Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF) vimeshutumiana vikali kuhusiana na kuvunjika kwa mikutano miwili ya kutoa maoni ya katiba Visiwani Zanzibar juzi.
CCM wamesema vurugu zinazotokea katika vituo vya kutoa maoni ya katiba zinaratibiwa na CUF na kutaka Tume ya Mabadiliko ya Katiba kuchukua hatua dhidi ya watu walioamua kuvunja sheria.
Tamko hilo lilitolewa jana na Katibu wa Kamati Maalum ya NEC Idara ya Itikadi na Uenezi ya CCM Zanzibar, Issa Haji Gavu, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar.
“Haya yanayofanyika sasa na kutokea ni matendo maovu, ni uhalifu na zaidi yakitaka kuturudisha tena katika zama nyeusi za mivutano, malumbano na kujenga upya uhasama,” alisema Gavu ambaye pia ni Naibu Waziri wa Miundombinu na Mawasiliano Zanzibar.
Alisema CUF imekuwa ikisafirisha wafuasi wake wanaotetea Muungano wa mkataba katika magari kwenda kutoa maoni katika maeneo wasiyoishi na kusababisha vurugu kati yao na wakazi halali katika maeneo hayo.
Gavu alisema watu wanaosafirishwa siyo wenye ulemavu wa viungo, lakini wanalazimika kusafirishwa kwa magari kwa kuwa ni wageni katika maeneo wanayokwenda kutoa maoni.
“Matukio haya kwa sehemu kubwa yana lengo la kuleta mmomonyoko wa kutovumiliana na kutostahamiliana kulikoanza kustawi na hivyo kujenga wasiwasi na hofu,” alisema Gavu.
Hata hivyo, alisema kwamba pamoja na wanachama wa CCM kuzomewa wanapotoa maoni kuhusu kuendelea kwa mfumo wa Muungano wa serikali mbili, CCM itaendelea kutetea mfumo huo kwa nguvu zake zote kwa vile ndiyo msingi wa ilani yake ya uchanguzi ya mwaka 2010-2015.
“Tunaamini kuwa maoni na mawazo ya kila mwananchi kwa ajili ya uundwaji wa katiba mpya ni sehemu ya utekelezaji wa misingi ya demokrasia na mtu yeyote hapaswi kuwekewa mipaka au ukomo wa kutoa mawazo yake,” alisema.
Alisema kuwa CUF imekuwa ikipandikiza watoa maoni mamluki ambao tayari wametoa maoni katika majimbo yao baada ya kuona wananchi wanaotaka mfumo wa Muungano wa serikali mbili ni wengi katika shehia mbalimbali.
“Ili uonekane bingwa, mwenye uchungu na Zanzibar, mzalendo wa kweli na mwana mageuzi makini, unalazimishwa utoe maoni yanayopendekeza mfumo mpya wa Muungano wa mkataba na hutakiwi utoe maoni ya serikali mbili, huu ni uvunjaji wa misingi ya demokrasia,” alisema Gavu.
CUF YAJIBU
Mkurugenzi wa Haki za Binadamu, Habari na Uenezi wa CUF, Salum Bimani, alikanusha chama hicho kuhusishwa na matukio ya vurugu hizo na kusisitiza kwamba zinafanywa na wabunge na wawakilishi wa CCM.
Alisema viongozi hao wamekuwa wakikusanya watu katika matawi ya CCM na kuwapeleka kutoa maoni ya Katiba kwa kutumia utaratibu maalum wa kupangwa mwanzo na kuwanyima haki watu wanaoonekana kuwa ni wafuasi wa vyama vya upinzani.
Aliwataka baadhi ya wabunge na wawakilishi wa CCM (majina tunayahifadhi) kuwa wamekuwa wakifanya kazi ya kupeleka watu kwenda kutoa maoni yanayoinga mkono ya Muungano wa serikali mbili.
Bimani alidai kuwa pamoja na Tume hiyo kuongozwa na wanasiasa wakongwe na watu wanaoheshimika katika jamii wakiwamo Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba; Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhan na Waziri Mkuu Mstaafu, Salim Ahmed Salim, lakini kazi imewashinda kutokana na majukumu ya tume kutekwa na viongozi wa CCM Zanzibar.
Alisema wananchi wamekuwa wakikusanywa na kupewa posho na kupikiwa pilau mambo ambayo yalitakiwa kukemewa na Tume na kuchukua hatua kali dhidi ya watu na viongozi wanaofanya vitendo hivyo.
KAULI YA WARIOBA
Kwa upande wake Warioba, alijibu madai ya Bimani na kusema kuwa vyama vya siasa vikae pembeni na kuwaacha wananchi watoe maoni yao bila kuingiliwa wala kushinikizwa.
Akizungumza na NIPASHE kwa njia ya simu jana, Jaji Warioba alisema wao wanafanya kazi ya kuchukua maoni ya wananchi na kwamba hawasikilizi vyama vya siasa vinasema nini.
“Sisi bado tunaendelea na kuchukua maoni ya wananchi ili waweze kupata katiba mpya na wala hatusikilizi na kuangalia vurugu za vyama vya siasa,” alisema na kuongeza: “Tunavitaka vikae pembeni na kuwaacha wananchi.”
Alisema mchakato wa kukusanya maoni unahusu wananchi na kwamba hawataki kufanyi kazi ya kulumbana na vyama vya siasa na kuacha kazi waliyopewa.
POLISI WAZUNGUMZA
Jeshi la Polisi Zanzibar limesema mabishano makali yaliyoibuka katika vituo vya kutoa maoni ya Katiba ndiyo chanzo cha mikutano miwili kuvunjika.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Unguja, alitoa kauli hiyo jana wakati akizungumzia vurugu za juzi zilizosababisha kuvunjika kwa mikutano miwili katika majimbo ya Mpendae na Magomeni.
Alisema mabishano hayo yamekuwa yakitokana na kundi moja la wananchi kulalamika kuwapo watu wanaojitokeza kutoa maoni wakati siyo wakazi halali katika maeneo ambayo mikutano hiyo inafanyika.
Hata hivyo, alisema jeshi hilo tayari limechukua hatua mbalimbali kuhakikisha tume hiyo inaendelea kutekeleza majukumu yake ikiwamo kuimarisha ulinzi.
Kamanda huyo alisema kuwa hadi jana hakuna mtu aliyekuwa amekamatwa.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment