikali haina uhusiano
wowote na ama tunaitwa Shirikisho au Muungano. Mifano miwili hapo juu
ituongoze, India ni Muungano unaitwa Shirikisho na Afrika Kusini ni Shirikisho
linaloitwa Muungano. Tanzania inaweza kuwa vyovyote vile ili mradi tu kunakuwa
na Mamlaka ya kutosha katika masuala ya Muungano ili kuiweka Nchi pamoja na
kuwa na Taifa imara mbele ya mataifa ya ulimwengu.
Muungano
wa Serikali 3 na sio Shirikisho la Serikali 3 ndio mapendekezo yangu. Muungano
(Union) wa Washirika ni bora, imara na endelevu zaidi kwa mazingira ya Afrika
kuliko Shirikisho (Federation) la Washirika.
Mapendekezo
yangu mahususi yaliyowasilishwa kwenye kamati namba 12 ni kama ilivyo hapa
chini.
SURA
YA KWANZA
SEHEMU
YA KWANZA
1(1)
Irekebishwe na kuandikwa upya na isomeke
Tanzania
ni Nchi Moja na ni Jamhuri ya Muungano yenye mamlaka kamili ambayo imetokana na
Muungano wa Nchi za Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar ambazo
kabla ya Hati ya Makubaliano ya Muungano ya Mwaka 1964, zilikuwa nchi huru.
1(2)
neno Shirikisho lifutwe na kuongeza maneno ....Nchi ya.... baada ya neno 'ni'
na kabla ya neno 'kidemokrasia'
Ongeza
ibara ya mpya ya 3 itakayosomeka
3(1)
Shughuli zote za Mamlaka ya Nchi katika Jamhuri ya Muungano zitatekelezwa na
kudhibitiwa na vyombo vitatu vyenye mamlaka ya Utendaji, vyombo vitatu vyenye
mamlaka ya kutekeleza utoaji haki, na pia vyombo vitatu vyenye madaraka ya
kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma
3(2)
Vyombo vyenye Mamlaka ya Utendaji vitakuwa ni Serikali ya Jamhuri ya Muungano,
Serikali ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika; vyombo vyenye Mamlaka ya
kutekeleza utoaji haki vitakuwa ni mahakama ya Juu ya Jamhuri ya
Muungano, Mahakama ya Tanganyika na Mahakama ya Zanzibar na vyombo vyenye
Mamlaka ya ya kutunga sheria na kusimamia utekelezaji wa shughuli za umma
vitakuwa ni Bunge la Jamhuri ya Muungano, Baraza la Wawakilishi la Tanganyika
na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar.
3(3)
Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za umma katika Jamhuri ya Muungano,
na kwa ajili ya mgawanyo wa madaraka juu ya shughuli hizo baina ya vyombo
vilivyotajwa katika ibara hii, kutakuwa na mambo ya Muungano kama
yalivyoorodheshwa katika Nyongeza ya Kwanza ya Katiba hii, kutakuwa na mambo ya
uratibu wa pamoja na kutakuwa na mambo yasiyo ya Muungano ambayo ni mambo
mengine yote yasiyo mambo ya Muungano na yasiyo ya uratibu wa pamoja.
3(4)
Kila chombo kilichotajwa katika ibara hii kitaundwa na kutekeleza majukumu yake
na Katiba za Serikali za Washirika na kwa kufuata masharti ya katiba hii.
3(5)
Kwa ajili ya utekelezaji bora wa shughuli za Serikali ya Jamhuri ya Muungano au
Serikali ya Tanganyika au Serikali ya Zanzibar Bunge laweza kuigawa Jamhuri ya
Muungano katika Mikoa kwa mujibu wa Sheria iliyotungwa na Bunge Isipokuwa
kwamba Bunge litapata kwanza Azimio la Baraza la Wawakilishi la Tanganyika kwa
mikoa ya Tanganyika au Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa mikoa ya Zanzibar.
SABABU
ZA MAREKEBISHO YANAYOPENDEKEZWA.
Rasimu
ya Katiba imetangaza tu kuwa 'Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(JMT)
ni Nchi' na kuacha 'ambiguity' ya kwamba Tanzania ni nchi ngapi.
Katiba
ya sasa imetamka bayana kuwa 'Tanzania ni Nchi Moja'. Rasimu pia imetamka
kwamba JMT inatokana na 'muungano wa nchi mbili'. Hivyo basi ni vema kuweka
wazi kabisa kuwa Nchi hizi mbili zimeunda nchi moja. Hii itaepusha migongano ya
siku za usoni kuhusu tafsiri ya Katiba na Mamlaka za Nchi. Ifahamike wazi kuwa
idadi ya Serikali haina uhusiano na uundaji wa nchi moja.
Rasimu
imetangaza kuwa Tanzania ni Shirikisho ingawa bado imetamka 'Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania (United Republic of Tanzania). Dhana za 'Union' na
'Federation' ni dhana mbili tofauti katika miungano.
Idadi
ya Serikali haina mahusiano ya moja kwa moja na aina ya Muungano kama ni
'Union' au ni 'Shirikisho'. Kwa mazingira ya Nchi za Kiafrika ni salama zaidi
kuwa na 'Union' kuliko Shirikisho. Kwa kutumia maneno ya Mwanasheria gwiji na
mwandishi wa Katiba ya India Bwana B M Ambedkar, "Muungano wa Washirika unatakiwa
zaidi kuliko Shirikisho la Washirika". Ni vema kuwa na Muungano wenye
Serikali ya Muungano yenye nguvu iwezekanavyo ili kuhimili vishindo na
changamoto dhidi ya Nchi yetu na umoja wetu bila kuathiri uhuru wa Serikali za
Washirika kuendesha mambo yao wenyewe bila bugudha.
Rasimu
imeweka sura ya Kwanza bila kutaja vyombo vya Jamhuri ya Muungano. Ni vema ili
kuondoa 'ambiguity' vyombo vya Jamhuri ya Muungano kutajwa kinagaubaga katika
Katiba ya Jamhuri ya Muungano katika sura ya 'uundwaji wa nchi'. Mapendekezo ya
ibara mpya za sehemu ya kwanza ya sura ya kwanza yanazingatia tahadhari hiyo.
Katika kutaja vyombo mapendekezo haya yanaonyesha dhahiri kuwa ugawaji wa Nchi
katika Mikoa inakuwa ni mamlaka ya Bunge. Serikali za Washirika zaweza kuwa na
mamlaka ya Serikali za Mitaa. Mikoa inapaswa kuwa mamlaka ya Bunge la Muungano
kwa sababu yaweza pia kutumika katika kupata Wabunge wa Muungano lakini pia
itasaidia kuondoa tabia ya kugawa mikoa hovyohovyo. Kimsingi ilipaswa
Mikoa yote ya Nchi itajwe ndani ya Katiba kuongezeka au kupunguka kwake
kutokane na maamuzi maalumu ya Bunge hata ikibidi iwe kwa theluthi mbili.
SURA
YA SITA
Ibara
ya 60(1) maneno shirikisho yafutwe na kubaki uwepo wa Serikali 3.
60(3)
isomeke
Muundo,
madaraka na mambo mengine ya kiutendaji yahusuyo Serikali ya Tanganyika, na
Serikali ya Zanzibar yataanishwa katika Katiba za Washirika na kwa kuzingatia
masharti ya Katiba hii.
Ibara
ya 63 iitwe 63(1)
Iongezwe
63(2)
Kwa
ajili ya uratibu bora wa shughuli za Mamlaka za Nchi na kwa ajili ya
kuhakikisha ufanisi na weledi katika uendeshaji bora wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania na mgawanyo wa madaraka, Serikali ya Jamhuri ya Muungano
itakuwa na mamlaka ya uratibu juu ya mambo ya uratibu kama yalivyoorodheshwa
katka nyongeza ya pili ya Katiba hii.
64(1)
maneno nchi washirika yaondoke na kubakia neno Washirika au Washirika wa
Muungano.
64(5)
isomeke
Serikali
za Washirika zitakuwa na hadhi na haki sawa ndani ya Jamhuri ya Muungano na
zitatekeleza majukumu yao kwa mambo yote yasiyo ya Muungano katika mamlaka za
Serikali za Washirika kwa mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za
Serikali za Washirika kwa kuzingatia masharti ya Katiba hii.
65
maeneo yote yenye maneno Nchi Washirika yafutwe na kuandikwa Washirika wa
Muungano
67
ifutwe yote
69
maneno Nchi yafutwe ....katiba za Washirika.......
69
(2) maneno Viongozi wakuu yafutwe na kuandikwa ' Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania na Wakuu wa Serikali za Washirika watakuwa ni Viongozi Wakuu wa Nchi'
69(3)
isomeke
Viongozi
wanaohusika na masharti ya ibara hii ni
(a)
Rais wa Jamhuri ya Muungano
(b)
Mkuu wa Serikali ya Tanganyika ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano
(c)
Mkuu wa Serikali ya Zanzibar ambaye pia atakuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri
ya Muungano.
Ongeza
ibara ya 70
(1)
Mkuu wa Nchi ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye ataitwa Rais atapatikana
kwa kuchaguliwa kwa kura na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano kwa Mujibu wa
masharti ya Katiba hii. Rais atakuwa pia Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya
Muungano.
(2)
Wakuu wa Serikali za Washirika watapatikana kutoka kwenye Mabaraza ya
Wawakilishi ya Washirika kutoka Chama cha siasa chenye wawakilishi wengi kwa
mujibu wa masharti yatakayowekwa na Katiba za Washirika na kwa kuzingatia
masharti ya Katiba hii.
SABABU
ZA MAPENDEKEZO
Lengo
ni kuhakikisha kuwa Jamhuri ya Muungano inabakia ni nchi moja yenye serikali 3
zenye mamlaka na madaraka yake yaliyofafanuliwa na katiba. Kwa kuwa tunaamua
kuwa na Nchi moja basi Serikali zinazoundwa zitakuwa ni Serikali Washirika na
sio nchi Washirika tena kama rasimu inavyoita. Kuweka wazi kuwa ni kiongozi
mmoja tu wa Serikali ndio atachaguiwa na wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano
naye ni Rais - Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi ya Ulinzi na
usalama.
Majina
ya Wakuu wa Serikali za Washrika yatatolewa na kwa mujibu wa Katiba zao na
hivyo hakuna sababu kwa Katiba ya Muungano kuunda majina isipokuwa tu Wakuu wa
Serikali za Washirika watakuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa
kuzingatia kuwa iwapo Rais wa Muungano anatoka upande mmoja wa Muungano, makamu
wa kwanza atatoka upande wa pili wa Muungano. Makamu wa Rais wanaweza kukaimu
Urais kwa masharti maalumu yatakayowekwa na Katiba.
Mapato
na mgawanyo wa Mapato ya Muungano katika Serikali Tatu
Dola
inapasa kuwa na rasilimali za kutosha na ziada inaweza kugawa kwa Washirika na
Mikoa katika wajibu wa kuhakikisha maendeleo yanawiana. Dola pia inaweza kuwa
na miradi ya Muungano. Kuna haja ya kuangalia kwa umakini mkubwa suala hili la
mapato ya Serikali ya muungano kama kweli kuna nia ya dhati ya kuendelea kuwa
na Muungano. Mapendekezo yangu ni kama ifuatavyo;
Mapato
ya Muungano
1.
Ushuru wa Forodha
2.
Mrahaba wa uvunaji wa Rasilimali ambapo 25% itabaki kwenye mkoa wenye
rasilimali na 75% itatumika na Serikali ya Muungano kugawa kwenye mikoa kwa
mujibu wa ‘formulae’ itakayokubaliwa kwa kuzingatia idadi ya watu, kiwango cha
umasikini na ukubwa wa kijiografia.
3.
Ushuru wa Bidhaa na huduma ambapo 60% itagawiwa kwa nchi Washirika kwa ajili ya
miradi maalumu ya muungano.
4.
Mapato kutoka kwenye kampuni za kibiashara za Serikali ya Muungano na gawio la
Benki Kuu ya Tanzania.
Mapato
ya Serikali za Washirika
1.
Kodi ya Mapato ya watu binafsi na Makampuni 2. Kodi ya Ongezeko la Thamani au
kodi kama hiyo 3. Tozo mbalimbali zitakazotungwa kwa mujibu wa sheria 4. Mapato
yasiyo ya kikodi kutoka idara na Wizara za Serikali.
Mapato
ya Mikoa
1.
25% ya Mrahaba kutokana na uvunaji wa Rasilimali/maliasili inayopatikana katika
mkoa husika 2. 10% ya makusanyo ya kodi ya mapato ya watu binafsi na makampuni
kutoka katika mkoa husika 3. Mgawo kutoka Serikali ya Muungano 4. Mgawo kutoka
Serikali ya Washirika 5. Tozo mbalimbali zitakazoanzishwa kwa mujibu wa sheria
ndogo ndogo zitakazopitishwa na Mabaraza ya Mikoa
Dodoma,
Aprili
2014
No comments:
Post a Comment