Na Mwandishi wa TANZANIA DAIMA
KAMATI Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), imemaliza
kikao chake cha siku mbili jijini Dar es Salaam, na kuazimia kuanza
Operesheni ya Vuguvugu la Mabadiliko (M4C) kwa ajili ya kumshinikiza
Rais Jakaya Kikwete, atekeleze madai yao.
Katika kikao hicho, mbali na ajenda nyingine, wajumbe walipokea na kujadili taarifa ya utekelezaji kutokana na maazimio ya kikao cha dharura kilichokutana Septemba 9, mwaka huu.
Miongoni mwa maazimio hayo, ilikuwa na kupata majibu ya utekelezaji
wa madai yao katika barua rasmi waliyomwandikia Rais Kikwete kupitia kwa
Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Baadhi ya masuala hayo ambayo yaliazimiwa ni kuwataka Waziri wa Mambo
ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta
Jenerali wa Polisi Said Mwema, Mkuu wa Operesheni wa Jeshi la Polisi,
Kamishna Paul Chagonja, na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine
Shilogile wawajibike kwa kujiuzulu nafasi zao au wafukuzwe kazi.
Kwamba kwa kuzingatia kuwa, mauaji kadhaa yalitokea mikononi mwa
Jeshi la Polisi, vile vile waliazimia kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Iringa, Michael Kamuhanda, Mkuu wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia Mkoa wa
Morogoro na askari waliosababisha mauaji ya raia wasio na hatia Morogoro
na Iringa wafikishwe mahakamani kujibu mashtaka ya mauaji.
Chanzo chetu cha siri kutoka ndani ya kikao hicho, kilieleza kuwa
wajumbe walielezwa kuwa rais amesema kuwa ataifanyia kazi barua hiyo, na
hivyo CHADEMA katika kutilia mkazo, waliazimia kufanya operesheni hiyo
kama shinikizo.
“Kwa hiyo kuanzia Januari mwakani, M4C itaanza rasmi ili kumshinikiza
Rais Kikwete atekeleze matakwa ya barua yetu kwa kuwaondoa viongozi hao
waliosababisha vifo vya raia wasio na hatia.
Rais Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM),
hivi karibuni waliwaonya viongozi wa chama chake kuacha kutegemea nguvu
ya Jeshi la Polisi katika kukabiliana na hoja za wapinzani.
Alisema kuwa, hoja za kisiasa zinajibiwa kisiasa, lakini akaeleza
kushangazwa na hatua ya viongozi wa CCM kukimbilia kuomba nguvu ya
polisi wakati wapinzani wanapoibua tuhuma dhidi ya chama hicho.
Kikao hicho cha siku mbili, mbali na kupokea taarifa hiyo kuhusu Rais
Kikwete, pia kilijadili ajenda tatu ambao ni taarifa ya hali ya siasa
nchini, mchakato wa mabadiliko ya katiba ya nchi na operesheni ya M4C.
Viongozi wakuu wa CHADEMA wamekuwa wakimkumbusha Rais Kikwete kujibu
barua yao na kuwachukulia hatua wahusika ili kuondoa hofu ambayo
imetawala kwa umma kuhusu mauaji ya raia yanayozidi kujitokeza.
Katika barua hiyo kwa Rais Kikwete, walitoa wito wakimtaka aunde tume
huru ya kiuchunguzi ya kimahakama (Judiciary Commission of Inquiry)
kuchunguza vifo vilivyotokea katika mazingira tata katika mikoa ya
Arusha, Tabora, Singida, Morogoro na Iringa.
No comments:
Post a Comment