WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Friday, April 18, 2014

Ukawa washikilia Katiba Mpya

  Kususia kwao mchakato kuathiri uamuzi
John Mnyika
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahya Khamis Hamad, amesema hatua ya kundi la wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) itaathiri maamuzi ya Bunge hilo kupitisha vifungu vya Rasimu ya Katiba mpya.
Alitoa kauli hiyo katika mahojiano na NIPASHE mjini hapa jana na kusema hiyo ni kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba Kifungu cha 26 (2) na Kanuni ya 64 (1) ya Bunge Maalumu, ili kufikia maamuzi, ni lazima kufikia uwiano wa theluthi mbili za wajumbe wote kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote kutoka Tanzania Zanzibar.

Hata hivyo, Hamad alisema Bunge halijafikia hatua ya kufanya maamuzi, hivyo hakuna haja ya kulizungumzia suala hilo.

 Alisema Ukawa hadi jana jioni walikuwa hawajawasilisha taarifa rasmi Ofisi za Bunge za kujitoa.

Akizungumzia hatima ya wajumbe 25 wa kundi la 201 waliojiunga na Ukawa kususia Bunge hilo, Hamad alisema sheria ipo kimya kuhusiana na suala hilo.

“Hata hivyo, kama mtu anasusia au kugoma, viongozi wana mamlaka ya kuchukua hatua,” alisema na kuongeza kuwa Kamati ya Uongozi ilikaa na kuzungumzia suala hilo na maamuzi yatatolewa.

WAJUMBE WATHIBITISHA KAULI YA KATIBU WA BUNGE
Wakizungumza na NIPASHE mjini Dodoma jana, baadhi ya wajumbe wa Bunge hilo, wakiwamo wanasheria walitoa maoni kuhusiana na hatua ya Ukawa kususia Bunge hilo na athari zinazoweza kupatikana katika kufikia maamuzi.

TUNDU LISSU
Mjumbe wa kundi linalounda Ukawa, Tundu Lissu, alisema theluthi mbili inayotajwa ni wajumbe wote, ambao wametajwa katika tamko la Rais lililoitisha Bunge Maalumu.

Alisema kutokana na Ukawa kujiondoa, Bunge hilo sasa haliwezi kupata theluthi mbili za kupitisha maamuzi.

Hata hivyo, alisema kikao kinachoendelea ni sahihi, kwani kina akidi mbili ya kuanza kikao na kutoa maamuzi.

“Akidi inayokosekana ni ya kufanya maamuzi, ya kuendelea kujadidli bungeni wanayo,” alisema Lissu.
 
PAUL KIMITI
Mwanasiasa mkongwe, Paul Kimiti, alisema kitendo hicho kitakuwa na athari kwa upande wa Zanzibar kupata theluthi mbili ya kura katika kupitisha sura na hatimaye katiba nzima.

“Kwa upande wa Tanzania Bara, hakuna tatizo. Itapatikana. Lakini upande wa Zanzibar itakuwa ngumu. Na lazima ujue hata kama wangekuwapo, ingekuwa vigumu kupatikana, kwani wajumbe kutoka Zanzibar wamegawanyika katika misingi ya itikadi za kisiasa CCM na CUF. Hivyo, kupata theluthi mbili ni ngumu. Hakuna anayejali hoja za mwenzake,” alisema Kimiti na kuongeza:

“Jambo hili litatusumbua sana. Sheria haikuzingatia hali halisi ya siasa za Tanzania, kwani jambo hata liwe zuri kiasi gani halitapita kwa sababu tu ya misimamo ya kisiasa. Tunawaomba wenzetu watuelewe. Tuna nia njema kabisa ya kupata katiba bora.”

ABDULKARIM SHAH
Mjumbe mwingine, Abdulkarim Shah, naye alisema itakuwa vigumu kwa wajumbe wa upande wa Zanzibar kupatikana theluthi mbili, baada ya baadhi yao kususia Bunge linaloendelea.

“Kutoka kwa wenzetu bungeni, kumenisikitisha sana. Wajue kwamba, tumekuja hapa kutengeneza katiba ya wananchi siyo ya vyama. Katiba ikishindikana, watakuwa wamewaangusha Watanzania,” alisema.

ASHA MTWANGI
Mjumbe Asha Mtwangi kutoka kundi la 201, alisema ana imani kama wajumbe watakuwa na nia njema ya kuwapatia wananchi katiba mpya iliyo bora, theluthi mbili ya wajumbe itapatikana kwa kila upande.

GOSBERT BLANDES
Mjumbe Gosbert Blandes alisema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, inalitaka Bunge katika kufikia maamuzi, lazima pande zote mbili zifikie theluthi mbili.

Alisema sheria hiyo inasema ni lazima theluthi mbili zipatikane kutoka Tanzania Bara na Zanzibar na maamuzi hayo yanatakiwa kufanyika katika kupitisha kila sura na ibara.
Blandes, ambaye ni mwanasheria, alisema iwapo theluthi mbili hazijapatikana au imepatikana upande mmoja, kipengele hicho kitakuwa kimekwama.

“Na iwapo tutafika mwisho na kupiga kura kwenye katiba, tutahitaji kupata theluthi mbili kutoka Bara na theluthi mbili kutoka Zanzibar,” alisema Blandes, ambaye pia ni Mbunge wa Karagwe (CCM).
Alisema iwapo Zanzibar au Tanzania Bara haikupata theluthi mbili kupitisha rasimu hiyo, mchakato wa katiba utakuwa umeishia bungeni na katiba iliyopendekezwa haiwezi kupita.

NAIBU WAZIRI

Naibu Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Abdallah Juma Sadallah, alisema maamuzi makubwa ya kupitisha mambo makubwa kama katiba yana njia mbili, ambazo unaweza kuamua kutokana na idadi ya watu watakaokuwapo.

Alisema katika mambo ya kitaifa, ni lazima itafutwe theluthi mbili, ambayo ukiigawa, unapata asilimia 66.6 kwa kila upande na kuwa uamuzi huo unachukulika kama kielelezo cha kidemokrasia.

“Hili katiba Baraza la Wawakilishi linatumika kwa mambo mazito…na katika Bunge la Jamhuri ya Muungano nayo ni kwa mambo mazito, yaani upande wa Zanzibar na wale wa Tanzania Bara,” alisema.

Alisema kama haikufikia theluthi mbili, hufanyika utaratibu mwingine wa kuangalia pande hizo mbili zimeshindana kwa asilimia ngapi.

“Tuangalie hawa hawakupata theluthi mbili. Lakini tunaangalia je, imefikia asilimia ngapi?…kwa sababu unaweza kusema hawakufikia asilimia 66, lakini wamefika asilimia 60. Sasa basi, ukitaka kuzungumza na mwenzio ndiyo hapo mnaingia kwenye maridhiano,” alisema.

Aidha, alisema iwapo theluthi mbili haitopatikana katika baadhi ya ibara inabidi kufanya maridhiano na ikishindikana rasimu hiyo haitapita.
 
ISACK CHEYO
Mjumbe Isack Cheyo kutoka chama cha United Democratic (UDP), alisema sheria na kanuni zilivyo, katika hali ya sasa bungeni, hakuna mshindi kwa sababu zinasema wajumbe theluthi mbili wa pande zote wanatakiwa kukubaliana katika maamuzi.

Lakini akasema hali ya ndani Tanzania Bara inaweza kufikisha idadi hiyo, lakini kwa wajumbe kutoka Zanzibar haitawezekana.
 
JOHN MNYIKA
John Mnyika alisema sheria inasema katika kufanya maamuzi inatakiwa theluthi ya wajumbe wote hata kama mjumbe aliyekwishaapa hatakuwapo.

“Katika maamuzi aliyekuwapo awali, atahesabiwa kama mjumbe wa kikao. Kutokuwapo hakumfanyi mjumbe asiwe mjumbe halali,” alisema Mnyika na kuongeza kuwa kutokuwapo kwa wajumbe wa Ukawa kutaathiri theluthi mbili kwa kuwa inahitajika katika mahudhurio hadi maamuzi.
 
WAJUMBE WA 201
Kwa mujibu wa Lissu, Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya 2013 haiwabani wajumbe 201 walioteuliwa na Rais.

Kwa hiyo, waliojiunga na Ukawa kususia Bunge, hakuna sheria inayoelekeza hatua za kuwachukulia licha ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kusema wataitwa na kuhojiwa.

Alifafanua kuwa Rais akishateua, hana mamlaka ya kutengua uteuzi wala kuufuta.

Imetayarishwa na Theodatus Muchunguzi, Abdallah Bawazir, Gaudensia Mngumi na Jacqueline Massano, Dodoma.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment