Tusiwe watu wa ‘fasta
fasta’, tunayo miaka bilioni ya kuishi hapa
Makala
yangu iliyopita ilijadili umuhimu wa kuwa na mtazamo wa mbali, na kufanya
mipango yetu kwa kuamini kwamba taifa letu litakuwapo baada ya sisi tuliopo
kutoweka.
Hii ina
maana ya kuachana na mtindo wa kulipua na kufanya kazi kwa njia za zimamoto.
Ina maana ya kupanga miradi mikubwa ndani ya programu pana zinazoangalia upeo
wa karne kadhaa zijazo.
Kila
nikitathmini utendaji wetu, na hasa utendaji wa wakuu wa Serikali, sioni
mtazamo wa aina hiyyo. Ninachoona ni kufanya mambo ‘ad hoc,’ haraka haraka, kwa
ajili ya leo au kesho tu, halafu tutaangalia. Tunalipua, hatuna mtazamo wa
kimkakati, kana kwamba muda si mrefu ujao tutakuwa hatupo tena.
Kutokana
na hali hii, tumezalisha ‘viongozi’ wengi wanaodhani kwamba kuchapa kazi maana
yake ni kupiga kelele majukwaani, kutoa amri kwa watendaji kupitia kauli za
majukwaani na kupitia televisheni.
Leo
hii, kila ‘kiongozi’ anashindana na mwingine kwa kujaribu kutoa amri nyingi
kuliko mwingine. Matokeo yake ni kwamba hatuna mipango ya muda mrefu wala
mipango iliyoratibiwa kuhusisha nchi nzima na sekta zote. Kila amri
inajitegemea na kila ‘kiongozi’ ana mipango yake.
Hii
ndiyo staili ninayoiita u-Mrema kutokana na staili aliyoianzisha Augustine
Mrema alipokuwa waziri aliyehusika na mambo ya usalama wa raia.
Naamini
kwamba Mrema alichukua staili ya kutoa matamko mengi hadharani ambayo mengi
yalikuwa ni amri kwa watu aliowataka wafanye hili au lile, kwa sababu hakuwa na
uwezo wa kutambua ni vipi Serikali inatakiwa kufanya kazi, akidhani kwamba
waziri mchapa kazi ni yule anayekwenda mwenyewe kukamata walanguzi wa pombe na
wafanya magendo ya kahawa.
Kinachotusumbua
leo, ni kwamba Mrema alifanikiwa mno katika juhudi zake za kupata umaarufu, kwani
wananchi wa kawaida ambao nao hawajui ni jinsi gani Serikali inatakiwa ifanye
kazi yake, walimuona kama shujaa.
Wananchi
wa kawaida waliziona zile amri za ‘siku saba’ kama ushahidi wa waziri
anayefanya kazi yake bara bara. Wala hawakuhoji ni kwanini mara kadhaa
aliwataka wafanyabiashara walioonekana kama wasio waaminifu wamfuate kijijini
kwake Moshi.
Wananchi
pia hawakuhoji ni kwanini Mrema alikuwa na ujasiri wa kuwalaumu mawaziri
wenzake hadharani kwa kusema kwamba walikuwa wanamzuia kufanya kazi yake
kikamilifu kwa kuwa walikuwa si waaminifu kwa wananchi.
Bila
shaka walikuwapo mawaziri walioona kwamba utendaji kazi serikalini haukupaswa
kuwa jinsi Mrema alivyokuwa akifanya, na bila shaka walisema hivyo katika vikao
vya Baraza la Mawaziri, lakini wakaonekana kama wasio na maana.
Katika
utaratibu wa Serikali inayoendeshwa kama Serikali, ilitakiwa Rais Ali Hassan
Mwinyi (wakati huo wa Mrema) amuondoe serikalini mapema asubuhi kwa kukiuka
utaratibu wa Serikali.
Badala
yake akampandisha cheo na kumfanya Naibu Waziri Mkuu, huku akiendelea kuwa
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, mamlaka makubwa mno mikononi mwa mtu
aliyekuwa ametia fora katika kuvuruga utaratibu wa utendaji serikalini. Sababu
zake ni nini? Nitajaribu kueleza.
Utawala
unaokabiliwa na malalamiko mengi ya wananchi bila kuwa na maelezo ya
kuridhisha, utakumbatia kila aina ya ubabaishaji alimradi unashabikiwa na
wananchi, kimsingi kwa sababu ushabiki wa wananchi unaonekana kuujengea
uhalali, na Mrema alionekana hivyo.
Wala
hakuwa wa kwanza, kwani hata Edward Sokoine alikuwa na muonekano huo wakati wa
kile kilichojulikana kama ‘Uhujumu Uchumi.’ Maana yake ni nini? Mfumo uliochoka
na ulioshindwa kutafuta majibu sahihi kwa maswali ya wananchi, utaegemea juhudi
za kiimla za mtendaji mmoja mmoja, kama Sokoine chini ya Mwalimu Nyerere na
Mrema chini ya Ali Hassan Mwinyi, na hawa tunaowashuhudia chini ya Rais Jakaya
Kikwete.
Maana
yake ni kwamba ni rahisi zaidi kuachia watu wawili au watatu wakapita wakifoka
na kutoa amri, badala ya kujenga mifumo ya utekelezaji iliyosimama juu ya
misingi ya kisera na kisheria, ambayo inasumbua akili, inahitaji usimamizi
makini na inahitaji uratibu ulio makini wa sekta zote zinazohusika na
zinazoingiliana. Hiyo ni kazi ngumu zaidi kuliko kutoa amri za kiimla.
Lakini
ni staili dhaifu na isiyo endelevu, haina mashiko ya kiutekelezaji, haina uwezo
wa kuenea kote nchini na inatoweka mara tu anapoondoka madarakani waziri au
mkuu yeyote aliyeianzisha. Ni moto wa kifuu unaowaka sehemu ulipowashiwa,
lakini usiosambaa sehemu nyingine yo yote, na baada ya muda mfupi tu
kitakachosalia ni majivu baridi.
Wale
wanaopendelea staili hii wanapaswa wajiulize, iwapo waziri ametembelea wilaya
moja ambako amekuta matatizo ya utendaji mbovu na akaona jawabu ni kutoa amri
ya kumsimamisha mtendaji au kusitisha zoezi fulani, je; ni wilaya ngapi anaweza
kujua zinaendeshawa vipi, zina matatizo yapi, na ni ngapi anaweza kuzitembelea
katika kipindi cha miaka mitano, na ni amri ngapi anaweza kutoa na kufuatilia
utekelezaji wake?
Tatizo
linalojitokeza katika wilaya moja linaweza kuwa ni ishara kwamba kuna matataizo
ya aina hiyo hiyo katika wilaya zote nchini. Watu wetu wanazo tabia
zinazofanana, mazoea ya utendaji yametufanya tujenge utamaduni unaoshabahiana,
na mara nyingi tunaambukizana udhaifu kama vile wizi, ubadhirifu, uzembe na
kutokujali.
Hivyo,
matatizo yetu yanaweza kupatiwa majawabu ya jumla iwapo tutaketi na kuyajadili
kama nchi na kuyatafutia dawa badala ya kutegemea amri za kiimla.
Ukoloni
ulikuwa ni mfumo wa hovyo, wa nchi moja kuitawala nyingine, lakini pamoja na
maovu yao yote, wakoloni walituachia utaratibu wa utendaji serikalini ambao
uliwafaa wao wakati wakitutawala na ungeweza kutufaa sisi pia, tukifanya
marekebisho kidogo. Cha kustaajabisha, ni kwamba yale maovu ya wakoloni
tumeyakumbatia, wakati yale machache mazuri tumeyatupilia mbali.
Hebu
tuirejee, tuiangalie mifumo yetu ya utawala, tuirekebishe. Tusifanye ‘fasta
fasta’ kwani bado tupo hapa kwa karne kadhaa zijazo, miaka milioni kadhaa.
Tunakimbilia wapi; tunakimbilia nini
Source: Raia
mwema
No comments:
Post a Comment