Na Baraka Mpenja, Dar Es salaam
0712461976
AKIWAANZISHA
washambuliaji wake watatu, Gaudence Mwaikimba, Kipre Herman Tchetche na
John Rapahel Raphael Bocco 'Adebayor', kocha wa Azam fc Mcameroon,
Joseph Marius Omog amefanikiwa kuongeza pointi tatu muhimu baada ya
kuwafumua maafande wa Ruvu Shooting mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu
soka Tanzania bara, kwenye uwanja wa Mabatini , Mlandizi mkoani Pwani.
Lengo la
Omog lilikuwa ni kufunga mabao mengi katika mchezo huo ili kuendelea
kujiweka mazingira mazuri ya kuiongoza Azam fc kuandika historia mpya ya
kutwaa ubingwa wao wa kwanza tangu wapande ligi kuu mwaka 2008/2009.
Mipango
yake ilianza kuzaa matunda dakika ya 8 ya mcheza ambapo mshambuliaji
wake ambaye mara nyingi hukalia benchi, Gaudence Mwaikimba kufunga bao
la kuongoza.(P.T)
Azam fc
walionekana kuwa na uchu wa kupata mabao zaidi, na katika dakika ya 37
kipindi cha kwanza, winga machachari, Himid Mau Mkami alitia kambani bao
la pili kufuatia krosi nzuri iliyochongwa na beki wa kulia, Erasto
Edward Nyoni.
Dakika 45 za kipindi cha kwanza zilimalizika kwa Azam fc kuwa kifua mbele kwa mabao 2-0.
Kipindi
cha pili kilipoanza, Azam fc walionekana kuendelea kuwepo mchezoni
ambapo dakika ya kwanza tu, Kipre Herman Tchetche aliandika bao la tatu
na kuwanyanyua mashabiki waliofurika uwanjani.
Kwa
matokeo hayo Azam fc wamezidi kujikita zaidi kileleni kwa kufikisha
pointi 56, pointi nne mbele ya mabingwa watetezi Yanga SC katika nafasi
ya pili.
Yanga walikuwa wanaufuatilia mchezo huo kwa makini ili kujiridhisha kama wataweza kutetea ubingwa wao msimu huu.
Jana
wanajangwani hawa walishinda mabao 2-1 dhidi ya Kagera Sugar na
kuwasogelea Azam fc kileleni, lakini leo mambo yamezidi kuwa magumu
zaidi kwao kutokana na matokeo ya Mabatini.
Ili
kutetea ubingwa wao, Yanga wanahitaji kushinda mechi mbili walizobakiza
dhidi ya JKT Oljoro na Simba sc, wakati huo huo wakiiombea mabaya Azam
fc ipoteze michezo yote miwili.
Wakati Yanga wakiwa katika presha kubwa, Azam fc wao wanahitaji pointi tatu tu kuwavua ubingwa Yanga.
Wakishinda
mechi moja kati ya mbili walizobakiza, wana Lambalamba watafikisha
pointi 59 ambazo Yanga hawataweza kufikisha hata kama watashinda mechi
zote walizosaliwa nazo kwa mabao 50.
Yanga
wakishinda mechi mbili zijazo watafikisha pointi 58 kibindoni ambazo
Azam fc wataweza kuzivuka kama watashinda mechi moja tu kati ya mbili
walizonazo mkononi.
Mechi ijayo, Azam fc watashuka dimbani dhidi ya Mbeya City katika uwanja wa Sokoine jijini Mbeya.
Hii
itakuwa mechi muhimu sana kwa Azam fc, lakini watahitaji kutumia nguvu
kubwa kuwafunga wagonga nyundo hawa wa Mbeya kwasababu ya rekodi yao
nzuri ya kutofungwa katika uwanja huo.
Mbeya City mpaka sasa wapo nafasi ya tatu katika msimamo wakiwa na pointi 46 baada ya kucheza mechi 24.
City
wameshapoteza nafasi mbili za juu kwasababu wakishinda mechi mbili
zilizobaki watafikisha pointi 52 ambazo zimeshafikiwa na Yanga, huku
wakiwa na michezo miwili mkononi.
Hata kama
Yanga watapoteza mechi mbili zijazo, kama Mbeya City watahitaji kuwa wa
pili watahitaji kushinda mechi mbili zilizobaki kwa ida kubwa mno ya
mabao.
Ukiangalia
wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, Yanga wametia kambani mabao
mengi mno zaidi ya Mbeya City. Hivyo bado nafasi ya pili kwao ni ngumu
kuipata.
Hata hivyo kushika nafasi ya tatu si haba kwao kwasababu ni msimu wao wa kwanza.
Wakati
Azam fc wakijiandaa kwenda Mbeya, tayari zipo tuhumu kwa wenyeji wao
Mbeya City kuwa wamehongwa na wana Lambalamba ili kucheza chini ya
kiwango.
Madai ya kuuzwa kwa mechi hiyo yamesambazwa kuhusu mambo matatu;
ambayo ni Timu ya Mbeya City kununuliwa basi na Klabu ya Azam, Kocha wao Juma Mwambusi amejengewa nyumba maeneo ya Chamazi, na wachezaji wao wamepewa fedha ili waweze kucheza chini ya kiwango dhidi ya Azam.
ambayo ni Timu ya Mbeya City kununuliwa basi na Klabu ya Azam, Kocha wao Juma Mwambusi amejengewa nyumba maeneo ya Chamazi, na wachezaji wao wamepewa fedha ili waweze kucheza chini ya kiwango dhidi ya Azam.
Hata
hivyo uongozi wa Mbeya City umekanusha tuhuma hizo na kusema watu
wanaosambaza taarifa hizo hawana malengo mazuri na klabu yao, zaidi
wanawachafua kwa mashabiki wao.
Bingwa atakayepatikana msimu huu atakuwa ni halali kutokana na ushindani mkubwa uliooneshwa na timu za juu.
Azam fc,
Yanga na Mbeya City toka mwanzo wa mzunguko wa pili zimefukuziana mno na
hatimaye sasa Mbeya City wamejitoa na kuwaacha Yanga na Azam fc
wakiendelea kuchuana.
Sasa Yanga na Azam fc ni kutegeana tu, atakayepoteza mechi atamnufaisha mwenzake.
Lakini
Yanga ndio watumwa kwa Azam fc kwasababu wanahitaji kutetea ubingwa wao,
wakati huo huo wakihenyeka kutaka kusawazisha pengo la pointi nne dhidi
ya Azam fc.
Ligi hiyo
itaingia raundi ya 25 Aprili 12 na 13 mwaka huu ambapo timu zote 14
zitakuwa viwanjani. Aprili 12 mwaka huu itakuwa Mtibwa Sugar vs Ruvu
Shooting (Manungu, Morogoro), Coastal Union vs JKT Ruvu (Mkwakwani,
Tanga), na Tanzania Prisons vs Rhino Rangers (Sokoine, Mbeya).
Aprili 13
mwaka huu ni Mgambo Shooting vs Kagera Sugar (Mkwakwani, Tanga), Simba
vs Ashanti United (Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam), Mbeya City vs Azam
(Sokoine, Mbeya) na Oljoro vs Yanga (Sheikh Kaluta Amri Abeid, Arusha).
Chanzo:www.shaffihdauda.com
No comments:
Post a Comment