Dar es Salaam. Rais Jakaya Kikwete ameendelea
kusisitiza kuwa Tume ya Jaji Joseph Warioba haina ushahidi kwamba
Watanzania wengi wanataka muundo wa Muungano wa serikali tatu.
Kauli hiyo aliitoa wiki hii jijini Dar es Salaam
kwenye mahojiano maalumu na Kituo cha Televisheni cha NTV kilichopo
chini ya Nation Media Group (NMG).
Baadhi ya vyombo vingine vya habari vilivyo chini
ya NMG ni gazeti hili la Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti kwa upande
wa Tanzania, Daily Monitor kwa upande wa Uganda na Daily Nation kwa
upande wa Kenya.
Rais Kikwete ambaye moja ya mambo atakayokumbukwa
kwenye uongozi wake ni kuasisi mchakato wa Katiba, alizungumzia hoja ya
serikali tatu akisema, hakuna ushahidi kwamba Watanzania wengi wanataka
muundo wa Muungano wa serikali tatu.
“Hakuna ushahidi kwamba watu wengi katika nchi hii
wanataka serikali tatu, hakuna ushahidi wa namna hiyo, hata tume
yenyewe haikubaini hicho. Kinachofanywa na vyombo vya habari ni kuandika
habari za wajumbe wa Bunge la Katiba wanaotaka serikali tatu, ndiyo
kwenye masilahi yao, wanapaza sauti za wale wanaotaka serikali tatu, hao
ndiyo sauti zao zinasikika. Lakini hawataki kupaza sauti za wale
wanaotaka serikali mbili,” alifafanua.
Hii ni mara ya pili kwa Rais Kikwete kuikosoa
ripoti ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph
Warioba. Mara ya kwanza aliikosoa wakati akizindua Bunge la Katiba Machi
21 mjini Dodoma.
Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa kipindi cha miaka 10, katika
mahojiano hayo alisema katika kuadhimisha miaka 50 ya Muungano, jambo
muhimu na kubwa ni kuendelea kuwapo kwa Muungano.
“Tunayo mifano ya nchi zilizojaribu kuungana, lakini zilishindwa, Senegal-Gambia, Ghana-Guinea, Misri na Libya.
“Muungano umeendelea kuwepo kwa nusu ya karne ni
mafanikio makubwa. Kumekuwepo na wakati mgumu na changamoto mbalimbali,
lakini tumeweza kukabiliana nazo na umeendelea kuwa imara zaidi. Siyo
kuendelea kuwepo tu pia umeendelea kuimarika na mchakato wa mabadiliko
ya Katiba utaimarisha zaidi Muungano na tutakuwa na Muungano imara baada
ya kupata Katiba Mpya,” alifafanua Rais Kikwete.
Akizungumza kwa kujiamini kutokana na uzoefu wake
wa muda mrefu ndani ya CCM na Serikali, Rais Kikwete alisema Muungano
ulikotoka ulikuwa imara na umeendelea kukua katika hali ya uimara wake.
“Kuna mambo ambayo tumefanya yamezidi kuimarisha Muungano na umeendelea kuwa na mafanikio makubwa.”
Alisema suala si kuendelea kwa muundo ulivyo sasa,
suala la msingi ni kujadili namna ya kutengeneza muundo wa Muungano,
kwamba upi ni bora.
Rais Kikwete: “Mimi ni mmoja wa wanaoamini kwamba muundo wa
serikali mbili ni bora zaidi kwetu. Siyo suala la kuendeleza hali
iliyopo, ni muhimu kubadilika kama kuna sauti zinazotaka kubadilika na
pia kama kuna hoja nzito ya kutaka mabadiliko, lakini sioni kama
Muungano wa Serikali tatu ni hoja nzito ya kufanya mabadiliko,
itasababisha matatizo mengine na mwisho kusababisha muungano kuvunjika.”
Rais Kikwete ambaye katika uzoefu wake wa kazi za
kisiasa amewahi kufanya kazi Zanzibar, alisema alipoingia madarakani
mwaka 2005 hoja kuu ilikuwa ni kutatua mzozo wa kisiasa uliokuwa
ukiendelea kwa muda mrefu kati ya vyama vya CUF na CCM visiwani humo.
Alisema: “Tumeweza kuutatua na sasa tuna Serikali
ya Umoja wa Kitaifa. Kabla ya hapo kulikuwa na matatizo mengi, wakati wa
uchaguzi mambo yanatulia, ukimalizika uchaguzi kunazuka matatizo ya
kisiasa, tukaamua kuvileta vyama hivi pamoja tukafanya mjadala wa kina
na uamuzi uliofikiwa ni kuwa na serikali ya umoja wa kitaifa, na sasa
Zanzibar kuna utulivu wa kisiasa.”
Rais Kikwete akizungumzia suala la Muungano
alisema wakati wa Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, aliunda
tume, Tume ya Shelukindo (iliongozwa na William Shelukindo) kuangalia
kero za Muungano na walikuja na kero 31.
Alisema alipoanza kazi mwaka 2006 kero za Muungano zilikuwa zimebaki 13, akashughulikia kero tisa, zimebaki kero nne tu.
Rais Kikwete alisema kimsingi uhuru wa vyombo vya
habari kwa Tanzania ni mpana na kwamba hata gazeti lililofungiwa ni moja
na mengine yalifungiwa kwa muda tu.
Alisisitiza kwamba habari za kuchochea majeshi
kufanya mapinduzi, habari za kuchochea vijana kuleta vurugu
hatazivumilia, na kwamba chombo cha habari kitakachojielekeza kwenye
habari za namna hiyo kitafungiwa.
“Wakiandika Rais Kikwete nchi imemshinda hainipi
tabu, kwa kuwa najua nchi haijanishinda,” alisema Rais Kikwete huku
akitoa mfano wa namna redio Mille Collines ya Rwanda ilivyochangia
mauaji ya halaiki nchini humo.
Rais Kikwete alitoa mfano mwingine wa namna vyombo
vya habari vilivyochangia uvunjaji wa amani ni mwandishi wa habari wa
Kenya ambaye amefunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kimataifa katika
Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), iliyopo The Hague nchini
Uholanzi.
Mwandishi wa habari aliyefunguliwa mashtaka ICC ni
mtangazaji wa Kituo cha Redio ya Kass FM, Joshua arap Sang. Rais
Kikwete huku akicheka alimuhoji mtangazaji wa NTV “Unataka habari kama
hizo tuzivumilie?”
Kuhusu rushwa, Rais Kikwete aliitaja idara ya
mahakama kuwa ni moja ya changamoto na wiki iliyopita alizungumza na
Jaji Mkuu kuona namna gani wanaweza kuboresha, kuongeza mafunzo kwa
wapelelezi au waendesha mashtaka, kutokana na watuhumiwa wengi wa rushwa
kuachiwa huru.
Kuhusu uchumi, Rais Kikwete ambaye amewahi kuwa
Waziri wa Fedha alisema kinachofanyika ni kuimarisha uchumi mkubwa, na
kwa mujibu wa wachumi, uchumi wa nchi ukikua kwa asilimia saba katika
kipindi cha miaka 10, pato la taifa huongezeka mara mbili na uchumi wa
Tanzania umekuwa ukikua kwa asilimia saba kwa kipindi hicho.
Akizungumzia uhusiano wake na Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Kikwete alisema hana mgogoro na kiongozi huyo, alichokifanya ni kutoa ushauri kuhusu namna ya kutatua migogoro ndani ya nchi yao, ni hiari yao kufuata ushauri wake
source: mwananchi
Akizungumzia uhusiano wake na Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais Kikwete alisema hana mgogoro na kiongozi huyo, alichokifanya ni kutoa ushauri kuhusu namna ya kutatua migogoro ndani ya nchi yao, ni hiari yao kufuata ushauri wake
source: mwananchi
No comments:
Post a Comment