Na Josephat Isango
Vita dhidi ya ufisadi ndani ya CCM sasa vimekwisha. CCM wamehama vita vya jukwaani wamekuja magazetini na mitandaoni, vita imewashinda wamefikia tamati. Iwe wanachama wanakubali au hawakubali, lakini sasa vita hivi vimekosa kiongozi, vita dhidi ya ufisadi vimekosa kamanda, vimekosa mtu anayeweza kuwaambia wenzake twendeni huku, tusiende huku, tujipange hivi, tusiseme hivi, tuamue hivi tukatekeleze hivi. Vita dhidi ya ufisadi au rushwa ndani ya CCM sasa imefika Tamati, atakayesikiliza wimbo mpya wenye maneno yale yale anadanganywa.
Chama chenyewe sasa, kimezama topeni, kinahitaji kutolewa. Kimetumbukia Shimoni, maji yamefika shingoni kwa watu wote wanaoelewa. Kwa sasa inahitajika mikutano michache sana ya wanasiasa wengine kuelezea hili na hili likieleweka, CCM hawatachungulia nje. Mikutano watafanya wapi na kama kwenye mikutano wakiulizwa maswali na kujibu basi kweli CCM itafufuka.
Lakini Wachunguzi wa mambo, wanasema kuwa kwa sasa, kushiriki harakati zozote za "kuhuisha CCM", sera mpya iliyotangazwa, ni sawa na kumkuta fisi aliyenyeshewa mvua ukamwotesha moto, akipata nguvu atakujeruhi. Ni sawa na kumtoa simba kwenye mtego alionasa. Je mtanzania yupi, anayeishi maisha magumu, anayechoshwa na michango, anayechoshwa na wizi wa mali ya umma, anyechoshwa kwa kukosa huduma za jamii ambaye yupo tayari kushiriki juhudi za kuhuisha CCM? Ni wale tu wanaonufaika na mfumo kandamizi, wanaokaa tabaka la wenye navyo, au wengine wasiojua ambao bado wanatumika kusaidia wezi.
Mchawi wa CCM ni CCM wenyewe. Wamejiponza kwa sababu ya Ujinga wao wa kutokujua mambo. Kutokana na ujinga huo, CCM imeponzwa na tabia ya Uropokaji. Hawajui kuwa tamko lina gharama. Kauli zao zinazidisha maswali kwa wananchi kuliko majibu.
CCM bila kutafakari waliwaletea watanzania dhana ya kukipatia chama chao sura mpya ndiyo iliyopewa jina la kujivua gamba na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya Taifa imekwishatengeneza mpango wa utekelezaji wa uamuzi huo.
Mpaka Makala hii inasomwa, tangu azimio hilo kupitishwa, hakuna mtu aliyechukuliwa hatua.
ilifika wakati, Katibu Mkuu wa wakati ule akasema “Bila shaka sasa wakati umefika wa chama kutekeleza ile sehemu ya pili ya azimio husika kwa kuwawajibisha wahusika, lakini utekelezaji wake hauna budi ufanyike kwa kufuata utaratibu uliowekwa ndani na kanuni za CCM za uongozi na maadili.’’ Lakini mpaka sasa hakuna kitu. Magamba yapo, waliosema wanawavua na kuwataja kwa majina, na kuweka mafuta ili Nape azunguke nchi nzima sasa ndio anafanya nao kazi. ? Tena anawaheshimu.
CCM Waliwatambia watanzania kuwa Msingi wa mpango wa kujivua gamba ulijengwa katika azimio la NEC lililosema: “Viongozi wanaotuhumiwa kwa ufisadi watafakari, wajipime na kuchukua hatua wao wenyewe kwa maslahi ya chama, wasipofanya hivyo, chama kiwawajibishe bila kuchelewa.
Hayo yamepita siku hizi tunazungumzia "Rejuvination of the party". Kuhuisha Chama. Yaani kiwe na Uhai, huku Kikwete akikataa kukubali akisema hakijafa, nape anasema kimekufa kinahitaji kufanywa kuwa hai. Hawajui kama wanapingana.
Aliyejitoa wa kwanza katika vita dhidi ya Ufisadi, na kukiuka maazimio ya NEC, akitumia busara za kung'ota ni Rais Jakaya Kikwete, baada ya kutojitokeza hadharani kuwalaumu mafisadi. Alianzisha wimbo wa kujivua Gamba, Nape akaitikia kiitikio akaendelea hatujui wimbo uliishia wapi hadi akaja na wimbo tofauti unaitwa kujihuisha.
Vita yaUfisadi ndani ya CCM imekosa kamanda wa kuiongoza, ukiacha mafisadi waliotangazwa na Kamati kuu ya CCM April mwaka 2011, watuhumiwa wengine walishatajwa huko nyuma na CCM ilitarajiwa kuwatosa katika uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, lakini Mzee wetu wa busara za Kung'ota, alifika kule akawapigia Kampeni wakaonekana wanafaa, iwe walituhumiwa kupokea Mlungura wa rada, au kashfa za Richmond, na masuala ya vijisenti.
Nape na kelele zote za ufisadi kwenye tenda za ujenzi wa Jengo la UVCCM. Nape aliyemlalamikia Lowassa katika sakata hilo, siku hizi yupo kimya, wapo naye jukwa moja, kuwakwanyua watanzania taratibu. Ameonja Unga wa ndere, amehamia tabaka alilolilaani. Hazungumzi tena kuhusu suala hilo.
CCM kwa uwezo wao mdogo walienda kutengeneza orodha nyingine kuleta kwa watanzania, lengo likiwa ni lile lile la kuwahadaa watanzania kuwa sasa vita ya Ufisadi inaanza. Waliyemtegemea kwa haraka, alikuwa ni Katibu Mkuu mpya, Abdulrahman Kinana. Mzee wa watu hakudumu hata siku chache, Meli zake zikakamatwa kwa kusafirisha pembe za ndovu. Wachambuzi wa mambo wakasema huyu naye ni hatari, "weka mbali na tembo". Serikali inapigana na Ujangili lakini meli ya Katibu Mkuu ndio inasafirisha. Akanukuliwa akisema kuwa
Kwamba nina hisa katika kampuni ya wakala wa meli ya Sharaf ni kweli.
“Lakini mimi sina nafasi yoyote ya kiutendaji na wala sishughuliki na uendeshaji wa kampuni hiyo. Kwa kweli sikujua na wala sikuhusika kwa namna yoyote ile na usafirishaji wa makontena hayo na mengine yoyote". Mimi kijana wa kitanzania nimejiuliza sana, kwamba Mzee huyu anamiliki fuso, anajua fuso ni yak wake na imechukua Machungwa toka Tanga, yameletwa Shinyanga ila hamjui mwenye machungwa, kama yeye hajui je dereva wa meli za kinana naye hajui Makontena ya pembe za ndovu yalikuwa ya nani? Wnasafirishaje mzigo bila kujua ni wa nani? Mzee Kinana naye chali, anafikiria namna ya kutoka ili aje awafafanulie watanzania tuhuma hii mbichi ya kuhusishwa na vyombo vyake vya usafiri katika Ujangili, tatizo linaloisumbua serkali.
Tumaini pekee la CCM, pekee na la mwisho kwenye benchi la Ufundi lilikuwa ni la Mzee Philip Mangula, katibu Mkuu wa Zamani wa ccm na sasa Makamu Mwenyekiti wa CCM bara. Mzee Mangula alirejea na gia mpya katika uongozi wa chama hicho kikongwe huku akiahidi atawang’oa viongozi walioingia katika uongozi wa kwa njia za mkato.
Mimi nilikuwa nalima nyanya na mapalachichi huko kijijini kabla ya kuombwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ili kukisaidia Chama hiki kukitoa hapa kilipo kwa kuwa rushwa imekithiri ndani yake na kazi hii nitaifanya na kuikamilisha ndani ya miezi sita kuanzia sasa,” alisema katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa na CCM Mkoa wa Dar es Salaam katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa lengo la kuwapongeza viongozi wapya wa juu wa chama hicho.
“Malalamiko yapo kwa ngazi mbalimbali za Chama, nimeyakuta mezani kwangu, ndani ya miezi sita itajulikana na walioingia kihalali wataendelea, walioingia hovyo hovyo watatupwa nje,” alisema.
“Viongozi wameingia kwa rushwa na hii nimeipenda na nitaifanyia kazi vizuri sana bila ya kumuonea mtu na kumuogopa mtu yeyote ndani ya Chama chetu ili kurudisha heshima yake,”
Siku chache tu baada ya Mangula kujitapa vile, aliyekwua Mbunge wa Njombe Magharibi (CCM), Yono Kevela amemtuhumu Makamu Mwenyekiti wa CCM Philip Mangula kwa kuvuruga uchaguzi wa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec) ya chama hicho, Wilaya ya Wanging’ombe kwa kuwabeba baadhi ya wagombea.
Katika madai yake ambayo ameyakatia rufani, Kevela amesema katika uchaguzi huo uliofanyika Julai 29 mwaka huu, mbali na kuwabeba wagombea hao, Mangula alishiriki kutengeneza makundi ya vitisho, rushwa na lugha za kejeli dhidi yake.
Alisema siku ya uchaguzi akiwa amekaa meza kuu, Mangula alipopewa nafasi ya kuhutubia, aliwaambia wajumbe kuhakikisha Kevela na mgombea mwingine Hamisi Nurdin hawapiti.
“Mangula alisema watu hao wasichaguliwe kwa kuwa wana malengo tofauti na yale ya kukitumikia chama,” alidai Kevela. Malengo yaliyodaiwa katika rufani hiyo ni kuwa Kevela anautaka ubunge wa Njombe Magharibi na Nurdin ana nia ya kutaka Makao Makuu ya Wilaya ya Wanging’ombe yawe Igwachanya. Sasa ni wazi Mangula hawezi kuwa hakimu kwa kesi inayomhusu. Yeye Mwenyewe naye ni mtuhumiwa wa rushwa na waliompitisha ni watoa rushwa. Vita imekwisha. CCM kila mmoja tangu mwanachama na Kiongozi wote wameshindwa, au wote wameshinda. Hakuna wa kumtuhumu mwenzake. Wote wanavuta hewa ile ile, hakuna anayeweza kumwambia mwenzake hewa hii ni chafu. Watanzania fikirini wenyewe ili muendelee kuibakiza CCM madarakani kwa hasara yenu.
Mimi ntamwambia Mungu kuwa niliwambia.
0786-426414
No comments:
Post a Comment