Dodoma. Mjumbe wa Bunge la Katiba,
David Kafulila jana aligeuka shujaa bungeni na kubebwa juujuu na wajumbe
wenzake kutoka kundi la walio wachache baada ya 'kusambaratisha' hoja
za wajumbe wanaopinga Serikali tatu.
Kafulila ambaye pia ni Mbunge wa
Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), alifanya hivyo alipokuwa akifafanua hoja
kutoka kundi la walio wachache katika Kamati Namba Tano.
Miongoni mwa hoja ambazo alizijibu na
kushangiliwa na wajumbe, ni juu ya gharama za Serikali tatu, kuwa
zitavunja Muungano, kwamba Serikali ya Muungano itakosa mapato, hoja ya
kumuenzi Mwalimu Julius Nyerere na uhalali wa takwimu za Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Alisema hoja kuwa Serikali tatu ni
kuvunja Muungano si za kweli, akisema ni propaganda zilezile ambazo CCM
ilizitumia mwaka 1992 kutembea nchi nzima kupinga mfumo wa vyama vingi.
"Wakati ule CCM ilitembea nchi nzima
huku wakionyesha video kuwa vyama vya upinzani vitaleta vita, lakini leo
miaka 20 baada ya kukubali mfumo wa vyama vingi hakuna vita
vilivyoletwa na upinzani," alisema Kafulila. Alisema haiwezekani tume
zote ambazo zinaundwa na Serikali zipendekeze serikali tatu na kila
wakati serikali iliyopo madarakani ikatae.
"Hoja ya serikali tatu siyo hoja ya
Warioba, tume zote zilizowahi kuchunguza muundo ya Muungano zote
zilipendekeza serikali tatu," alisema na kuongeza: "Ofisi ya Rais
ilipendekeza serikali tatu, ofisi ya Waziri Mkuu ilipendekeza serikali
tatu, inatuwia vigumu ndani ya muda mfupi, vyombo hivi vibadilike na
kutaka serikali mbili."
Alisema wanaotaka serikali tatu
wanataka kwa namna ambayo inaimarisha Muungano, tofauti na maoni ya
walio wengi kuwa serikali ya Muungano itakuwa legelege kwa kuwa itakosa
nguvu za kiuchumi.
"Ni kweli inawezekana vyanzo vya
mapato vilivyopendekezwa havitoshi kuendesha Bunge, lakini ndiyo sababu
tupo hapa, haiwezekani ripoti ya Tume iwe imekamilika pande zote,"
alisema na kuongeza:
"Wamependekeza badala ya kutegemea
vyanzo vya washirika, tumependekeza kodi ya bandari ambayo ni karibu
Sh3.6 trilioni inaweza kuwa ni kodi ya Serikali ya Muungano. Kodi hiyo
pekee inatosha kuendesha wizara zote ambazo gharama yake si zaidi ya Sh3
trilioni."
"Kuna hoja hapa, haiwezekani kuwa
fedha za bandari zote ziwe zinachangia Muungano kwani ni fedha za
Tanganyika, lakini Muungano wowote ni lazima kukubali nchi kubwa
kuchangia zaidi."
Kafulila ambaye hata baada ya kumaliza
muda wake wajumbe walipiga kelele wakitaka aendelee, alisema kwa
Serikali ya Muungano kupata mapato hayo tu, itakuwa haina haja ya
kusubiri fedha za nchi washirika na pia itakuwa na uwezo wa kuchangia
fedha kwa nchi washirika.
"Haiwezekani Watanganyika wakubali
kubeba gharama kubwa ya serikali mbili badala ya gharama ndogo za
serikali tatu na hii ndiyo inawapa hofu Wazanzibari kudhani kuna kitu
kinachofichwa," alisema. Kuhusu hoja ya kutumia maneno ya Nyerere
kupinga Muungano wa serikali tatu, alisema Mwalimu hakuwa nabii,
alitazama mambo kwa wakati ule na alikuwa akibadilika kutokana na
wakati.
chanzo Mwananchi
No comments:
Post a Comment