WAJUMBE
wa Bunge Maalum la Katiba wanaotoka Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
waliotoka bungeni juzi jioni wamepanga kufanya mkutano wa hadhara
Zanzibar kesho, kwa kile walichodai ni kuwaeleza wananchi ukweli wa
mambo yanayojiri katika Bunge linaloendelea hivi sasa.
Ukawa
wameamua kuchukua hatua hiyo, huku Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba,
Samuel Sitta akisema ofisi yake ipo tayari kwa mazungumzo na wajumbe
hao ikiwa ni njia ya kuwezesha mchakato wa kutunga Katiba kuendelea kwa
pamoja na kwa amani.
“ Mimi
nadhani sababu za kitendo chao walichokifanya jana (juzi) hazitoshi,
mlango wangu uko wazi, nimeongea na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na yeye
kama kiongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), mlango wake upo wazi kwa
mazungumzo,” alisema Sitta jana.(Martha Magessa)
Akizungumza
na wajumbe wa Ukawa kwenye ukumbi wa African Dream mjini hapa jana,
Mjumbe wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema wameamua kuchukua
hatua hiyo ili kuwaeleza ukweli wananchi juu ya mambo yanayoendelea hivi
sasa Dodoma.
“Tulitoka
jana bungeni kwa sababu hatukuona haja ya kuendelea kuwepo huku lugha
zinazotumika ni za matusi, ubaguzi, kejeli na pia Rasimu iliyokuwa
ikijadiliwa sio ile ya Tume iliyowasilishwa bungeni,” alisema Lipumba.
Kutokana
na hali hiyo, alisema wameamua kwenda Zanzibar kufanya mkutano na
wananchi na kuwaeleza hayo ikiwa ni pamoja na kuwaeleza kauli ya Waziri
wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Uratibu na Bunge, William Lukuvi aliyoitoa
hivi karibuni wakati alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe za kusimikwa
kwa Askofu Joseph wa Kanisa la Methodist mjini hapa.
Alisema
wajumbe wote wa Ukawa wasio na dharura watasafiri Jumamosi asubuhi
kwenda Zanzibar kushiriki mkutano huo na nia yao ni kutaka Bunge
lijadili rasimu ya Katiba mpya iliyowasilishwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba na sio rasimu ambayo haijawasilishwa na Tume.
Mwenyekiti
wa Ukawa, Freeman Mbowe alisema Kamati ya Uongozi ya Bunge Maalum
ilikutana jana ambapo yeye alipewa taarifa kuwa ni Kamati ya Uongozi
kuhusu Bunge la Bajeti, lakini alipofika ndani alikuta mjadala
unaoendelea ni kuhusu Bunge Maalum, aliondoka.
HABARILEO
No comments:
Post a Comment