WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Sunday, April 13, 2014

Wakaidi wa mabondeni wasipewe misaada

Mvua ndiyo hizo zinanyesha na tunashuhudia athari zake katika maeneo kadha wa kadha nchini.
Wapo wanaozifurahia kwa ajili ya chakula, lakini wapo wanaozichukia hata kufikia kukufuru Mungu kutokana tu wao waliamua kujenga bondeni lakini wapo ambao zimewaletea athari za kiuchumi kwa maana ya kuharibika kwa miundombinu.

Mvua hizi ni dhahiri athari zake zimemgusa kila mtu, kilio kilichopo si cha wa bondeni tu, bali hata wale wa mlimani.

Pamoja na kwamba athari zake zimegusa watu wengi ikiwamo serikali yenyewe, lakini kilio kikubwa kipo kwa watu wa bondeni.

Zipo taarifa hasa katika mkoa wa Dar es Salaam kwamba watu wanane wamekwisha poteza maisha.

Mbali na vifo hivyo, ni dhahiri mvua hizo zimeacha maumivu mengi ikiwa ni pamoja na watu kupata majeraha, uharibifu wa mali lakini wengi kukosa makazi kutokana na mvua hizo kusomba nyumba zao.

Ipo miundombinu iliyoharibika, kwa mfano mkoa wa Dar es Salaam tayari daraja la mto Mzinga linalounganisha Chanika na Mbagala limekatika.

Daraja lingine kubwa ni lile la mto Mpiji ambalo ni kiunganishi kikubwa cha Bagamoyo na Dar es Salaam nalo limekatika.

Athari hizi ni sehemu ndogo tu za mvua hizo zinazoendelea kunyesha karibu nchi nzima.
Pamoja na Mamlaka ya Hali ya Hewa Nchini kutoa hadhari ya mara kwa mara, wapo baadhi ya watu wasiozingatia ushauri wa mamlaka hiyo.

Zipo jitihada zilizofanywa na serikali katika kuhakikisha raia wake hawapati athari hasa zinazosababishwa na mvua, lakini baadhi ya raia wamekuwa wakaidi.

Kwa mfano, Dar es Salaam eneo la Jangwani ambalo ni maarufu kwa wakazi wake kupata mafuriko hata mvua zinapokuwa si nyingi, serikali ilifanya utaratibu na kuwatafutia viwanja katika eneo la Mabwepande, lakini wakazi hao kwa ukaidi tu, wamesusa kuishi huko.

Kibaya zaidi wapo wanaodaiwa kuuza viwanja vyao na kurudi Jangwani, na leo hii ndiyo wanailalamikia serikali.

Katika hali isiyo ya kawaida, mkazi wa jangwani anatoka kifua mbele akiitupia lawama serikali, ili hali watu tunafahamu walihamishwa lakini baadhi eti hawahami mpaka wapewi fidia!

Swali la kujiuliza, unapewa fidia ya nini? Hata kuokoa maisha yako unastahili kulipwa fidia? Wajiulize ni gharama kiasi gani, achilia mbali kupoteza ndugu zao, wanazozipata wakati huu wa mvua?

Katika safu hii nilishatoa mapendekezo kuwa, wakazi wote wanaoishi bondeni hasa Jangwani ambao tunafahamu fika walipewa maeneo lakini wakayakataa, ikiwezekana eneo hilo la Jangwani likabidhiwe liwe milki ya jeshi.

Likiwa chini ya uangalizi wa Jeshi tena la Ulinzi (JWTZ) tutakuwa tumewatendea haki ndugu zetu hawa na baadaye watatushukuru kwa kufanikiwa kuwaondoa katika eneo hatarishi.

Kuna usemi ulikuwa unapendelewa sana kutumiwa na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuf Makamba unaosema “gombana na ndugu yako katika jambo mtakalokuja kupatana.”

Ni wakati wa kutowaonea huruma wakazi wa bondeni, ni bora tukagombana nao sasa ili baadaye tujekupatana kuliko tukashuhudia kila mara wakipoteza mali, ndugu zao na wengine kuachiwa majeraha ya kudumu.

Pamoja na kwamba wakazi hao serikali imewaandalia utaratibu mzuri wa sehemu ya kuishi, lakini kutokana na ukaidi wao, wanapopata madhara Jumuiya za Kimataifa hazitatuelewa na badala yake Tanzania itanyooshewa vidole kwa kutojali watu wake.

Kwa upande wa serikali, ni muda sasa wa kujipanga kurejesha miundombinu itakayoharibika, ni dhahiri kuwa fedha nyingi zitatumika. Hakuna ujanja, majanga yote hutokea kwa dharura, hivyo serikali ijiandae kwa udharura huo.

Si kwa upande wa miundombinu tu, bali serikali ijiandae pia kusaidia wakulima ambao mazao yao yatasombwa na mvua na wao kubaki kama yatima.

Kampuni na watu binafsi wenye uwezo zijitokeze katika kusaidia serikali kuwanusuru waathirika wa mvua hizi, lakini si watu wa Jangwani bali wale ambao makazi yao si hatarishi bali mvua imewafuata.

Wakati hayo yakiendelea kama ilivyo desturi ya Watanzania, unapoona jirani yako ameathiriwa na mvua hizi, mhifadhi.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment