Sasa serikali mbili kupingwa nchi nzima
Prof. Shivji ashambuliwa kuwa kigeugeu
Prof. Shivji ashambuliwa kuwa kigeugeu
Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba, Tundu Lissu na Ismail Jussa,Wakizungumza na wandishi wa habari jana mjini Dodoma.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), umehamishia mapambano yake nje ya Bunge la Maalumu la Katiba ili kuhakikisha kwamba Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba haichakachuliwi.
Kuanzia jana viongozi wa Ukawa inayoundwa na vyama vya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF) na NCCR-Mageuzi walianza kukutana na wananchi kupitia mikutano ya hadhara jijini Mwanza na kuwaeleza kwamba ikiwa rasimu itachakachuliwa waikatae wakati wa kupiga kura ya maoni kwa ajili ya kuipitisha Katiba hiyo.
Katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika uwanja wa Mirongo, Katibu Mkuu Chadema, Dk. Willibrod Slaa, aliwataka Watanzania wapige kura ya hapana, ikiwa CCM kupitia wingi wa wabunge wao katika Bunge Maalumu la Katiba watashinikiza muundo wa serikali mbili badala ya serikali tatu kama ilivyopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Hata hivyo, alimshangaa Prof. Issa Shivji kwa kuunga mkono muundo wa serikali tofauti na kauli aliyowahi kuitoa miaka kadhaa iliyopita kuwa Zanzibar inastahili kuwa nchi kamili.
“Mimi ninawashauri Watanzania wenzangu msikubali kuburuzwa iwapo CCM kwa kutumia wingi wa wajumbe kwenye Bunge Maalum la Katiba wataamua muundo wa serikali mbili badala ya maoni yenu kuwa mnataka muundo wa serikali tatu...kwa hiyo mpige kura ya hapana," alisema Dk. Slaa huku akishangiliwa na umati wa wananchi.
Alisema hotuba ya Rais Kikwete baada ya Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu ya Katiba haikuwa na nia njema kwa wananchi, kwa vile ililenga kuwatisha juu ya kuwepo kwa serikali tatu, jambo ambalo ni kuinglia uhuru wa wananchi na kinyume cha katiba iliyopo.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, pamoja na kupokea vitisho kutoka CCM na serikali yake, Ukawa wataendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu wajibu wao katika mchakato wa kupa Katiba mpya.
Alisema baada mkutano wa Mwanza, yeye na makatibu wengine wa NCCR-Mageuzi na CUF watapanga ni lini mikutano kama hiyo itafanyka kayika mikoa ya Mbeya, Tanga, Rukwa, Ruvuma na visiwani Zanzibar.
Kaimu Katibu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Bara, Abdul Kambaya, alisema hotuba iliyotolewa na Rais Kikwete iliegemea upande wa chama chake.
Naye Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mozena Nyambabe, aliwataka wananchi kupiga kura ya hapana ikiwa CCM inayotetea serikali mbili itashinikiza muundo wa sasa wa muungano uendelee.
LISSU, JUSSA WAMSHANGAA SHIVJI
Katika hatua nyingine, siku moja baada ya Prof. Shivji kuonya juu ya muundo wa serikali tatu, wajumbe wawili wa Bunge Maalum la Katiba, wamemjia juu na kusema kuwa anasaliti msimamo na machapisho yake aliyoyasimamia kwa zaidi ya miaka 30 iliyopita kwa lengo la kuifurahisha serikali na CCM.
Wakizungumza na wandishi wa habari jana mjini Dodoma, wajumbe hao, Tundu Lissu na Ismail Jussa Ladhu, walisema wanamshangaa Prof. Shivji kwa matamshi yake na kutoamini kama aliyoyasema ilikuwa ni kwa akili yake au alishinikizwa.
Lissu alisema kuwa msimamo wa sasa wa Prof. Shivji kwamba Muungano wa serikali mbili unapaswa kudumishwa, umeshtua kwa kuwa unapingana na maandiko yake aliyochapisha kwenye vitabu mbalimbali yakipinga Muundo wa serikali mbili.
Lissu ambaye ni mwanafunzi wa Prof. Shivji alisema kutokana na kumpenda mhadhiri huyo aliitwa ‘Mtoto wa Shivji’ na kwamba mwaka 1990 Prof. Shivji alitoa mhadhara wa kiprofesa uliosababisha apewe u-profesa akizungumzia misingi ya kisheria na uhalali wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Alisema kuwa katika mhadhara huo, Prof. Shivji alisema kuwa ili makubaliano ya Muungano yaweze kupata uhalali, ni lazima yatungiwe sheria ya kuridhia makubaliano hayo na mabunge ya nchi washirika.
Alisema kwa mujibu wa Prof. Shivji, upande wa Tanganyika ipo sheria iliyotungwa na Bunge la Tanganyika ya kuridhia Muungano huo, lakini kwa wakati huo hakuwa na ushahidi wowote kama upande wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilitunga sheria hiyo.
“Katika mhadhara huo, Shivji alisema kuwa Bunge la Tanganyika lilitunga sheria kuridhia mapatano ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, lakini hakuwa na ushahidi wa sheria ya aina hiyo kutungwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar,” alisema Lissu akimnukuu Prof. Shivji.
Alisema kuwa miaka 18 baadaye Prof. Shivji aliandika kitabu kingine akisema kuwa katika utafiti wake sasa anao ushahidi kwamba Baraza la Mapinduzi la Zanzibar halikutunga sheria ya kuridhia mapatano ya Muungano.
Alisema Prof. Shivji katika kitabu hicho alichokiita ‘Pan Africanism or Pragmatism’, alisema kuwa sheria ya kuridhia muungano kwa upande wa Zanzibar ilighushiwa na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali la Tanganyika mwaka 1964.
Alisema kwa machapisho hayo, Prof. Shivji alikuwa akipinga muundo wa Muungano wa serikali mbili, lakini anashangazwa na hatua ya sasa ya mhadhiri huyo kugeuka ghafla na kutamka hadharani kuwa muundo huo unapaswa kudumishwa.
Lissu alisema kuwa wamejipanga na wanazo nyaraka zote za kupambana ndani ya Bunge Maalum la Katiba kuhakikisha sasa unaanzishwa muundo wa Muungano usiokuwa na kero kama ilivyo hivi sasa na anaamini kuwa muundo mzuri ni ule uliopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba wa serikali tatu.
“Tumejipanga, tutamjibu Prof. Shivji kwenye vikao vya Bunge Maalum ambapo ndio mahali sahihi pa kujadili Rasimu ya Katiba na kufanya marekebisho yenye maslahi kwa Watanzania wote,” alisema Lissu.
Kwa upande wake Jussa alisema machapisho ya Prof. Shivji ndiyo yaliyochangia kuamsha vuguvugu la Wazanzibari kudai haki kwenye muundo wa Muungano, hivyo anashangazwa na kitendo cha Prof. Shivji kuyageuka machapisho yake na kutangaza hadharani kuunga mkono muundo ambao alikuwa akiukosoa kwa miaka mingi.
Alisema kitendo hicho kimemkwaza kwa kuwa yeye ni miongoni mwa Wazanzibar waliompatia ushirikiano mkubwa wakati akifanya utafiti wa masuala ya Muungano Visiwani Zanzibar.
“Mimi binafsi niliujua vema msimamo wa Prof. Shivji kwa sababu nilitoa mchango wangu kwake wakati akifanya utafiki kiasi cha kufikia hata yeye mwenyewe kunipa heshima kwa kunishukuru katika kitabu chake cha Pan African or Pragmatism kuwa hakuupenda muundo wa serikali mbili, lakini ghafla amegeuka na kuunga mkono, kwa kuwa mhadhara alioutumia uliandaliwa na serikali inawezekana amefanya hivyo kwa shinikizo,” alisema Ladu.
Alisema mbali na Prof. Shivji kutumika kupiga propaganda za CCM, lakini yeye na wenzake waliofundishwa na Prof. Shivji wataendelea kubaki na msimamo thabiti wa kuhakikisha unapatikana muundo wa Muungano wenye usawa kwa nchi zote washirika.
Imeandikwa na Juma Ng’oko, Mwanza na Emmanuel Lengwa, Ashton Balaigwa, Dodoma
CHANZO:
NIPASHE
No comments:
Post a Comment