KAMATI za
Bunge Maalumu la Katiba zimeanza kuwasilisha bungeni maoni yake, kuhusu
mijadala ya sura ya kwanza na ya sita ya rasimu ya Katiba mpya, huku
wengi wakikataa muundo wa serikali tatu, kwa kusema utaibua hisia za
ubaguzi kwa wananchi wa taifa moja.
Miongoni
mwa kamati zilizowasilisha maoni jana bungeni ni Kamati Namba Tano,
ambayo Makamu Mwenyekiti wake, Assumpter Mshama, alisema muundo wa
serikali tatu ukipita, utaibua hisia hizo, ambazo hazipati nafasi katika
mfumo uliopo wa serikali mbili.
Assumpter
alimnukuu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aliyesema; “Nje ya
Muungano, hakuna Wazanzibari, kuna wao Wapemba na sisi Waunguja…dhambi
hii haitaacha kuitafuna Tanganyika ambayo ina makabila mengi.”
Mbali na
ubaguzi, walio wengi katika kamati hiyo walielezea hatari nyingine ya
muundo unaopendekezwa, utajenga mazingira ya kulisambaratisha Taifa.
“Sura ya
17 ya rasimu inathibitisha kitakachotokea endapo muundo unaopendekezwa
utakubaliwa. Mojawapo ya mambo yanayozungumziwa na sura hii ni masuala
ya kugawana rasilimali, kugawana watumishi wa umma, madeni na mambo
mengine.
“Mambo
haya badala ya kuwaleta karibu, inawatenganisha wananchi wa pande mbili
za Muungano…kwa mnasaba huu, muundo wa serikali mbili ndio ulioafikiwa
na wajumbe wengi kuwa unalifaa taifa letu kwa kuzingatia maslahi ya
kiuchumi, kijamii, kisiasa na kiusalama ya wananchi wa pande mbili,”
alisema.
Kuhusu
kero za Muungano zinazodaiwa kudumu kwa miaka 50 na kuwa kichocheo cha
kupendekezwa kwa serikali tatu, walio wengi katika Kamati hiyo walisema
changamoto hizo wanazitambua na jitihada zinafanyika kuzikabili.
“Walio
wengi wanaamini kuwa muundo wa serikali tatu hautakuwa suluhisho badala
yake utaibua changamoto nyingine nyingi. Mchakato huu ni fursa kubwa na
ya pekee kuzishughulikia changamoto hizi kwa mapana yake. “Mapendekezo
yaliyotolewa na walio wengi, yanalenga kuzipa jitihada hizi kinga za
kikatiba na kisheria ili ufumbuzi wake uwe endelevu,” alisema Assumpter.
Kutokana
na hoja hizo, Assumpter alisema walio wengi wanapendekeza katika Sura ya
Sita, Ibara ya 60 (1), irekebishwe na kusomeka “Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania itakuwa na muundo wa serikali mbili ambazo ni: “Serikali ya
Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania; na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Wajumbe
wengi pia katika Kamati hiyo, wamependekeza kuwepo kwa viongozi wakuu
wenye mamlaka ya utendaji katika Jamuhuri ya Muungano waliotajwa katika
Ibara ndogo ya (3), ambao watawajibika kila mmoja wao katika kutekeleza
madaraka waliyopewa kuhakikisha wanalinda, wanaimarisha na kudumisha
Muungano.
Viongozi
wakuu hao ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano, Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya
Muungano, Rais wa Zanzibar na Waziri Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Tanganyika kufufuliwa?
Kamati
hiyo Namba Tano, walio wengi wamependekeza kabla ya Rasimu ya Katiba
kupitisha muundo wa serikali tatu, ni lazima nchi inayoitwa Tanganyika
iwepo kwanza na kupewa mamlaka yake, kisha iamue inataka Muungano wa
aina gani.
Makamu
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mshama alisema rasimu ya Katiba inapendekeza
muundo wa serikali tatu zitakazotokana na Muungano wa nchi mbili, lakini
hivi sasa Tanganyika inayopendekezwa kama nchi mshirika haipo.
Alifafanua
Tanganyika haipo kwa kuwa mamlaka, uendeshaji na masuala yake yote
yalikwishakabidhiwa kikatiba na kisheria katika nchi inayoitwa Jamuhuri
ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1964.
“Hivyo
kama kuna shirikisho linapendekezwa basi ni lazima kwanza nchi hiyo
inayoitwa Tanganyika iwepo, iwe na Katiba yake na vyombo vyote vya
utawala ili iweze kuwa na mamlaka ya kuamua kama inataka Muungano.
“Muungano wenyewe wa aina gani na kama ni shirikisho, basi Tanganyika
iamue kwa msingi wa kuyakubali masharti ya shirikisho linalopendekezwa.
Hilo likifanyika Hati ya Makubaliano iliyopo na ambayo ndiyo inayotajwa
na Rasimu ya Katiba, itabaki kuwa waraka wa kihistoria,” alisema
Assumpter.
Kamati Namba 2
Mwenyekiti
wa Kamati Namba Mbili, Dk Shamsi Vuai Nahodha, alisema katika ibara ya
kwanza inayohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe walikuwa na
mjadala mkali kuhusu maana ya maneno Muungano na Shirikisho, ambayo
ufafanuzi wake ulitolewa.
Alisema
Muungano ni makubaliano ya zaidi ya nchi moja, kuunda dola moja yenye
nguvu, ambapo majukumu ya msingi ya nchi hizo yanakabidhiwa kwenye
Serikali ya Muungano.
Alisisitiza
Muungano wa Tanzania ni makubaliano kati ya Tanganyika na Zanzibar,
ambapo Tanganyika ilikabidhi madaraka yake yote kwa serikali ya Muungano
na Zanzibar ilikasimu baadhi ya madaraka yake kwa serikali ya Muungano.
Kwa
upande wa Shirikisho, Dk Nahodha alisema Shirikisho ni makubaliano ya
nchi mbili au zaidi, zinazounda Serikali moja chini ya kiongozi mmoja,
lakini kwa muktadha wa rasimu ya Katiba iliyopo, Shirikisho
linalozungumziwa litakuwa na serikali tatu na Marais watatu.
Alisema
baada ya ufafanuzi wa kina, wajumbe walifanya uamuzi katika Ibara ya
Kwanza wajumbe wengi ambao hawakufikia theluthi mbili walipendekeza neno
Shirikisho lifutwe kwa sababu tatu; Kwanza, hati ya makubaliano ya
Muungano inazungumzia kuwepo kwa serikali mbili yaani serikali ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
“Hata
Rasimu ya Katiba katika Ibara 1 (3) inatambua hati ya Muungano kama
msingi na mwendelezo wa makubaliano hayo,” alisema Nahodha.
Alisema
sababu ya pili ni Hati hiyo ya Muungano mpaka sasa haijafutwa na wala
haijabadilishwa na tatu, Shirikisho la Serikali tatu linalopendekezwa
katika rasimu, litakuwa dhaifu kiasi cha kushindwa kudhibiti ulinzi wa
eneo la Bahari ya Hindi lenye rasilimali nyingi ambazo mataifa makubwa
wanaziwania.
“Udhaifu
huu utayapa mwanya mataifa hayo kuzirubuni nchi washirika zisichangie
gharama za kuendesha serikali ya shirikisho hasa tukizingatia kuwa
serikali ya Shirikisho haina vyanzo vya uhakika vya mapato na endapo
jambo hili litatokea Shirikisho litadhoofika na hatimaye kuvunjika.”
Msingi wa Muungano
Akizungumzia
Sura ya Sita, inayozungumzia muundo wa Jamhuri ya Muungano alisema
wajumbe walijadili na kuchambua na kukubaliana kwamba Muundo wa Serikali
Mbili, kama ulivyoanishwa katika hati ya Muungano, ndio msingi mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema
hata hivyo baada ya kupiga kura kwa ajili ya kupata uamuzi, theluthi
mbili ya upande wa Tanzania Bara haikupatikana. Alisema ingawa theluthi
mbili haikupatikana, wajumbe wengi kutoka pande zote, walipendekeza
kwamba Ibara hiyo ifanyiwe marekebisho.
Alisema
kutokana na marekebisho hayo; Ibara ya 60 (1), itasomeka; “Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania itakuwa na muundo wa serikali mbili ambazo ni (a)
Serikali ya Jamhuri ya Muungano na (b) Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar.
Ibara ya
60 (2) sasa itasomeka kwamba “Shughuli za Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania zitatekelezwa na kusimamiwa na (a) vyombo viwili vyenye mamlaka
ya utendaji, (b) vyombo viwili vyenye mamlaka ya kutunga sheria na (c)
vyombo viwili vyenye mamlaka ya utoaji haki. Hoja kinzani Akisoma maoni
kinzani, Dk Nahodha alisema katika mjadala huo baadhi ya wajumbe
walikuwa na mtazamo hasi hususani neno Shirikisho lilipotumika.
Kwa
mujibu wa Nahodha, baadhi walisema wajumbe walio wengi walidhamiria kwa
kiwango kikubwa kuleta marekebisho ama nakala ya rasimu yao ya siri ili
kubadili kiini cha rasimu rasmi, ambayo kimsingi ni maoni na mapendekezo
ya wananchi kama yalivyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba,
iliyoundwa na Rais.
No comments:
Post a Comment