Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Rais Jakaya Mrisho Kikwete (wa pili kushoto) Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein (kushoto), Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Davis Mwamunyange,Makamu wa Rais Dk Mohammed Gharib Bilal, Wakiwa makini wakati wimbo wa Taifa ulipokuwa ukiimbwa kwenye uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya miaka 51 ya uhuru jana.Picha na Salhim Shao
RAIS Jakaya Kikwete amesema wenye hila na chuki pekee ndiyo wanaosema kuwa Tanzania hakuna maendeleo.
Alisema hayo jana alipolihutubia Taifa kwenye maadhimisho ya miaka 51 ya Uhuru wa Tanzania yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
“Utaratibu uliopo ni kuzungumza kila baada ya miaka mitano, lakini mwaka huu ninazungumza na wananchi kutokana na kuwapo kwa viongozi wa mataifa ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc). Nataka wasikie mafanikio yetu ya miaka 51 ya Uhuru,” alisema Rais Kikwete.
Viongozi walioshiriki maadhimisho hayo ni marais Armando Guebuza wa Msumbiji, Joseph Kabila wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo (DRC) na Hifikepunye Pohamba wa Namibia.
Nchi zilizotuma wawakilishi katika sherehe hizo zilizohudhuriwa na umati wa watu ni Lesotho, Zambia, Angola, Swaziland, Shelisheli, Rwanda, Zimbabwe, Mauritius na Malawi.
Rais Kikwete alisema mwenye macho hawezi kusema lolote, lakini kwa mwenye hila hakosi maneno na kutoa dosari kwa maendeleo yaliyofikiwa.
“Watu waliobahatika kuiona Tanzania ya mwaka 1961 wakija sasa hivi, wataona mabadiliko makubwa. Kuna mabadiliko makubwa na hii inatokana na kuboresha nyanja mbalimbali za kiuchumi, ulinzi na usalama na miundombinu... kwa wenye hila hawakosi la kusema ila mwenye macho haambiwi tazama,” alisema.
Aliwashukuru viongozi walioshiriki mkutano SADC… “Tumepata bahati ya uwepo wa viongozi waandamizi wa SADC baada ya kukubali ombi langu la kuhudhuria sherehe hizi japo wengine wametoa udhuru na kutuma wawakilishi,” alisema.
Viongozi mashuhuri wakosekana
Baadhi ya viongozi wa kitaifa wakiwamo wastaafu, hawakuwamo katika sherehe hizo.
Miongoni mwa viongozi hao ni pamoja na mtangulizi wa Kikwete, Benjamin Mkapa ambaye yuko Lushoto mkoani Tanga.
Wengine ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Idd ambao hata hivyo, haikuelezwa sababu za kukosekana kwao.
Wanasiasa walonga
Baadhi ya wanasiasa walioshiriki kwenye maadhimisho hayo walisema licha ya Tanzania kupata Uhuru mwaka 1961, taifa bado linakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwamo ubora wa elimu.
“Ni miaka 51 sasa tangu tupate uhuru, lakini bado kuna tatizo la utoaji wa elimu bora kwa wananchi. Serikali inapaswa kujipanga kuboresha sekta ya elimu,” alisema Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, James Mbatia.
Alisema elimu iliyopo ni duni na haikidhi viwango ikilinganishwa na kipindi cha uhuru, kutokana na hali hiyo wanapaswa kuandaa mkakati madhubuti ili kuhakikisha kuwa mafanikio yanaendana na elimu bora.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Democratic Alliance (Tadea), John Chipaka alisema uwepo wa viongozi wa SADC umefanya maadhimisho hayo kuwa makubwa, jambo linaloweza kuifanya Serikali ionekane inawajibika kwa wananchi wake.
Maadhimisho hayo yalipambwa kwa gwaride maalumu lililoandaliwa na vikosi vya ulinzi na usalama likiongozwa na Luteni Kanali Omary Londo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ).
Rais asamehe wafungwa
Katika kuadhimisha miaka 51 ya Uhuru, Rais Kikwete amewaachia huru wafungwa 3,814 waliokuwa magerezani kwa makosa mbalimbali.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi alisema Rais ametumia madaraka chini ya Ibara ya 45 (1) (d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Alisema wafungwa watakaofaidika na msamaha huo ni wale waliotumikia kifungo kisichozidi miaka mitano ambao hadi siku ya msamaha ambayo ni jana watakuwa wametumikia robo ya vifungo vyao.
Wengine ni wafungwa wanaougua Ukimwi, kifua kikuu na saratani na ambao wako katika hali mbaya baada ya kuthibitishwa na madaktari.
Pia msamaha huo utawahusu wafungwa wazee wenye umri wa miaka 70, wanawake walioingia gerezani wakiwa wajawazito, wenye watoto wanaonyonya na wasionyonya pamoja na wenye ulemavu wa mwili na akili.
Taarifa hiyo ilisema msamaha huo hautawahusu wafungwa waliohukumiwa kunyongwa na au kifungo cha maisha.
Pia hautawahusu wenye makosa ya kujihusisha na dawa za kulevya, kupokea na kutoa rushwa na makosa ya unyang’anyi wa kutumia silaha.
Wengine ni wafungwa waliopatikana na silaha au risasi, wenye makosa ya kunajisi, kubaka na kulawiti, wizi wa magari kwa kutumia silaha na waliowapa mimba wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
Wengine waliokosa msamaha huo ni wezi wa miundombinu kama vile nyaya za simu na umeme, mafuta ya transfoma na wafungwa wazoefu ambao wanatumikia kifungo cha pili na kuendelea.
Wengine ni wale waliowahi kupunguziwa kifungo kwa msamaha wa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.
“Wengine ambao hawahusiki na msamaha huo ni wafungwa waliowahi kutoroka wakiwa chini ya ulinzi ambao bado wanaendelea kutumikia vifungo vyao,” alisema Waziri Nchimbi katika taarifa yake.
Taarifa hiyo pia ilisema wafungwa waliohukumiwa kifungo cha makosa ya kutumia vibaya madaraka yao na wale waliozuia watoto kupata masomo hawatahusika na msamaha huo.
Mwananchi
No comments:
Post a Comment