Kanuni ya 37 (1), inasomeka: “… ili ibara au
Rasimu iweze kupitishwa itahitaji kuungwa mkono na wingi wa theluthi
mbili ya wajumbe kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili toka Zanzibar”.
Taarifa zisizo rasmi zinasema ili kuwezesha
kupatikana kwa theluthi mbili kutoka upande wa Tanzania Visiwani CCM
walikuwa wakihitaji kupata kura 16 ikilinganishwa na idadi yao ya sasa
ya wanaounga mkono.
Kamati ya Uongozi
Harakati zinazofanywa na Sitta zimekuja saa chache
tangu kumalizika kwa kikao cha Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalumu,
ambacho habari zinasema kilimwelekeza kiongozi huyo kufanya jitihada za
kutatua mgogoro uliopo.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis
Hamad alisema kikao cha Kamati ya Uongozi hakikufikia uamuzi kuhusiana
na wajumbe wanaounda Ukawa kutoka bungeni kwa sababu hawajapata taarifa
ya nini kilichowafanya waondoke.
“Hakuna cha kushika hapa, hatukujua kwa nini
walitoka bungeni lakini Mwenyekiti (Sitta) alikuwa akiwatafuta ili kujua
sababu za kutoka kwao bungeni,” alisema Hamad na kuongeza: “Mwenyekiti
anawatafuta na tulikubaliana wakipatikana atatuita ili tuzungumze,”
alisema Hamad.
Hamad alimnukuu Sitta kuwa milango iko wazi kwa
Ukawa kwa mazungumzo. Pia alisema Waziri Mkuu, Mizengo Pinda yuko tayari
kuzungumza nao ili kufikia mwafaka kuhusiana na tatizo ambalo
limewafanya kutoka bungeni.
Mmoja wa wajumbe wa kikao hicho aliliambia gazeti
hili kuwa: “Kimsingi tulikubaliana wote katika kikao kwamba bila wenzetu
hatuwezi kupata Katiba Mpya, kwa hiyo tulimwomba mwenyekiti (Sitta)
awatafute viongozi wa Ukawa ili afahamu msimamo na mwelekeo wao na
ikiwezekana waanze mazungumzo.”
Mjumbe huyo aliongeza: “Tulishauri pia kwamba
Mwenyekiti awafahamishe wakubwa walioko serikalini kuona jinsi gani
wanaweza kuwatafuta wenzao ili watafute mwafaka, maana hali tuliyofikia
ni mbaya.”
Alisema ilishauriwa kwamba zitafutwe njia za
kumhusisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa
Zanzibar, Seif Sharif Hamad kama hatua ya kushawishi upande wa Ukawa
kulegeza msimamo wao.
Mjumbe mwingine alisema katika kikao hicho
yalitolewa mapendekezo kwamba Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ifanyiwe
marekebisho ili kuruhusu kufanyika kuwa kura ya maoni kwa sura mbili; ya
kwanza na ya sita za Rasimu ya Katiba, lakini wazo hilo lilipingwa.
“Hilo wazo lilitolewa sawa, lakini lilionekana
kama halitafaa kwa sababu kimsingi hata kura zikipigwa baina ya serikali
mbili na tatu, matokeo ya Zanzibar yanafahamika, kwa hiyo tuliona jambo
la msingi ni kufanyika kwa mazungumzo,” alifafanua mjumbe huyo.
Alisema kikao hicho hakikuwa na hitimisho kuhusu suala hilo
kutokana na wajumbe wa kikoa hicho ambao ni wanachama wa Ukawa akiwamo
Mbowe kukisusia.
Mazungumzo Zanzibar
Habari zaidi ambazo zililifikia gazeti hili
zinasema kumekuwa na harakati zinazofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar kutaka mazunguzo na CUF.
Mmoja wa viongozi wa CUF ambaye pia ni Mjumbe wa
Bunge la Katiba, Ismail Jussa alisema awali mazungumzo ya kutaka
Zanzibar kuwa na msimamo mmoja yalianzia kabla ya wajumbe kufika
bungeni.
“Sisi Chama cha CUF tulitaka kuwapo na msimamo
mmoja mara kadhaa kabla ya kuja bungeni lakini Balozi Seif Alli Idd
(Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar), hakuliafiki jambo hili,” alisema.
Alisema Jumamosi iliyopita Balozi Idd aliwaita
yeye na Waziri wa Katiba na Sheria, Abubakar Khamis Bakary na Waziri wa
Viwanda, Biashara na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui ili kutaka mazungumzo
yafanyike.
“Alituambia kuwa kuna Wawakilishi wa upande wa CCM
walimfuata na kumwomba akutane nasi ili tufanye maridhiano kupata sauti
moja kutoka Zanzibar,” alisema.
Alisema lengo la mwito huo ni kuwashawishi ili kupata Katiba yenye muundo wa serikali mbili ambao utatatua kero mbalimbali.
Alisema walimshauri Balozi Idd kufanya mazungumzo
na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein ili akutane na Maalim Seif
kufanya maridhiano hayo. “Sisi wakishafanya maridhaino yatashuka chini
na sisi tutayapokea na kuyafanyia kazi,” alisema.
Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili kwa simu
jana, Balozi Iddi alisema hakuna mazungumzo yoyote ambayo
yamekwishaanzishwa baina yao na CUF.
“Hili siyo suala la Serikali ya Umoja wa Kitaifa
kwa sababu wao waliondoka katika Bunge wenyewe na uamuzi wa kurejea ni
wa kwao wenyewe,” alisema Balozi Iddi.
Msimamo wa CUF
source mwananchi:
Jussa alisema msimamo wao ni serikali tatu ambazo zilipendekezwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, kwa sababu hawaoni ni vipi mfumo wa
serikali mbili utaondoa kero ya Tanganyika kuvaa koti la muungano.
“Kwa hatua hii tuliyofikia amechelewa kufanya maridhiano ambayo tuliyaomba tangu awali kabla ya kuja huku,” alisema Jussa.
Hata hivyo, alisema hawataweza kufikia maridhiano
bila kushirikisha wenzao wa Tanzania Bara kwani wataua nguvu ya Umoja wa
Katiba ya Wananchi (Ukawa).
“Hatuwezi kufikia maridhiano bila kuwashirikisha
wenzetu wa Bara (Ukawa), maana huko kutakuwa ni kuvunja nguvu umoja
wetu,” alisema.
Alisema maridhiano ya kutaka Zanzibar kuwa na
kauli moja yalianza miaka mitatu iliyopita lakini yalikwamishwa na
viongozi wa juu wa CCM wa upande wa Zanzibar.
“Tatizo ni kwamba wenzetu hawana nia njema na maridhianao haya ya kutaka Zanzibar tuwe kitu komoja,” alisema Jussa.
Imeandikwa na Neville Meena, Daniel Mjema, Ibrahim Bakari, Sharon Sauwa, Edwin Mjwahuzi na Beatrice Moses
No comments:
Post a Comment