Kwa wale wanaodai serikali tatu ni jibu la matatizo ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar wamekosea sana kwani Serikali tatu ni gharama kubwa zaidi na umasikini utazidi kuimarika ndani ya pande zote mbili za muungano pale sehemu kubwa ya pato la taifa ikizidi kuishia kugharamia serikali tatu kubwa zaidi badala ya maendeleo ya kiuchumi na wawekezaji kuendelea kutukwepa kutokana na hilo.
Zanzibar tayari inaumia sana kiuchumi kutokana na huu muungano kwani ingekuwa kisiwa chenye dola yake kamili na tulivu ingeweza kuwa kivutio kikubwa zaidi kwa wawekezaji wa kimataifa kuliko hata Mauritius ambayo iko mbali zaidi na masoko ya Africa kusini mwa jangwa la Sahara. Wawekezaji wengi hupendelea zaidi vile visiwa vidogo vidogo vyenye dola kamili jirani na masoko makubwa na vianzio vya mali ghafi kibara.
Kasoro mbaya zaidi ndani ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar zitajitokeza wakati wagombea wa Urais katika ngazi ya muungano watakuwa mmoja Mkristu na mwingine Muisilamu ambapo karibu Wazanzibari wote watajitokeza kumpigia kura ya ndiyo mgombea Muisilamu na kumkataa mgombea Mkristu bila kuzingatia ni nani bora zaidi kwa nafasi hiyo ya urais. Kitakachojitokeza ni muungano utakaokuwa ukitujengea hisia za udini na hujuma ya demokrasia ndani ya jumuia ya watu waliounganishwa kisiasa.
Kwa vile muungano haujawahi kuwa chaguo la raia wa pande mbili ndani ya muungano, basi ni vizuri ukaachika kimya kimya tuone kama raia wataulilia. Bila muungano mahusiano ya aina zote kati ya raia wa Zanzibar na Tanganyika yataboreka zaidi.
Tuachane na huu muungano wa Kisiasa kama njia mojawapo ya kuheshimu matengano Mungu aliyotuwekea kwa njia maji ya bahari kati ya Zanzibar na Tanganyika ili Wazanzibari na Watanganyika waweze kuendeleza ushirikiano endelevu uliojengeka kwa misingi ya kibiashara na sio misingi ya kisiasa iliyoboreshwa na udini.
Cha kutafakari ni namna ya kuboresha uhusiano na ushirikiano na sio muungano baina ya watu wa Zanzibar na wale wa Tanganyika.
Inabidi pia kuzingatia kwamba pale inapojitokeza kwamba watu ndani ya dola hii karibu wote ni Wakristu au Waisilamu na ndani ya dola ile ni mchanganyiko wa Waisilamu na Wakristu basi uhusiano na ushirikiano endelevu baina ya dola hizo mbili ni ule uliojengeka kwa misingi ya kibiashara kati dola hizo mbili huru badala ya ule uliojengeka kwa misingi ya muungano wa kisiasa kati ya dola hizo mbili. Hii ni mojawapo ya zile njia muhimu sana kuzingatia pale inapotakiwa kuepusha na kupunguza chuki zitokanazo na udini ili kuboresha mahusiano na mashirikiano miongoni mwa jamii zilizotofautiana kidini.
Dk. Antipas Massawe - massaweantipas@hotmail.com
Source: http://www.wavuti.com
No comments:
Post a Comment