Matokeo ya uchaguzi wa Urais nchini Korea Kusini ambayo yametangazwa na Televisheni ya taifa ya nchi hiyo yameonesha Taifa hilo limefanikiwa kwa mara ya kwanza kumchagua Rais mwanamke ambaye ni Park Guen-Hye.
Guen-Hye amefanikiwa kumuangusha mpinzani wake kwenye kinyang'anyiro hicho Moon Jae-In kwa kupata asilimia hamsini na mbili nukta tano ya kura zote huku mshindani wake akiambulia asilimia arobaini na saba nukta moja.
Matokeo hayo yamekuja saa tatu baada ya zoezi la kupigakura kufungwa ambapo Vituo vya Televisheni vya KBS, SBS na MBC vimetangaza ushindi huo ambao ni wa kihistoria katika Taifa hilo.
Guen-Hye Rais huyo kwanza mwanamke katika Taifa hilo ataapishwa rasmi tarehe 25 mwezi februari mwakani.
Rais Geun-Hye ameahidi kuunda sera madhubuti juu ya usalama wa nchi hiyo wakati huu akitafuta kuwa na mahusiano mazuri na Korea kaskazini.
Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu kunyakua ushindi wa kihistoria nchini humo, Park amesema kuwa jaribio la roketi la hivi karibuni lililofanywa na Korea Kaskazini limelenga kutoa vitisho kwa adui zake hali inayodhihirisha kuwa hali ya usalama wa Korea kusini ni tete.
Kufuatia ushindi wa mwanamama huyo wachambuzi wa siasa wanaona kuwa ni hatua mpya katika siasa za Korea Kusini ambapo huenda ikabadili mwelekeo wa siasa za Korea kusini na kuwahusisha zaidi wanawake katika masuala ya uongozi.
Kwa upande mwingine wachambuzi wanaona kuwa mwanamke huyu atakabiliwa na changamoto kubwa ya kufumua mfumo dume wa uongozi uliokuwepo na kuleta mfumo utakaohusisha jinsi zote kwa manufaa ya taifa hilo.
No comments:
Post a Comment