Pwani. Safari ya miaka 74
duniani ya nguli wa muziki wa dansi nchini, Muhidin Mwalimu Gurumo
ilifikia tamati jana baada ya kuzikwa kijijini kwake Masaki Wilaya ya
Kisarawe mkoani Pwani.
Gurumo alifikwa na mauti Aprili 14, mwaka huu
katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) alikokuwa amelazwa kwa
matibabu ya ugonjwa wa moyo, maradhi yaliyomsumbua kwa kipindi kirefu.
Safari ya mwisho ya nguli huyo ilianzia jana
asubuhi nyumbani kwake Tabata External kwa waombolezaji wakiongozwa na
Makamu wa Rais, Dk Mohamed Gharib Bilal kutoa heshima za mwisho na
salamu kutoka makundi mbalimbali kutolewa.
Msafara wa magari zaidi ya 20 ulianza saa 05:15
kwenda Masaki na ulifika saa 7:10 nyumbani kwake. Mwili wa Gurumo
ulipelekwa msikitini kwa ajili ya sala kisha saa 07:40 mazishi
yalifanyika katika makaburi ya Masaki mkabala na ilipo nyumba yake.
Akimzungumzia nguli huyo wa muziki, mtangazaji mkongwe ndani na nje ya nchi, Tido Mhando alisema tungo za nyimbo alizoimba Gurumo zilikuwa zenye kuelimisha na kuiburudisha jamii.
Mhando, ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL), alisema Gurumo alitumia tungo zake kuhamasisha jamii na kupigania uhuru wa Waafrika.
“Jana (juzi) kuna redio ilikuwa ikipiga nyimbo
zake zaidi ya 20. Hakika nyimbo zote zilikuwa nzuri kutokana na umahiri
wake wa utunzi vitu, ambavyo vijana wetu wanashindwa kufanya hivyo leo
hii,” alisema Mhando.
Aliongeza: “Vijana wetu wanatakiwa kuiga kutokana na ustadi wa Gurumo wa kuimba, ustadi wa lugha ya Kiswahili, hivyo waige mfano wake.”
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment