WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Thursday, December 6, 2012

Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Maoni


 Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Alabama, Michenzani Mjini Zanzibar
 Wafuasi na wapenzi wa CUF wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Chama hicho Maalim Seif Sharif Hamad wakati akiwahutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Alabama, Michenzani Mjini Zanzibar.
 Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu wa CUF, Salum Bimani akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Alabama, Michenzani Mjini Zanzibar.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad akiwahutubia wafuasi na wapenzi wa Chama hicho katika mkutano wa hadhara uliofanyika viwanja vya Alabama, Michenzani Mjini Zanzibar. (Picha na Salmin Said, OMKR)


ZANZIBAR                                         06/12/2012.
KATIBU Mkuu wa Chama cha Wananchi CUF, Maalim Seif Sharif Hamad ametoa wito kwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuratibu Maoni ya Wananchi juu ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Sinde Warioba na tume yake kuweka bayana muundo wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya yatakayo jadili maoni ya wananchi, ili kuepusha Mabaraza hayo kutawaliwa na wajumbe wa chama kimoja.
Maalim Seif alisema hayo jana huko katika viwanja vya Alabama Michenzani, wakati alipokuwa akihutubia mkutano wa hadhara ulioandaliwa na chama hicho, ikiwa ni siku moja kabla ya Tume hiyo ya kuratibu maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba kuanza kazi hiyo katika Wilaya ya Mjini hii leo tarehe 06/12/2012.

Maalim Seif ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alisema baada ya hatua hiyo ya kuchukua maoni ya wananchi kukamilika, tume itarudi ofisini kuyajadili na baadaye yataundwa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya ambayo pia yataweza kujadili maoni hayo ya wananchi, kabla ya kuchukuliwa hatua nyengine.

Alisema kuwa lazima kuwe na uwazi na wananchi waelezwe Mabaraza hayo yataundwa na wajumbe wepi, ili kuondoa dhana mbaya inayoweza kujengwa na wananchi kuwa wajumbe hao watatoka katika chama kimoja cha siasa.
Alisema dhana kama hiyo ikijengeka inaweza kusababisha dosari katika mchakato mzima wa mabadiliko ya Katiba, hivyo tume hiyo ichukue hatua za makusudi kulitolea ufafanuzi suala hilo.  

“Mheshimiwa Warioba lazima muwe wawazi, hadi sasa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya hapana anayejua muundo wake, vyenginevyo unaweza ukakuta wajumbe wote wanatoka katika chama kimoja”, alishauri Maalim Seif. 

Aidha, Maalim Seif alisema uwazi pia unahitajika wakati wa kuundwa kwa Bunge la Katiba, ambapo mbali ya Wabunge wote na Wawakilishi wote kuwa wajumbe kuna wajumbe wengine 164, ambao watateuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano kwa ushirikiano na Rais wa Zanzibar, lakini hadi sasa utaratibu gani utatumiwa kuwapata wajumbe hao haufahamiki. 

Alisema ili kujenga imani kwa wananchi na kuepusha dhana mbaya itahitajika uadilifu mkubwa kwa Rais, hasa kwa wale watakaotoka Zanzibar basi kuna haja wawe angalau 55, na vile vile wasitoke katika chama kimoja cha siasa.

Aidha, Maalim Seif alisema hata katika suala la kura ya maoni itakayokuja kufuatia huko mbele, bado kuna masuala mengine ya kujiuliza, kuhusu utaratiubu upi utatumika, wakati wa kura hiyo kwa Wazanzibari wanaoishi Tanzania Bara na watu wa Tanzania Bara wanaoishi Zanzibar.
Alieleza kuwa hofu hiyo inakuja kwa vile sheria ya mabadilikko ya katiba inasema mabadiliko hayo yatapitishwa, iwapo angalau nusu ya wananchi wa kila upande kati ya Tanzania Bara na Zanzibar wataunga mkono mabadiliko hayo, hivyo amehimiza mambo hayo lazima kwanza yawekwe wazi.

Kuhusu maoni ya wananchi juu ya mabadiliko ya Katiba, Maalim Seif ametowa wito kwa Wazanzibari kutoa maoni ambayo yatazingatia zaidi maslahi ya Zanzibar, na kusema kuwa mfumo wa Muungano wa serikali mbili uliopo sasa kamwe hauwezi kuleta ufumbuzi wa matatizo ndani ya Muungano yaliyodumu tokea Muungano huo ulipoanzishwa.

Aidha aliwafahamisha wananchi hao kuondokana na dhana ya serikali mbili kwani haina maslahi ya nchi kwani hata rais wa Zanzibar huwa anabezwa katika kufanya baadhi ya maamuzi kwa nchi yake.

“Mimi sina haja ya kuficha wala kutafuna maneno, mimi ni muumini wa Muungano wa Mkataba, maana ni imani yangu kuwa muundo wa Muungano huu tuliuonao hauwezi kuondoa kasoro zilizopo hadi kiama”, alisema Katibu Mkuu wa CUF.    
Alitoa wito kwa wananchi katika Wilaya ya Mjini kujitokeza kwa wingi kwenda kutoa maoni kuanzia leo, na wasikubali kudanganywa na baadhi ya watu wanaotoa fedha kuwarubuni wakatoe maoni, kama wanavyowaelekeza wao.
Mapema, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Umma na Haki za Binaadamu wa CUF, Salum Bimani aliwataka Wazanzibari kuweka mbele maslahi ya Zanzibar katika zoezi la kutoa maoni ya katiba na kuweka kando itikadi zao za vyama vya siasa.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar Hamad Massoud Hamad, kwa upande wake amesema Chama hicho kimezidi kuimarika kuliko wakati wowote tangu kuanzishwa kwake, na kuwaomba wananchi waendelee kukiunga mkono ili kutimiza malengo yake ya kutetea maslahi ya Zanzibar ndani na nje ya nchi.

Hassan Hamad (OMKR).

No comments:

Post a Comment