Siku moja
baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samwel Sitta kukiri
kuchezewa kwa saini ya aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius
Msekwa na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Msekwa amesema,
'mzungumzaji huyo ana lake jambo'.(Hudugu Ng'amilo)
Sitta
akizungumza juzi mjini Dodoma alisema ni kweli kuna maneno katika hati
hiyo ya sheria namba 22 ya 1964, iliyosainiwa na Nyerere na Msekwa,
Aprili 25, 1964, yameongezwa.
Alifafanua
kuwa saini ya Nyerere imeongezwa herufi 'us' kwa kompyuta na katika
sehemu ya saini ya Msekwa kumeandikwa neno 'Msekwa' kwa kompyuta, jambo
ambalo ni makosa. Sitta alisema walioongeza maneno hayo ni wafanyakazi
wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali baada ya kuona sehemu ya
maandishi kwenye saini hizo hayasomeki, lakini walifanya makosa.
Msekwa
akizungumza jana alisema: "Saini iliyo katika hati original (halisi) ni
ya kwangu mimi, lakini huyo anayesema zimechezewa muulizeni atakuwa na
lake jambo. Kama kompyuta imekosea ni leo kwa kuwa kipindi hicho
kompyuta hazikuwapo."
Aliongeza:
"Ana lengo gani la kutilia shaka, ana lengo gani la kusema
imechakachuliwa, kinachotakiwa ni hati original ambayo iko ofisi ya
Katibu wa Bunge itolewe, kwanini tuendelee kuandikia mate wakati wino
upo?"
Maoni mengine
Mjumbe wa
Bodi ya Kituo cha Taarifa kwa Wananchi Umma (TCIB), Hebron Mwakagenda
alisema yote hayo yanatokea ni kuvuruga hoja iliyopo mezani.
Alisema
kitendo cha kupoteza muda kuzungumzia suala la kuchezewa kwa saini
halitakiwi kwani kama maudhui yake hayakuchezewa basi hoja ya muundo wa
Muungano uamuliwe na wananchi wenyewe.
"Tusianze
kupoteza muda kwa mambo ambayo hayapo cha msingi wananchi wenyewe
waulizwe wanaupenda Muungano au la lakini tusianze kumtafuta mchawi kuwa
saini zimechezewa wananchi waamue wenyewe kuhusu Muungano," alisema
Mwakagenda.
Sakata lilivyoanza
Utata huo
ulianza wiki hii baada ya kamati za Bunge Maalumu la Katiba kuanza
vikao vyake vya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba,
zinazohusu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na muundo wake.
Hali hiyo
ilitokana na kutopatikana kwa hati ya Muungano wa Tanganyika na
Zanzibar na ile ya Sheria ya Baraza la Mapinduzi ya kuridhia Mkataba wa
Muungano.Aprili 2 mwaka huu, Kamati namba 2 ilimwalika, Spika Mstaafu wa
Bunge la Muungano, Pius Msekwa kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo, lakini
uhalali wa saini zake uliibua malumbano makali. Msekwa aliitwa kutokana
na kwamba ndiye aliyekuwa Katibu wa Bunge la Tanganyika wakati huo.
Mwenyekiti
wa kamati hiyo, Shamsi Vuai Nahodha, alithibitisha kutokea utata huo na
kwamba walilazimika kumuita Msekwa ili kupata ufafanuzi wa masuala
kadhaa na Msekwa alisema saini zilizopo katika hati hiyo ni ya kwake.
Nahodha
alisema kwa maelezo ya Msekwa, inaonekana hati ya Muungano ipo Umoja wa
Mataifa (UN), kwani kabla ya Muungano, Tanganyika ilikuwa na kiti chake
UN na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar hali kadhalika.
Aliongeza kuwa baada ya UN kuomba uthibitisho wa Muungano, ndipo walipelekewa hati hiyo na kwamba haijawahi kurejeshwa.
Kwa
upande wake Katibu wa Bunge la Katiba, Yahya Hamis Hamad alisema hati
hiyo ipo Dar es Salaam na ni moja tu, hivyo siyo rahisi kuipeleka
bungeni Dodoma.
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment