Dodoma. Kundi la Tanzania Kwanza linaloundwa na
baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba limelaani hatua ya kundi la Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kwa kususia vikao vya Bunge hilo
linaloendelea mjini hapa.
Mwenyekiti wa Tanzania kwanza Said Nkumba akizungumza na waandishi wa habari jana alisema, kundi lake linakichukulia kitendo cha Ukawa kama usaliti ili kuwapotezea matumaini wananchi ya kupatikana kwa Katiba Mpya kama ilivyokusudiwa.
“Tunachukulia kama usaliti kwa wananchi ambao wana matumaini ya kupata Katiba itakayopendekezwa na itakayolenga kuwaondolea kero za maisha hivyo kuwawekea misingi imara ya maendeleo,” alisema Nkumba.
Alisisitiza, “Kwa kitendo hiki, Tanzania Kwanza tunawaambia wananchi hawa Ukawa hawana nia njema wala uchungu na nchi hii na kwani sababu wamekimbia na kuacha nafasi ya kuwatetea wanawake, watoto na watu wenye ulemavu, vijana na wazee pamoja na makundi mbalimbali ya kijamii,” alisema.
Nkumba alisema kundi la Tanzania Kwanza linawatoa hofu wananchi kwa kuwa mchakato utaendelea kwa kushirikiana na wale wenye uchungu na wanaotambua wajibu wao katika kulienzi taifa kwa kuhakikisha wanafanikisha lengo lililokusudiwa.
Alisema Ukawa walionyesha nia ya kukwamisha mchakato huo kwa visingizio mbalimbali ikiwamo la kubishana kuhusu upigaji wa kura wakitaka kura za siri lakini waliporuhusiwa kupiga za siri na wazi wakaanza kuwalazimisha wajumbe wao kupiga kura za wazi.
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment