Deo Filikunjombe
MBUNGE wa Ludewa, Deo Filikunjombe (CCM) amekipasha chama chake, kwamba kimewafanya Watanzania waamini kwamba rasilimali za nchi ni mali ya chama hicho, jambo ambalo siyo sahihi.
Filikunjombe alitoa kauli hiyo Dar es Salaam jana jijini Dar es Salaam wakati wa kongamano lililoandaliwa na Kikundi cha Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDASA).
Alisema kwamba, kuna mitazamo imejengeka kwa wana CCM walio wengi, kwamba Watanzania wote ni mali ya CCM.
“Sisi wana CCM hasa wale ambao tumepewa ridhaa na wananchi kuwatumikia, tunapaswa kutambua kwamba Tanzania siyo mali yetu, hivyo jambo la muhimu la kufanya ni kutumia nafasi zetu kuwaongoza na kuwaletea maendeleo kwa kutumia rasilimali za nchi. Kwa mfano, hawa maprofesa wa chuo kikuu wana nafasi kubwa katika kulijenga taifa na kuandaa kizazi chenye elimu lakini utashangaa kuona wasomi ndiyo wanaalikwa kwenye harusi na kuchangia mamilioni lakini kwenye sekta ya elimu hawahudhurii. Leo kila mtanzania akiamua kuchangia Sh 24,000 ni dhahiri wanafunzi wa vyuo vikuu vyote nchini watasoma bure, hivyo tuungane tuijenge Tanzania,”alisema Filikunjombe.
Pamoja na hayo, alisema kutokana na Watanzania kuongozwa na CCM kwa muda mrefu pamoja na mfumo ulivyo wa kiutawala, wananchi wanaamini kila kitu ni mali ya CCM.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, January Makamba, alisema suala la Tanzania kuongozawa na rais kijana haliepukiki kwa sababu vijana wana uwezo wa kushika wadhifa huo.
Kutokana na hali hiyo, alisema litakua ni jambo la busara kama rais ajae, mwaka 2015 atakuwa ni kijana.
Hata hivyo, Mjumbe wa Tume ya Katiba mpya, Joseph Butiku, alipinga hoja hiyo na kusema suala la urais haliendani na umri bali uwezo wa anayeongoza.
Kutokana na hali hiyo, aliwataka vijana wafanya kazi kwa bidii ili ukifika wakati wa kumchagua rais, wawe na kitu cha kuzungumza badala ya kuendeleza maneno yasiyokuwa na masingi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Julius Mtatiro, alisema CCM imeshindwa kubadilisha maisha ya Watanzania katika kipindi cha miaka 51 na kwamba umefika wakati chama hicho kiondoke madarakani bila kuondolewa na wananchi.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alisema Tanzania ilipofikia inatakiwa kuwa na viongozi wenye mipango dhabiti ya kutatua umasikini na kuleta ajira kwa vijana.
“Ni kweli Tanzania ni masikini na baada ya miaka 13 Watanzania watafikia milioni 65 na baada ya miaka 50 watafikia milioni 100. Kwa idadi hiyo, taifa bado lina changamoto kubwa sana ya kujiuliza ni jinsi gani ya kutatua na kuleta maendeleo na jambo la muhimu ni kufanya ufafiti wa kimaendeleo. Bila kuwapata viongozi wenye dhamira njema na rasilimali za nchi, tutaendelea kulalamika kila mwaka lakini tukiwekeza kwenye umeme hakika ajira itapatikana,” alisema Membe.
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment