Ikulu imeeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi yake kwa taifa ya kulipatia Katiba Mpya ifikapo Aprili 26, 2014.
Katibu
Mkuu Kiongozi (KMK), Balozi Ombeni Sefue alilieleza kuwa kwa hali ya
mchakato huo ilivyo sasa, wameshindwa kufikia lengo hilo, lakini
hawajakata tamaa kuhusu kupatikana Katiba Mpya ndani ya mwaka huu.
"Kweli
matarajio ya awali yalikuwa hayo, lakini kama unavyoona hali ilivyo, ni
vigumu kusema matarajio mengine, ingawa majadiliano yaliyofanywa mwaka
huu ni lazima Katiba inayopendekezwa iwasilishwe kwa wananchi na mwakani
tutakuwa na Katiba Mpya," alieleza Balozi Sefue.(Hudugu Ng'amilo)
Katika
hali isiyoeleweka Balozi Sefue alisisitiza msimamo wa awali wa Serikali
kwamba Katiba itakayopatikana itatumika kwenye Uchaguzi Mkuu,
unaotarajiwa kufanyika mwaka ujao.
Dk Slaa
Katibu
Mkuu wa Chama cha Maendeleo na Demokrasia (Chadema), Dk. Willbroad Slaa,
alisema hilo ni fundisho kwa Serikali kwamba kiburi na jeuri havitakiwi
katika masuala yanayohusu umma.
Alisema
muda huo wa kupatikana Katiba Mpya ulipotangazwa, walioanzisha kilio cha
kudai Katiba Mpya nchini ambao aliwataja kuwa ni vyama vya upinzani vya
siasa, taasisi mbalimbali za kijamii walipinga na kutoa ushauri kwa
Serikali, lakini walipuuzwa.
Dk. Slaa
alisema walipendekeza kwamba badala ya kupeleka mchakato wa Katiba
mchakamchaka, warekebishe kwa mara ya 15 Katiba inayotumika, ili iende
na wakati wa sasa ikiwamo Uchaguzi Mkuu ujao kwa lengo la kutoa muda wa
kutosha kwa mchakato wa taifa kupata Katiba Mpya.
"Lakini
walitukebehi na kututukana sana, sasa kiko wapi Aprili 26 hiyo hapo na
Katiba haijapatikana na kusema itapatikana mwaka huu na kutumika kwenye
Uchaguzi Mkuu mwakani ni ndoto za mchana," alieleza Dk. Slaa.
Dk. Slaa
alisema tukio hilo liwe fundisho kwa Serikali, wawe wakweli, wanyoofu na
wafahamu kuwa nje ya Serikali kuna watu makini na wanaojua vilivyo
mchakato wa Katiba.
Alisema
ana taarifa za Bunge Maalumu kuahirishwa Mei 9, 2014 ili kupisha Bunge
la Bajeti. Hivyo mategemeo ya Katiba Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao,
yanatia shaka.
"Kwa
akili ya kawaida tu isiyohitaji elimu ya chuo chochote, kutumia Katiba
Mpya kwenye Uchaguzi Mkuu ujao ni jambo lisilowezekana kwa hiyo waache
kutuletea matumaini yasiyokuwapo, sisi siyo watoto wadogo," alieleza Dk.
Slaa.
Kauli ya LHRC
Mkurugenzi
wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba,
alisema siyo tu Serikali imeshindwa kutimiza ahadi ya muda
iliyojiwekea, bali hata mchakato wenyewe haueleweki.
Dk.
Bisimba alisema kwa hali ilivyo, hawana hakika ya kupata Katiba na
ikipatikana haitakidhi matakwa ya wananchi, kwa kuwa wanataka Katiba ya
watu siyo ya kundi moja la watu.
"Mambo ya
nchi hii tunayafahamu, inaweza ikapatikana kwa nguvu lakini wajue
wananchi wataikataa na hata ikilazimishwa, haitakidhi mahitaji, itaweza
kuathiri ustawi wa taifa," alieleza Dk. Bisimba.
Alisema
hilo waliliona mapema, wakataka kila hatua ya mchakato ipewe muda wa
kutosha kabla ya hatua nyingine, ili wananchi waelimishwe lakini
hawakusikilizwa.
Alisema
kuwa katika mazingira hayohayo, Tume ya Mabadiliko ya Katiba ilifanya
kazi kubwa hadi kufanikisha maoni ya wananchi kupatikana na kutengeneza
Rasimu ya kwanza na ya pili iliyowasilishwa bungeni Machi 18, 2014,
lakini kwa jinsi Bunge Maalumu linavyoendeshwa, kuna kila dalili kwamba
kazi hiyo itaharibiwa.
"Wakichezea
Rasimu wajue wanachezea maoni ya wananchi, wanaoweza kuyakataa kupitia
kura ya maoni na hivyo kusababishia taifa hasara isiyomithilika,"
alieleza Dk. Bisimba.
Dk.
Bisimba alisema mchakato huo umegharimu taifa fedha nyingi, muda mwingi,
nguvu, akili, afya na hata uhai wa watu, hautakiwi kufanyiwa mzaha.
Alipotafutwa
Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Asha-Rose Migiro ili kuzungumzia suala
hilo jana hakupatikana, lakini Naibu Waziri wa wizara hiyo Angela
Kairuki, alisema kuwa kwa hali ilivyo ni dhahiri haiwezekani kupata
Katiba Mpya kwa muda huu tofauti na ilivyodhaniwa awali.
Hata
hivyo, Kairuki alisema hawezi kuzungumzia hatua iliyofikiwa katika
mchakato huo kwani mwenye mamlaka ya kuzungumzia ratiba ya Bunge Maalumu
la Katiba ni mwenyekiti wake, Samuel Sitta.
"Hata
hivyo tunachotakiwa kuzungumzia ni ubora wa kazi inayofanyika ili
kufikia lengo la kupata Katiba itakayoongoza nchi kwa miaka 50 ijayo,"
alisema Kairuki.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment