Tunapowahubiria injili wenye njaa
Chifu Thomas Marealle (Juni 12, 1915 – Februari 14, 2007) Mangi Mkuu wa huko Uchaggani wakati fulani mwaka 1957 alipata kusema, "Huwezi kuhubiri injili kwa watu wenye njaa".
Kwa hizi siku mbili nimesoma mtandaoni watu wengi wakiwaponda wanafunzi wa UDSM wanaosemekana kufanya vitendo vya ngono ili waweze kujikimu kimaisha kutokana na ugumu wa maisha unaosababishwa na ukosefu wa mikopo kwa wakati ama kukosa kabisa.
Badala ya kuwaponda, ninadhani ingependeza tungewaambia wanafunzi hawa wafanye nini ili waweze kujikimu maisha nje ya utegemezi wa pesa za serikali (inawezekana siyo zao).
Sijui nani anayeweza kusema kwa maisha ya hapa Dar es Salaama utaweza kuishi vipi pasipo pesa? Natamani awepo mtu awaambie dada zetu na watoto wa ndugu zetu wafanye nini ili waweze kumudu kusoma na kutafuta pesa kwa njia bora zaidi.
Sikusudii kuwatetea wanafunzi hao. Lakini nakusudia kuziambia mamlaka zinazohusika zinapaswa kuguswa na uzembe (neno baya? basi niseme kutojali kwake) unaopelekea wanafunzi hao kutafuta mabadala wa namna ya kujikimu.
Ni aibu kubwa sana. Sitaki kusema ni aibu kwa wanafunzi hao. Bali nataka kusema ni aibu kwa taifa ambalo baada ya muda mfupi litakuwa na viongozi waliosoma kwa biashara ya ngono. Viongozi watakaosimama kwenye majukwaa na kuiambia jamii juu ya maadili na tabia zenye kupendeza.
Taifa hilo litakuwa ni zao la taifa lisilojali. Litakuwa ni zao la taifa lililoshindwa kufahamu vipaumbele vyake vya msingi ni nini. Litakuwa taifa la kipekee sana. Litakuwa ni taifa lililotokana na taifa lililoona serikali haina fedha za kutosha kutatua matatizo ya wanafunzi ilhali taifa hilo hilo lilikuwa na pesa za magari ya anasa na posho za kufuru kwa walioshika mipini.
Sitamani kuyasema haya. Lakini nisichokitamani zaidi, ni kuwa mnafiki.
Ukiyatazama maisha ya wanafunzi wengi wa elimu ya juu, utasikitika sana. Lakini jamii hailioni hilo kama tatizo. Tatizo kubwa linaloonekana ni wanafunzi kuishi maisha ya anasa na kujaza music systems vyumbani mwao (huu mjadala ulisumbua sana kwenye gazeti la Rais mwaka 2005 na 2006). Tunasahau (ama tunajua ukweli ila tunauficha) kuwa wanaoishi maisha ya anasa ni wachache katika wengi wa wanafunzi wa elimu ya juu. Kuna wachache wanaotoka familia zenye uwezo, wachache wenye ajira zao, na wachache wenye biashara zao.
Lakini sehemu kubwa ya wanafunzi wa elimu ya juu ni watoto wa Watanzania masikini kabisa. Tena wengi wao wamekuja mjini kwa sababu ya elimu tu. Hawa ni Watanzania ambao wakikosa fedha kutoka serikalini, maisha yao hayaelezeki.
Hawa ni Watanzania wanaolazimika kukomunika (kushindia chai na mkate), ambavyo pia vina gharama zake. Hata hiyo akiba kidogo inapomalizika, nini kinategemewa?
Mimi nadhani, badala ya kuandika mitandaoni na pahala pengine tukizilaani tabia za wanafunzi hawa, tungekumbuka kuziamsha mamlaka zinazohusika ziyatazame mambo haya kwa kina kwa macho yote na kuchukuwa hatua stahiki katika kutatua matatizo ya wanafunzi hawa.
Wizara ya Elimu na idara za serikali hususani Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu amkeni jamani.
Nirudie kuazima maneno ya Mangi Mkuu Marealle kuwa hatuwezi kuhubiri injili kwa watu wenye njaa.
Ahsanteni kwa kunisoma.
Fadhy Mtanga,
Kijitonyama, Dar es Salaam.
Mei 25, 2012.
No comments:
Post a Comment