- HII KULINGANA NA MAPITIO YALIYOFANYWA NA BLOG YA UKADIRIFU NA MUNGUPAMOJANASI.
Kama umeshawahi kupata na kusoma makala mbalimbali za mwandishi Maggid mjengwa katika magazeti ya Raia Mwema, na Kwanzajamii kwa kweli utakubaliana na mimi
kuwa Ndugu Magid amekuwa ni mwandishi ambaye amesaidia sana kuelimisha jamii
katika hoja mbali mbali za maendeleo hata pale hoja zake zilipokuwa zikipingwa
na watu wengine lakini aliendelea kusimama katika ukweli kwa faida ya Jamii ya
Tanzania na mwisho wa siku ukweli unabaki kuwa ukweli.
Makala zake zimetumiwa na blogs nyingi katika kuhabarisha
jamii ya Tanzania waishia popote pale duniani.
Amekuwa ni mwandishi ambaye amekuwa akiandika na
kujishughulisha sana na maisha ya jamii za kawaida na wakati na kukosoa utendaji
wa serikali katika mazingira yeyote yale bila hata kuuma uma akiwa anasimamia
ukweli.
Amekuwa anajitahidi sana kuelimisha jamii bila kusimamia
upande wowote wa siasa hata kama anajijua ni mpenzi wa mwanasiasa au chama gani.
Hebu tuangalie baadhi tu ya nakuu zake ambazo zimetokana
na kazi zake mbalimbali:
BARAZA
JIPYA LA MAWAZIRI: TAFSIRI YA MAGGID MJENGWA ( MAKALA, RAIA MWEMA).
“Kijana, hatukuandika bei, maana, gharama ya ukweli mzima
ni uhai wako. Je, uko tayari kulipa?” Kijana yule akatimua mbio. Nyuma aliacha
vumbi. Hakuwa tayari kulipa gharama ya ukweli mzima. Yumkini ukweli utakaousema
mwanadamu waweza usiwafurahishe wachache, walakini, ukawa wenye kuleta tija,
furaha na matumaini kwa walio wengi. Mimi nitasena hapa ukweli wangu, kuwa
Baraza jipya la mawaziri ni mabadiliko ya sura ya Baraza lakini si mabadiliko
ya mfumo uliosababisha udhaifu wa kiutendaji ikiwamo ‘madudu’ yale tuliyoyaona
bungeni hivi karibuni.”
“Ushauri kama huu unafundisha tu si wanasiasa hata
jamii kuelewa kuwa hata kama kesho CUF
au CHADEMA wakiingia madarakani kwa mfumo huu huu, nao, kwa kiasi kikubwa,
watafanya hivi hivi. Ndio maana ya kusisitiza, kuwa, tulilo nalo sasa ni tatizo
la kimfumo ambalo ndiyo chimbuko la utendaji mbovu wa kuanzia mawaziri na walio
chini yao. Ni mfumo unaomfanya waziri, awajibike zaidi kwa chama chake badala
ya taifa kwa ujumla wake”.
Gulio la mafisadi makala ya Raia mwema/ Spika Makinda
‘amechemsha’ Raia Mwema 217
“Tulipo sasa ni kwa baadhi ya viongozi wetu kuigeuza nchi
yetu kuwa gulio la mafisadi. Kwamba kila mwenye uwezo atafute mtaji. Awahi
nafasi ya uongozi itakayomsaidia kuingia gulioni. Huko ni mahala pa kufanya
biashara, si kuwatumikia wananchi. Kwa bahati mbaya, hata rasilimali zetu
wanazipeleka gulioni. Ili kuinusuru nchi yetu, sote kwa pamoja. Bila kujali
itikadi zetu za vyama, tuna lazima ya kulifunga gulio hili Sasa”.
Miaka 51 ya Uhuru na maneno ya Mkapa makala Raia Mwema
272
“Kuwapo kwa
amani na usalama katika nchi, hujengeka katika misingi ya haki na usawa,
misingi ya kuaminiana. Misingi ya kuheshimu haki na uhuru wa raia kutoa mawazo
yao. Ni lazima kuwapo misingi imara ya demokrasia. Wananchi ni vema wakawaamini
viongozi wao, na viongozi pia ni vizuri wakawaamini wananchi wao. Na ili
viongozi waaminike, ni lazima wawe wakweli na wawazi na Wawe waadilifu”.
“Haya ni mambo ya msingi
kabisa kuyatafakari. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Ni lazima tuaminiane.
Tulio wengi tuna mapenzi ya dhati na nchi yetu. Kama taifa, miaka 51 ya Uhuru
inatutaka tutafakari kwa kina juu ya mustakabali wa taifa letu”.
“Maana, haitakuwa
busara kuliacha suala hili likapita kama yanavyopita mengine ilihali
limegharimu maisha ya Watanzania. Na kubwa zaidi kwa sasa, ni kwa pande zote
katika mgogoro huu kutambua; kuwa kwa sasa mvutano unaoendelea hautatoa
mshindi, ni kwa vile, katika kilichotokea na kinachoendelea kufanyika sasa,
sote, kama Taifa, tumeshindwa”.
“Huu ni wakati wa kutanguliza busara na hekima. Tufanye
yote, lakini, njia mujarab ya kutanzua mgogoro huu uliopo sasa ni mazungumzo
katika mazingira ya kuheshimiana, basi. Kinachoonekana sasa ni kwa baadhi ya
viongozi kuwa mbali na umma. Viongozi kuwa mbali na hali halisi. Baadhi
ya kauli wanazotoa zinadhihirisha umbali huo kati yao na wanaowaongoza”.
Tanzania ina vyote kasoro Watanzania Toleo la 218
“Nimepata kuandika huko nyuma (Juni 16, 2004) kuwa
Tanzania ina vyote, kasoro Watanzania. Niliandika; kuwa Tanzania ni nchi nzuri
sana. Ni nchi ya kujivunia. Kwamba Tanzania ni nchi kubwa sana kwa eneo. Ni
nchi yenye rasilimali nyingi; ardhi yenye rutuba, mito, maziwa, milima,
mabonde, bahari na vivutio vingi vya asili. Hata hivyo, Tanzania ni moja ya
nchi masikini sana duniani. Kwa nini? Ndiyo, kikubwa kinachokosekana Tanzania
ni Watanzania. Tanzania tunayoijenga sasa ni mkusanyiko tu wa watu wa makundi
mbalimbali wenye kwenda kwa staili ya 'kila mtu na lwake'. Idadi ya Watanzania
wenye uzalendo na mapenzi kwa nchi yao inazidi kupungua. Ubinafsi umekithiri,
na ubinafsi mbaya zaidi ni ule wenye kufanywa na viongozi.”
" Bila Utawala Bora, bila kuwa na demokrasia, bila
kuheshimu Haki za Kibinadamu, mafanikio ya kiuchumi hayatawezekana."
“Hakika hakuna uchumi unaokua bila uwepo wa utulivu wa
kisiasa. Kina Jaji Warioba wahakikishe wanaleta Katiba itakayohakikisha, mbali
ya mambo ya mengine, inatupa Tume Huru Ya Uchaguzi”
CCM
Kama Barcelona! ( Makala, Raia Mwema)
“CCM nayo inaamini, siku zote, kuwa kuna njia moja tu
ya kuendesha siasa katika nchi hii, na njia hiyo ni ya CCM”!
Hakuna busara nyingine yeyote kwa sasa
bali ni kwa CCM kuruhusu na kuendesha kwa salama mchakato wa mabadiliko makubwa
yanayotakiwa na umma. Mabadiliko hayaepukiki. Ni hali ya dunia kwa sasa. Ni
kama wimbi la maji ya bahari. Limeshajikusanya. Kwa CCM chaguo ni moja tu,
kuenenda na wimbi hilo la mabadiliko au kukubali kufunikwa nalo.
Hilo la mwisho laweza kuharakisha kifo
cha CCM. Ni jambo baya, maana, hata kama Watanzania watachagua upinzani ifikapo
2015, nchi yetu inahitaji chama imara cha upinzani, na CCM inaweza kuvaa viatu
hivyo”.
“Nchi yetu inapita sasa katika kipindi kigumu tangu
tupate uhuru wetu. Ni kipindi kinachowataka viongozi, na hususan viongozi wa
kisiasa, kutanguliza hekima na busara badala ya jazba, chuki na visasi. Hayo
matatu ya mwisho ni mambo maovu yenye kuambukiza kwa haraka”.
“Kamwe tusiruhusu jazba, chuki na visasi vitawale siasa
zetu. Hii ni nchi yetu. Ni nchi yetu sote. Hakuna mtu, kikundi au
chama cha siasa chenye haki zaidi ya kuongoza nchi hii kuliko wengine wote”.
Mwandishi Ni Mjumbe, Hauawi- Makala Ya Maggid Mjengwa
Raia Mwema September 7 2012
“Hii ni nchi yetu. Tutafanya makosa makubwa
kuwaachia viongozi wa kisiasa pekee, jukumu la kulinda maslahi ya nchi
yetu. Tunapita sasa katika kipindi kigumu tangu tupate Uhuru.
Dunia imebadilika, na nchi yetu inapitia
kwenye kipindi cha mabadiliko. Hakuna mtu au chama cha siasa kinachoweza
kuyazuia mabadiliko haya. Kufanya hivyo ni kutuletea machafuko na kuvunja
amani yetu. Tuna jukumu la kufanya tunayoweza, na kwa kutanguliza busara,
kuipitisha salama nchi yetu katika kipindi hiki cha mabadiliko. Maana,
tukiingia kwenye machafuko, basi, hakutakuwa na mshindi, maana, sote
tutashindwa”.
Dhana ya uandishi wa habari:
Mwandishi Maggid Mjengwa ameendelea kusimamia ukweli kuwa vyombo vyetu
vya habari vimekuwa vya kishabiki bila utumiaji wa taaluma ya kiuandishi, na tabia ya vyombo vya habari hususan magazeti kuibuka
na vichwa vya habari vinavyoashiria moja kwa moja uchochezi. Maggid alitoa
mfano kwamba “inaweza kutokea mtu mmoja ama mwislam au mkristo amefanya jambo
la kukashifu dini nyingine. Sasa badala ya kuandika fulani kafanya hiki na
kile, magazeti yanaibuka na vichwa vya habari tena kwenye kurasa za mbele
vyenye mwelekeo wa kujumuisha kundi zima la dini fulani. Utasikia "Waislam
wafanya fujo", au "Wakristo wakasirishwa". Aina hii ya
uandishi italipeleka Taifa pabaya;
ukombozi wa waandishi
“Huko nyuma nimepata kuanzisha mjadala wa umuhimu wa kuwepo kwa ruzuku kwa
vyombo vya habari ili navyo viweze kupata nguvu ya kuendesha shughuli zao
ikiwamo hata uwezo wa kuwasafirisha wanahabari wao kwenye matukio badala ya
gharama hizo za usafiri kutegemea ‘ bahasha’ za wanasiasa na wamiliki wa
makampuni ya biashara, ambao , masharti yasiyoandikwa ya wao kutoa bahasha zao,
ni namna wanahabari hao watakavyoripoti habari za kuwapamba na itakazowafurahisha
watoa bahasha”.
“Naam, wanahabari unganeni. Huu si wakati wa
kulilia huruma za watawala ikiwamo wanasiasa. Huu ni wakati wa kupambana kudai
ruzuku ya Serikali kwa vyombo vya habari. Ni ruzuku, pamoja na mauzo ( kama ni
magazeti) na matangazo ndivyo vitakavyo wafanya muwe huru. Vinginevyo,
mtaendelea kuachana na jukumu la kuutumikia umma wa Tanzania na badala yake
mtabaki kuwatumikia wanasiasa, wafanyabiashara na makampuni makubwa”.
Hatari ya siasa kuchanganyika na dini Raia Mwema 260
Watanzania tuliwashuhudia baadhi ya viongozi
wa kidini; Uislamu na Ukristo, wakitumia nyumba za ibada, si kwa kazi ya
kiroho, kazi ya kuhubiri yaliyo mema kwa mwanadamu, bali walifanya kazi ya
siasa. Kazi ya kuhutubia mambo ya siasa na kutoa maelekezo ya kisiasa ya moja
kwa moja.
Hayo yamefanyika misikitini na makanisani. Ni hatari! Jambo hili linaiweka rehani amani ya nchi yetu. Linahatarisha umoja wetu wa Kitaifa. Maana, makanisani na misikitini wanakusanyika Watanzania wa itikadi tofauti za kisiasa, na wengine ni watoto, hawajawa tayari kupokea hotuba za kisiasa, bali watoto wako tayari kupokea mahubiri na mafundisho ya kiroho.
Naam, ni ukweli sasa, kuwa dini imejichanganya na siasa. Na huu si mseto mwema kwa nchi yetu.
Udhaifu wa JK -
Tafsiri ya Maggid Mjengwa
“Kuna hoja mezani juu ya udhaifu wa JK, imetokea Bungeni. Yumkini,
kama mwanadamu, JK ana mapungufu na udhaifu wake, nani asiye na mapungufu na
udhaifu? Lakini, tukimzungumzia JK kama taasisi ya ’ Urais’, namwona Rais
anayejipambanua na waliomtangulia. Ni kwa kujitahidi kufanya yale yalo
nafuu na yenye manufaa kwa nchi yetu kwenye mfumo dhaifu uliopo.
Wanadamu
tunapaswa kuhukumu dhamira ya mtu na si matokeo. Bado namwona JK kama kiongozi
mwenye dhamira njema kwa nchi yetu. Nauona ujasiri ndani ya JK. Ni ujasiri wa
kufanya yale ambayo, hata ndani ya chama chake hayakupata fanyika”
“Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa. Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu”.
“Maana, katika jamii, mabadiliko yanapaswa yaendane pia na fikra mpya . Na jamii huingiwa na mashaka na kukosa imani pale fikra mpya zinapotekelezwa na watu wale wale ambao hawataki kabisa kuwaruhusu wengine kushiriki uongozi wa nchi. Watu ambao bado miongoni mwao wanaamini kuwa tofauti za kifikra ni jambo baya. Kwamba upinzani ni uadui, ni uhaini. Kwamba wapinzani ni wa kuwakatakata na kuwatupa. Sasa, katika hali ya sasa utawachinja wangapi ukawamaliza? Ni fikra za kiwendawazimu”.
KATIBA NA UKOMO WA MALI
“Kiongozi anayefahamu jinsi watu mitaani na vijijini
wanavyoathirika na vitendo vya ufisadi hatopata kigugumizi kukemea na kulaani
ufisadi kila anapopata fursa ya kufanya hivyo”.
“Tuna baadhi ya viongozi wenye utajiri wa ajabu
kushinda hata hao wafadhili wanaotupa misaada. Yote hii inatokana na ubinafsi
na uchoyo wa viongozi hawa. Wako tayari nchi inunue vifaa vibovu vya mamilioni
ya dola za Marekani ili mradi wao wamehakikishiwa 10% yao. Katiba iweke wazi, kuwa kutakuwapo na ukomo
wa kiwango cha fedha ambacho kiongozi wa kuchaguliwa au mtumishi wa umma
anaweza kutoa kama zawadi kwa jamii. Kinyume chake iwe ni kosa la jinai. Naam,
Katiba mpya itusaidie kuwafanya viongozi wetu wafukuzie zaidi maendeleo ya
wananchi kuliko mikate yao. Inawezekana”
kwa niaba ya Blogs za ukadirifu na mungupamojanasi tunakutakia kila la kheri katika mwaka 2013; uwe ni mwaka mwingine kwako ambao utaendeleza utashi wako na uwezo wako wa uandishi kwa faida ya Jamii ya Tanzania; KEEP IT UP;
kwa niaba ya Blogs za ukadirifu na mungupamojanasi tunakutakia kila la kheri katika mwaka 2013; uwe ni mwaka mwingine kwako ambao utaendeleza utashi wako na uwezo wako wa uandishi kwa faida ya Jamii ya Tanzania; KEEP IT UP;
No comments:
Post a Comment