Wachezaji wa
Zanzibar wakiwa wamembeba kipa wao, Mwadini Ally baada ya kupangua mkwaju mmoja
wa penalti, na kuiwezesha timu hiyo kutinga Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya
Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge baada ya kuifunga Burundi kwa
penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Lugogo, mjini Kampala, Uganda jioni hii. Zanzibar
sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi.
Na Mahmoud Zubeiry,
Kampala
ZANZIBAR imeingia
Nusu Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker
Challenge baada ya kuifunga Burundi kwa penalti 5-4 kwenye Uwanja wa Lugogo,
mjini Kampala, Uganda jioni hii kufuatia sare ya bila kufungana ndani ya dakika
90.
Kwa matokeo hayo,
Zanzibar sasa itacheza na mshindi kati ya Kenya na Malawi katika Nusu Fainali.
Shujaa wa Zanzibar
leo alikuwa ni Abdallah Othman aliyefunga penalti ya mwisho, baada ya kipa
Mwadini Ally kupangua penalti ya Abdul Fiston wa Burundi.
Manahodha
wa timu zote, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ wa Zanzibar na Suleiman Ndikumana wa
Burundin walipoteza penalti zao leo.
Ndikumana alikuwa wa
kwanza kwenda kupiga na mkwaju wake ukaota mbawa na kupaa juu ya lango, wakati
wenzake waliofunga mbali na Fiston kupoteza ni Steve Nzigamasabo, Amisi Tambwe,
Chris Nduwarugira, Leopold Nkurinkiye na Gael Duhatindavyi.
Upande wa Zanzibar
Heroes, Khamis Mcha ‘Vialli’ alikwenda kufunga penalti ya kwanza ya Zanzibar,
Adeyom Saleh Mohamed akafunga ya pili, Jaku Juma akafunga ya tatu, kabla ya
Cannavaro kumpelekea mikononi mkwaju wake kipa Arthur Arakaza wa Burundi, Samir
Hajji Nuhu akafunga ya tano, Aggrey Morris akafunga ya sita na Othman
kutumbukiza nyavuni ya ushindi.
Zanzibar leo walicheza
soka ya kuvutia na kiungo Suleiman Kassim ‘Selembe’ ndiye aliyekuwa nyota ya
mchezo kutokana shughuli kubwa aliyoifanya akicheza katika dimba la juu.
Ndikumana leo aliwekewa
ulinzi mkali na hakuwa na madhara kwa Watanzania wa upande wa pili wa
Bahari.
Mapema katika mchezo wa
kwanza wa Robo Fainali, Bara ilifanikiwa pia kuingia Nusu baada ya kuilaza
Rwanda mabao 2-0 kwenye Uwanja huo huo wa Lugogo mjini hapa.
Hadi mapumziko, Stars
walikuwa mbele kwa bao 1-0 lililotiwa kimiani na kiungo Amri Kiemba, dakika mya
33 akiunganisha pasi ya Mwinyi Kazimoto aliyewapunguza wachezaji wawili wa
Rwanda kabla ya kutoa pasi maridadi.
Katika mechi hiyo iliyochezeshwa
na refa Mohamed El Fadil kutoka Sudan, mshambuliaji John Raphael Bocco
‘Adebayor’ alikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi ya Rwanda na aliwafanya
waende kwenye vyumba vya kupumzikia wakiwa hoi.
Katika hicho kipindi cha
kwanza, Rwanda walikosa bao la wazi dakika ya 12 baada ya krosi ya Jean Claude
Iranzi kuokolewa na beki Kevin Yondan kwa kichwa na dakika ya 19 Jean Baptiste
Mugiraneza alipiga juu akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.
Stars pamoja na kufunga
bao hilo kipindi hicho cha kwanza, katika dakika ya 30 krosi nzuri ya Salum
Abubakar ‘Sure Boy’, Mrisho Ngassa na Bocco walishindwa kuiunganisha na
ikawapita wote.
Ngassa tena, katika dakika
ya 38 alipiga shuti kali kutoka wingi ya kushoto, lakini likaenda nje sentimita
chache.
Kipindi cha pili,
Kipindi cha pili Stars
walirudi vizuri tena na kuendelea kucheza kwa kuonana, ingawa na Rwanda nao
waliendelea kucheza kwa bidii kutafuta bao la kusawazisha.
Hata hivyo, walikuwa ni
Stars tena waliofanikiwa kupata bao la pili 53 baada ya John Bocco kuuwahi
mpira uliotemwa na kipa Jean Claude Ndoli kufuatia shuti kali la Mwinyi
Kazimoto kutoka nje ya eneo la hatari.
Baada ya bao hilo, Rwanda
walionekana kupagawa, lakini hawakusahau kushambulia lango la Stars na dakika
ya 86 Dadi Birori hakujali ameotea akasukuma mpira nyavuni, lakini refa
akakataa bao hilo.
Kwa ushindi huo, Stars
sasa inasubiri mshindi kati ya Uganda na Ethiopia kesho kukutana naye kwenye
Nusu Fainali.
Stars; Juma Kaseja, Erasto
Nyoni, Amir Maftah, Shomary Kapombe, Kevin Yondan, Amri Kiemba, Salum
Abubakar/Athumani Iddi dk51, Frank Domayo, Mwinyi Kazimoto, Mrisho Ngassa na
John Bocco/Shaaban Nditi dk 85.
Rwanda; Jean Claude Ndoli,
Emery Basiyenge, Ismail Nshutimayamangara/Fabrice Twagizimana dk19, Jimmy
Mbaraga/Imran Nshiyimana dk67, Charles Tibingana/Barnabe Mbuyumbyi dk61, Michel
Rusheshangoga, Jean Baptiste Mugiraneza, Haruna Niyonzima, Jean Claude Iranzi,
Dadi Birori na Tumaine Ntamuhanga
Imewekwa na MAPARA
TASWIRA MBALIMBALI ZA MECHI KATI YA STARS V RWANDA , ZANZIBAR V BURUNDI
Wachezaji wa Bara wakimpongeza Bocco baada ya kufunga bao la pili katika Robo Fainali ya kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Rwanda. Bocco alishangilia huku akichechemea baada ya kufunfa bao hilo kutokana na kuumia, baada ya kugongwa na kipa wa Rwanda, Jean Claude Ndoli wakati anaenda kufunga. Bara ilishinda 2-0 na kutinga Nusu Fainali.
Mfungaji wa penalti ya mwisho na ya ushindi ya Zanzibar, Abdallah Othman akikimbia kushangiloia baada ya kumaliza mechi ya Robo Fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA Tusker Challenge dhidi ya Burundi kwenye Uwanja wa Lugogo mjini Kampala, Uganda, Zanzibar ilishinda kwa penalti 6-5 baada ya sare ya 0-0 ndani ya dakika 90.
Kaseja amedaka, huku Yondan akiwa tayari kumsaidia
Manahidha wakisalimiana kabla ya mechi, Juma Kaseja wa Bara kulia na Haruna Niyonzima wa Rwanda kushoto
Kikosi cha Rwanda leo
Kikosi cha Bara leo
Watanzania waliokuja kuisapoti timu hapa
Shomary Kapombe akimdhibiti Dadi Birori
Athumani Iddi 'Chuji' akiruka juu kulia kuokoa
Amri Kiemba anamkokota mchezaji wa Rwanda
Kocha Milutin Sredojevic 'Micho'
John Bocco akiwashughulisha mabeki wa Rwanda
Refa anaonyesha kati, baada ya Kiemba anayekimbia nyuma yake kufunga bao la kwanza
Bao la Kiemba
Mwinyi Kazimoto kulia akimburuza mchezaji wa Rwanda
Ulinzi mkali langoni mwa Rwanda, lakini bado mbili zilipenya
Bocco anasababisha
Jean Claude Ndoli wa Rwanda aliyeruka hewani kudaka moja ya michomo ya hatari iliyoelekezwa langoni mwake
Mwinyi huyooo
Ndikumana chini, shughuli ya Issa Othman Ally kushoto
Aggrey Moris akimdhibiti mshambuliaji wa Burundi
Suleiman Kassim Selembe kulia anakokota ngoma
Abdulaghan Gullam akitafuta mbinu za kumtoka mchezaji wa Burundi
Aggrey Morris anapanda kusaidia mashambulizi baada ya kuokoa
Selembe anapasua katikati ya watu
Issa Othman Ally anaondoka na mpira mbele ya wachezaji wa Burundi
Jaku Juma akipambana na beki wa Burundi
Ndikumana akijuta baada ya kukosa penalti
Balozi wa Tanzania nchini Ugamda, kulia akimpongeza kocha wa Zanzibar
Wachezaji wa Zanzibar wakimpongeza Abdallah Othman
Wachezaji wa Zanzibar na baadhi ya viongozi wakimpongeza Abdallah Othman katikati aliyesujudu
Picha zote kwa hisani ya Bin Zubery Blog
No comments:
Post a Comment