Mahakama Kuu ya Zanzibar imetupa kesi waliyokuwa wamefungua viongozi wa Jumuiya ya Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu (Jumiki), maarufu kama “Uamsho”, wakipinga kunyimwa huduma wakiwa mahabusu katika Gereza la Kinua Miguu mjini Zanzibar.
Kesi hiyo namba 2 ya mwaka 2012 ilifunguliwa na Wakili Abdalla Juma Mohamed, kwa niaba ya wateja wake wanane, wakiwamo viongozi wa Uamsho dhidi ya Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar (DPP), Ibrahim Mzee Ibrahim, Novemba 8, mwaka huu.
Akisoma hukumu dhidi ya kesi hiyo jana, Jaji Mkusa Isack Sepetu, alisema kesi hiyo imefunguliwa kinyume cha kifungu cha 4 sura 28 cha Sheria ya Mawakili na Wanasheria ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).
Jaji Mkusa alisema nyaraka za kesi zimewasilishwa mahakamani kinyume cha sheria kutokana na kukosekana kwa jina la mtu aliyekula kiapo kwa niaba ya washitakiwa pamoja na kukosekana kwa tarehe katika hati ya kiapo.
Aidha, alisema hati ya kiapo imetayarishwa kimakosa kutokana na jina la mtayarishaji kutoambatanishwa katika hati ya kiapo kabla ya kufunguliwa kesi hiyo.
Jaji Mkusa alisema kwa kuwa hati za kiapo zilitayarishwa na wakili mzoefu kwa niaba ya washitakiwa, Abdallah Juma Mohammed, alitakiwa kuwa makini na kuhakikisha jina lake na tarehe vinazingatiwa katika hati ya kiapo kabla ya kufungua kesi mwaka huu.
“Kimsingi maombi hayo hayakukidhi matakwa ya kisheria na hayana nguvu za sheria kusikilizwa na Mahakama,” alisema Jaji Mkusa.
Jaji Mkusa aliwataka wahusika kuwa makini wanapowasilisha maombi kama hayo au nyaraka, ikiwamo kuangalia kama maombi yao yamekidhi matakwa ya kisheria.
Viongozi wa Uamsho walifungua kesi wakipinga kitendo cha uongozi wa Chuo cha Mafunzo Zanzibar (Magereza) kuwanyima fursa ya kula chakula kutoka nyumbani, kufanya ibada ya pamoja siku ya Ijumaa, kila mshitakiwa kufungiwa katika selo saa 24, kunyimwa haki ya kubadilisha nguo, kusoma vitabu vya Kur’an, kukutana na jamaa zao, pamoja na kuchaganyika katika selo.
Pia waliomba Mahakama Kuu Zanzibar kupitia upya uamuzi wa DPP wa kufunga dhamana ya washitakiwa hao kwa kutumia Kifungu cha 3 (d) sura ya 47 cha Sheria ya Usalama wa Taifa.
Kesi ya msingi inayowakabili viongozi hao wa Uamsho itatajwa tena Januari 3, mwakani.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment