WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, April 13, 2014

Kikwete: Sokoine ni alama na kielelezo cha uongozi bora

  Mtoto wa Sokoine aliza baadhi ya umati
Rais Jakaya Kikwete akiweka shada la maua katika kaburi la aliyekuwa waziri Mkuu wa Tanzania hayati Edward Moringe Sokoine.
Rais Jakaya Kikwete, amesema taifa halipaswi kulia kutokana na kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Moringe Sokoine, kwa sababu kufanya hivyo ni sawa na kukata tamaa na kushindwa kuenzi mfano wa maisha yake ya uadilifu na uaminifu katika kazi alizofanya.
Aliwataka  Watanzania kusherehekea ushindi wa maisha yake kwa kuwatumikia wananchi bila ubaguzi wa aina yo yote, upendeleo wala tabia ya kujilimbikizia mali na ardhi ili kumuenzi kwani alikuwa alama na kielelezo cha uongozi bora nchini.

Akizungumza katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha Sokoine yaliyofanyika nyumbani kwake Monduli Juu jana na kuhudhuriwa na umati mkubwa watu kutoka maeneo mbalimbali nchini, Rais Kikwete alimuelezea Sokoine kama shujaa na kwamba shujaa hapaswi kuliliwa bali kuenziwa.

“Sokoine alikuwa kiongozi aliyetambua kuwa kiongozi hodari hupimwa wakati wa matatizo, hivyo alikuwa mwadilifu aliyechukia sana maovu, alikua mkweli na mchapakazi, aliyepata faraja kuona matatizo ya wananchi yanapatiwa ufumbuzi haraka,” alisema.

Alisema  alikuwa kiongozi aliyependa elimu hata kuacha nafasi ya u Waziri Mkuu na kwenda kusoma tofauti na na wengi  ambao wakiwa madarakani hawapendi kufanya hivyo.

Pia alimwelezea kuwa hakuwa kiongozi aliyependa kujilimbikizia ardhi na akatoa mfano wa ekari 128 ambazo aliahidi kuzitoa kwa Kanisa Katoliki ili wajenge chuo cha maendeleo.

Alisema siku moja kabla ya Sokoine kufariki dunia kwa ajali ya gari akitokea bungeni mjini Dodoma, bunge lilipitisha Sheria namba 6 ya kuanzisha Chuo Kikuu  cha Kilimo, lakini baada ya kufa kwake serikali iliona vema kumuenzi kwa chuo hicho kutumia jina lake.

Alisema serikali ina azma ya kupanua na kukiboresha chuo pamoja na kukamilisha ujenzi wa Shule ya Sekondari itakayokuwa ikichukua mchepuo wa sayansi, na kwamba shule hiyo itajengwa eneo  alikopata ajali.

Pia alisema serikali imepanga kujenga Chuo Kikuu cha Mwalimu Nyerere huko Butiama, kwa lengo la kumuenzi Rais Julius Kambarage Nyerere.

Askofu Mkuu Lebulu:
Mapema Askofu  Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Arusha, Josephat Lebulu, aliyekuwa akiongoza misa ya kumbukumbu ya kifo cha Sokoine,  alisema  umati wa watu waliokuja kuadhimisha kumbukumbu ya miaka 30 ya kifo cha Sokoine ni kielelezo cha sifa ya kwanza aliyokuwa nayo ya kumcha Mwenyezi Mungu na nyingine ikiwa ni kujali utu na watu aliokuwa akiwaongoza.

Mahubiri hayo yaliyofanyika nyumbani kwa Hayati Sokoine Monduli Juu jana, Askofu Mkuu Lebulu alisema watu hao wamekusanyika hapo kwa sababu Sokoine alikuwa mtu aliyewajali na kuwapenda watu aliokuwa akiwaongoza bila ubaguzi wo wote wa kikabila, dini au kiitikadi.

“Hatukuja hapa eti kwa sababu Sokoine ni wa familia yako, eti kwa sababu Sokoine alikuwa rafiki yako, eti kwa sababu Sokoine alikuwa wa kabila lako.

“Hata familia yake haikutaka tuje hapa kwa sababu ya kumuenzi yeye,  au ni kwa sababu alikuwa wa dini na madhehebu ya Kikristo au kwa sababu alikuwa ni mwanachama wa CCM la, tumekuja hapa kwa sababu alikuwa Mcha Mungu na mtu aliyekuwa akijali utu na watu,” alisema.

Ibada hiyo ilihudhuriwa na Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wastaafu Dk Salim Ahmed Salim, Edward Lowassa, Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Anne Makinda, baadhi ya mawaziri, wabunge, wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba wakiongozwa na Paul Kimiti, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa na serikali.

Sheikh Mkuu Mkoa wa Arusha:
Wa kwanza kutoa dua alikuwa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Juma, ambaye alitaja sifa nyingi ambazo Sokoine alikuwa nazo kama vile ukweli, upendo na alikuwa akifanya kazi bila ubaguzi wo wote wa kidini, kikabila na kiitikadi.

Familia yatekeleza ahadi ya baba yao:
Familia ya Sokoine jana ilikabidhi hati ya eneo la shamba la ukubwa wa ekari 128 kwa Kanisa Katoliki kwa ajili ya kujenga chuo cha maendeleo kwa wakazi wa eneo hilo.

Pia waliahidi kutekeleza ahadi yake ya kutoa asilimia 10 ya mshahara wake na mbuzi kama mchango wake kanisani na walisema watatekeleza ahadi hiyo.

Lowassa anena:
Lowassa alimshukuru Rais Kikwete kwa kukubali kuja kuwa mgeni rasmi  kwenye kumbukumbuku hiyo na kuwapatia matamba na ujenzi wa malambo ya maji. “Ulitujua wakati wa njaa na sisi tunahaki ya kukushukuru na wananchi wa Monduli wanakupenda,” alisema.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment