Mzee alisema hayo jana, alipozungumza katika mdahalo wa kujadili
na kutafakari muundo huo wa Serikali, ulioandaliwa na Baraza la Habari Tanzania
(MCT) kwa lengo la kutoa elimu zaidi kwa waandishi wa habari, kuhusu umuhimu wa
Serikali ya aina hiyo na changamoto zake.
Pamoja na kutaka waandishi wa habari, kuitangaza vizuri Serikali hiyo,
kwa kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kuleta amani na utulivu nchini na
kuondosha siasa za chuki na uhasama, pia alitaja changamoto inazozikabili,
ikiwemo hiyo ya Muungano.
Akifafanua changamoto hiyo, alisema inatokana na tofauti ya sera
zinazotokana na vyama vya siasa katika kuongoza nchi, ikiwemo katika Muungano
ambapo sera ya CCM ni Muungano wa Serikali mbili wakati sera za CUF ni Muungano
wa Mkataba.
Alisema tofauti ya sera za vyama katika suala la Muungano,
linalokwenda sambamba na utoaji wa maoni ya wananchi katika marekebisho ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kiasi kikubwa limeanza kuzusha
malumbano na kutishia kuyumba kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa.
“Kumejitokeza suala la tofauti ya sera za vyama vya siasa kati ya CCM na CUF katika utoaji wa maoni ya marekebisho ya Katiba...limeanza kuzusha malumbano ambayo yanaweza kuyumbisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Mzee.
“Kumejitokeza suala la tofauti ya sera za vyama vya siasa kati ya CCM na CUF katika utoaji wa maoni ya marekebisho ya Katiba...limeanza kuzusha malumbano ambayo yanaweza kuyumbisha Serikali ya Umoja wa Kitaifa,” alisema Mzee.
Alisema pia lipo tatizo kwa baadhi ya watendaji wa Serikali,
kushindwa kuheshimu utendaji wa Serikali hiyo huku wengine wakiifananisha na
paa moja katika nyumba ambalo linaweza kuanguka wakati wowote.
Mzee ambaye amewahi kuwa Katibu wa Baraza la Wawakilishi, alisema
wakati umefika kwa baadhi ya taasisi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,
muundo wake uwe na sura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa huku akitoa mfano wa
Baraza la Wawakilishi.
“Pale katika Baraza la Wawakilishi, muundo wake una shaka...hakuna
sura ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sababu Spika anatoka katika Chama Cha
Mapinduzi pamoja na Naibu wake na watendaji wengine”, alisema.
Pamoja na changamoto hizo, Mzee alitaja mafanikio makubwa ya
Serikali hiyo, ambayo yanapaswa kutangazwa na vyombo vya habari, kuwa ni
kuimarika kwa utulivu wa nchi na washiriki wa maendeleo kurudisha misaada yao
katika nyanja mbalimbali.
Alisema zipo baadhi ya nchi za Bara la Afrika, zilizounda Serikali
ya Umoja wa Kitaifa, lakini zimeshindwa kupata mafanikio mazuri katika kipindi
kifupi, ikilinganishwa na Zanzibar, kwa kuwa viongozi wake wakuu wamekuwa
wakilumbana mara kwa mara.
“Serikali ya Umoja wa Kitaifa kwa sasa inafikia umri wa miaka
miwili tangu kuasisiwa kwake, lakini nawaomba waandishi wa habari waeleze
mafanikio yake kwa wananchi, ikiwemo kurudi kwa amani na kuondoka chuki na
siasa za uhasama,” alisisitiza.
Source: Lukwangule blog
No comments:
Post a Comment