Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba,
Zitto Kabwe amesema kuandikwa kwa Katiba isiyokubaliwa na pande zote
kutasababisha gharama kubwa kuliko zile zinazotajwa za serikali tatu.
Akichangia hoja kwenye Bunge hilo
jana, Zitto alisema kuna kila sababu ya kukaa na kukubaliana ili kupata
Katiba itakayokubalika pande zote.
"Muundo wa Muungano una hatari ya
kuvunjika iwapo hakuna matakwa ya dhati ya watu kuungana... Maneno ya
kusema Serikali tatu zitavunja Muungano ni ya siasa na hayana msingi wa
kisayansi. Urusi ilivunjika sababu haikuwa na demokrasia na siyo sababu
ya idadi ya Serikali," alisema.
Zitto ambaye pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), alisema hofu ya gharama
inayotajwa katika uendeshaji wa muundo wa serikali tatu haina msingi
wowote kwa kuwa hakuna ushahidi wa kitaalamu unaothibitisha gharama hizo
.
"Nimesikia watu wanasema eti
tutalazimika kujenga ikulu mpya, nani kasema lazima tuwe na marais
watatu? Tunaweza kuwa na rais mmoja kwenye nchi na wakuu wa nchi
washirika wawili... Ni jambo la makubaliano tu," alisema.
Alisema bajeti ya mwaka huu ni Sh18
trilioni, kati ya hizo Sh5.3 trilioni ndizo zinazohudumia wizara za
Muungano, lakini serikali ina uwezo wa kukusanya kodi zaidi ya Sh10
trilioni pamoja na mapato mengine.
"Kuna jumla ya Sh2.3 trilioni
hatuzikusanyi kila mwaka kutoka kwenye kampuni kubwa, kwa uwezo wetu wa
pato la ndani asilimia 17 tunao uwezo wa kuendesha serikali ya muundo wa
idadi yoyote.
"Hofu ya Serikali ya Muungano kutokuwa
na fedha ni sababu halisi, ni kweli kwamba ushuru wa bidhaa pekee yake
hauwezi kutuendeshea serikali. Sasa nini kazi yetu, tunaingia hapa ili
kuboresha hayo maeneo, kama hatuwezi tumekuja kufanya nini hapa?"
alihoji.
Jussa akomaa
Mjumbe wa Bunge hilo, Ismail Jussa
jana alisisitiza kwamba Wazanzibari wengi hawapo tayari kuendelea na
mfumo wa serikali mbili kwa sababu unawatesa na kuwadhalilisha.
Jussa ambaye ni mjumbe wa Baraza la
Wawakilishi Zanzibar kupitia CUF, alisema haoni haya kuzungumzia suala
hilo kwa niaba ya Wazanzibari.
"Hoja nyingi zimetoka (kuhusu
Muungano), lakini naendelea kuzungumza kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar
na katika hili sioni haya kwa sababu naamini kwamba wanakisimamia kile
ambacho sisi tunasimamia nacho ni Zanzibar yenye mamlaka kamili,"
alisema Jussa.
Alisema amekuwa akijiuliza kwa nini
serikali mbili zinang'ang'aniwa na CCM licha ya kunung'unikiwa na baadhi
ya wanachama wake kwa miaka 50?
"Hapa wala maneno hayo hayajasemwa na
CUF, wala na mpinzani. Hapa ninayo Ripoti ya Amina Salum Ali ya Novemba
1992 ikiorodhesha matatizo lukuki ya mfumo wa serikali mbili na wajumbe
wake hawa wote walikuwa ni kutoka CCM, mwenyekiti wake Amina Salum Ali,
katibu wake Ali Juma Shamhuna ndiyo walioleta ripoti hii," alisema Jussa
huku akionyesha ripoti hiyo.
Kutokana na hali hiyo, alisema anaona
ni kuwadanganya Wazanzibari kwamba serikali mbili zitatatua matatizo
yao, hivyo kuwafanya wajiulize mbona hazikuyatatua kwa miaka 50
iliyopita.(E.L)
SOURCE: MJENGWA BLOG
No comments:
Post a Comment