WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Monday, December 3, 2012

Aeshi sasa ruksa kukata rufani



ALIYEKUWA Mbunge wa Sumbawanga mjini, Aeshi Hillary aliyevuliwa wadhifa huo na Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, amepata tumaini jipya baada ya mahakama hiyo kumruhusiwa kukata rufani kwa mara nyingine.
Hillaly, aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),  alivuliwa wadhifa huo na aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga, Bethuel Mmila April 30, 2012, kufuatia kesi iliyofunguliwa na Nobert Yamsebo.
Baada ya kuvuliwa wadhifa huo, Hillary alikata rufaa Mahakama ya Rufani akipinga hukumu ya Mahakama Kuu Sumbawanga kumvua wadhifa huo, lakini Oktoba 18, 2012, Mahakama ya Rufani ilitupilia mbali rufaa hiyo.
Hata hivyo, Mahakama Kuu Kanda ya Sumbawanga imempa nafasi tena ya kukata rufaa, baada ya kuwasilisha maombi ya kuongezewa muda wa kuwasilisha kusudio la kukata rufaa upya, kupitia kwa Wakili wake, Richard Rweyongeza.
Wakili Rweyongeza alisema kuwa uamuzi huo ulitolewa na  Jaji Lawrence Kaduri Alhamisi iliyopita, na kwamba wamepewa siku 14 kuwasilisha taarifa ya kusudio la kukata rufaa.
Wakili Rweyongeza aliongeza kuwa, kwa mujibu wa uamuzi huo,  wanatakiwa  kukata rufaa ndani ya siku 60 baada kufanya marekebisho ya dosari zilizobainika katika rufaa ya kwanza.
Rufaa ya awali ya Hilaly,  ilitupiliwa mbali na mahakama hiyo katika uamuzi uliotolewa na Jopo la Majaji watatu, Januari Msofe, Edward Rutakangwa, na Engela Kileo, baada ya kubaini kasoro za kisheria.
Kasoro hiyo ni kutokuwepo kwa mwenendo wa maombi ya mlalamikaji katika kesi ya msingi, ya kuomba mahakama impangie kiwango cha pesa ambacho alipaswa kulipa kama amana ya kufungua kesi hiyo, kwa wa kifungu cha 111 (3) cha Sheria hiyo ya Uchaguzi ya mwaka 2010.
Kwa mujibu wa kifungu hicho, Mahakama  ilisema kwamba mtu anayefungua kesi ya uchaguzi ni lazima awasilishe maombi ili mahakama impangie kiwango cha, amana anachopaswa kulipa ndani ya siku 14 tangu kufungua kesi.
Pia kifungu hicho kinaelekeza kwamba ndani ya siku 14 nyingine tangu siku ya maombi hayo, mahakama hiyo iwe imeshapanga kiwango hicho.
Mahakama hiyo ilisema kuwa ni muhimu wa mwenendo huo ni kuipa nafasi mahakama kuona kama maombi yaliwasilishwa ndani ya muda baada ya kesi kufunguliwa na pili ni kuona kama maombi hayo yaliamuliwa ndani ya muda tangu kuwasilishwa.
Mahakama hiyo ilisema kuwa, kwa mujibu wa Kanuni ya 96 (1) na (3) za Kanuni za Mahakama ya Rufani, si jukumu la upande katika kesi kuamua kuwa nyaraka fulani ni muhimu au si muhimu katika rufaa, kama wakili wa Hilaly, Rweyongeza alivyodai.
"Kutokuwepo kwa nyaraka hizo, rufaa haina nguvu chini ya Kanuni ya 96 (1) (k) ya Kanuni za Mahakama ya Rufani, hivyo rufaa inatupiliwa mbali."
Katika kesi ya msingi namba 01 ya mwaka 2010, Yamsebo aliyekuwa mgombea wa ubunge katika jimbo hilo kupitia Chadema,  alikuwa akipinga matokeo yaliyompa ushindi wa Hilaly  kwa kupata kura 17,328,  huku Yamsebo akipata 17,132.
Alikuwa akidai kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa Katiba na Sheria ya Uchaguzi na hivyo kusababisha uchaguzi huo kutofanyika kwa haki na uhuru, huku pia akimtuhumu Hillaly  na wafuasi wake kutoa rushwa kwa wapiga kura mbalimbali ili wamchague.
Katika uamuzi wake, Mahakama Kuu ilikubaliana na baadhi ya hoja zilizotolewa na mlalamikaji na hatimaye kutengua ushindi wa Hilaly.
Akisoma hukumu hiyo, Jaji Mfawidhi Betweli Mmila wa alisema: “Baada ya kupitia hoja zote, nashawishika kusema kuwa uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa si wa haki na huru.”
Jaji Mmila alieleza kuridhika kuwa kulikuwapo na mazingira ya rushwa na kutokuwapo kwa mazingira huru katika kampeni kwa baadhi ya maeneo.
Sababu nyingine alisema kuwa ni kukosekana mazingira huru katika kampeni kwenye vijiji vya Mtimbwa na Kisumba ambako mgombea wa Chadema alizuiwa na baadhi ya wakazi wa eneo hilo kufanya kampeni zake.
Hata hivyo, Mei 28, 2012, Hilaly alikata rufaa namba 55 ya mwaka 2012, dhidi ya Yasemsebo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG)Justus Kalama na Vitus Kapufi, akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu.
Kutokana na rufaa hiyo dhidi yake, Yamsebo kupitia kwa Wakili wake, Victor Mkumbe, aliweka pingamizi la awali (PO)pamoja na mambo mengine akidai kuwa Hilaly hakuwa amelipia ada ya kufungua rufaa hiyo ya Sh2000.
Kabla ya kuanza kusikiliza pingamizi la Yamsebo dhidi ya rufaa ya Hilaly, mahakama hiyo ilibaini kutokuwapo mwenendo huo wa maombi ya Yamsebo kupangiwa gharama za kufungulia kesi hiyo ya msingi, ndipo ikaamua kutupilia mbali rufaa hiyo.
Mwananchi

No comments:

Post a Comment