WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Tuesday, December 18, 2012

DR MAGUFULI APELEKA BOMOA BOMOA MOROCCO




WAZIRI wa Ujenzi, Dk John Magufuli ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kuanza kuvunja nyumba zilizopo ndani ya hifadhi ya Barabara ya Mwenge hadi Morocco, Dar es Salaam ili kupisha ujenzi wa barabara nne za lami.

Pia, ameitaka Tanroads kuacha kigugumizi katika ujenzi wa barabara za juu jijini Dar es Salaam (flyovers) kwa kuwa fedha kwa ajili ya kazi hiyo zipo.Waziri Magufuli alitoa wito huo Dar es Salaam jana, alipokuwa akizindua bodi mpya ya Mfuko wa Barabara na Bodi ya Tanroads.

“Barabara ya Mwenge- Morocco nyumba zinatakiwa kubomolewa. Zibomolewe haraka ili kupisha ujenzi. Nasema Tanroads acheni kigugumizi kwenye masuala haya,” alisisitiza Dk Magufuli.

Ingawa hakuzianisha nyumba zilizotakiwa kubomolewa katika barabara hiyo, sehemu kubwa ina nyumba za thamani kubwa hasa ghorofa jambo ambalo linatarajiwa kuwaweka katika wakati mgumu wamiliki wake.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Tanroads, Patrick Mfugale alisema: “Nyumba zitakazobomolewa siyo nyingi. Ni zile zilizojengwa ndani ya mita 30 ya hifadhi ya barabara. Kinachotuchelewesha ni kuondolewa kwa nyaya za umeme pamoja na mfumo mkubwa wa maji ili tuweze kuanza ujenzi.”

Waziri Magufuli alisema fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo zipo na hata za kuwalipa wamiliki wa nyumba hizo zipo, hivyo akasisitiza kuwa kazi ya kuzibomoa inapaswa kuanza mara moja.
“Wanaostahili kulipwa fidia walipwe na ambao hawastahili waondoke. Suala la kwamba mko kwenye mchakato life na libaki kuwa neno la wanasiasa tu,” alisema Magufuli.

Bajeti ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2012/13, imeonyesha kuwa barabara hiyo yenye urefu wa kilometa 4.3, ujenzi wake unafadhiliwa na Serikali ya Japan.
Kuhusu ujenzi wa barabara za juu, Waziri Magufuli alisema ni jambo linalowezekana na halihitaji kufanyiwa mchakato wowote.

Alisema ni muhimu bodi hiyo mpya ikasimamia ujenzi wa barabara hizo ili kupunguza msongamano wa magari Dar es Salaam.

“Tengenezeni ‘flyovers’ nyingi nyingi, ni kazi ndogo lakini inashangaza kwa nini Tanroads inakuwa na kigugumizi,” alisema Magufuli na kuongeza: “Wahandisi wa Tanroads fanyeni hivyo, mbona kule Kenya mambo yamefanyika bila tatizo? Acheni kigugumizi na siasa mfanye kazi.”

source: vijimambo.blog

No comments:

Post a Comment