WHATEVER YOUR ARE BE A GOOD ONE;

A nation that is afraid to let its people judge the truth and falsehood in an open market is a nation that is afraid of its people. John F. Kennedy

“Taifa letu – taifa lolote – ni zuri na mahali pazuri pa kuishi kama raia wake watalifanya liwe hivyo. Uongozi wake unaweza kuwa mzuri, mbaya au usiojali lakini kama watu wake wameamka (ki-elimu?) na wanajitambua, haitachukua muda mrefu kuwakilisha mtazamo wa jamii na kubadili mawazo na matumaini ya taifa.” Julius Kambarage Nyerere


Saturday, December 29, 2012

Lissu amkaanga Profesa Shivji



Fredy Azzah
HATUA ya mwanazuoni wa siku nyingi nchini, Profesa Issa Shivji kupinga hukumu ya Mahakama ya Rufani Tanzania iliyomrejeshea ubunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema imemtia matatani na baadhi ya watu wanasema gwiji huyo wa sheria “huenda amenukuliwa vibaya au hajasoma hukumu husika.”
Jana Wakili wa Lema, Tundu Lissu, alimkosoa Profesa Shivji pamoja na Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika, Francis Stolla akisema wanasheria hao wamepotoka katika matamshi yao ya kupinga hukumu ya Mahakama ya Rufani.
Matamshi ya Shivji pia yaliiteka mijadala katika mitandao ya kijamii ya Jamii Forums, Mabadiliko na Facebook ambako wachangiaji  walikuwa wakivutana huku baadhi yao wakisema wazi kwamba msomi huyo amekosea huku wengine wakimtetea kwamba yuko sahihi.
Akizungumza na gazeti hili jana kutoka Songea mkoani Ruvuma, Lissu alipinga vikali hoja zilizotolewa na Profesa Shivji pamoja na Stolla, akisema kuwa hazina mashiko na zinaweza kutolewa tu na mtu ambaye hakufuatilia mwenendo wa kesi hiyo.
Juzi Profesa Shivji na Stolla walinukuliwa wakiikosoa hukumu ya Mahakama ya Rufani, iliyomrejesha bungeni Lema wakisema hukumu hiyo iliyotolewa na majaji watatu Salum Massati, Bernard Luanda na kiongozi wao Nathalia Kimaro, inapingana na sheria.
Lissu katika maelezo yake alisema uamuzi wa mahakama katika kesi ya Lema umejenga upya msingi bora wa matumizi ya vyombo vya uamuzi, kwani kesi nyingi za kupinga matokeo ya ubunge, zimekuwa zikifunguliwa na watu ambao wamekuwa wakitumwa na vigogo wa kisiasa na watu wenye fedha.
Akizungumza na Mwananchi, Lissu alisema hoja hizo hazina mashiko na kuwa ile iliyotolewa na Profesa Shivji inatokana na msomi huyo kuzungumza kitaalamu bila kuangalia mazingira halisi ya siasa za Kitanzania.
Lissu alisema mahakama ya rufani haikupiga marufuku wapiga kura kufungua kesi za kupinga ila iliwataka tu kufanya hivyo pale haki zao zinapokiukwa.
“Kwanza siyo kweli kwamba mahakama imepiga marufuku wapiga kura kufungua kesi, ilisema watafanya hivyo pale ambapo haki zao zimevunjwa, haki zenyewe ni kupiga kura, kura zao kutohesabiwa ama suala jingine litakalomnyima kupiga kura, hizo ndiyo haki za mpiga kura,” alisema na kuongeza:
“Sasa mwalimu wangu, Profesa Shivji yeye anatazama tu kwa jicho la kitaalamu na kusema haki za binadamu zimekiukwa, kwa muda wanasiasa, matajiri na CCM wamekuwa wakiwatumia wananchi kuwapinga wabunge wa upinzani.”
Uchambuzi wa Lissu
Alitoa mfano akisema katika uchaguzi wa 1995, Dk Willibrod Slaa alishinda ubunge na watu wanaojiita wananchi walifungua kesi kupinga ushindi huo, mwaka 2000 wakampinga tena na hata 2005.
Alisema 1995 Makongoro Nyerere aliposhinda ubunge katika Jimbo la Arusha Mjini kupitia NCCR- Mageuzi, watu wanaojiita wananchi walifungua kesi ambayo matokeo yake yalikuwa mbunge huyo kupoteza kiti chake.
Lissu alisema 2005 aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Marehemu Chacha Wangwe alifunguliwa kesi na watu waliojiita wananchi ambao mwisho wake walishindwa.
“Hawa wananchi ambao wanafungua kesi zenye mawakili wanaolipwa mamilioni ya fedha ni watu ambao hata fedha za kununua viatu hawana,  hawa waliokuwa wakimpinga Marehemu Wangwe nikiwa mahakamani niliwauliza kama wanawajua mawakili waliokuwa wanawatetea, walikuwa hawawajui.
Nikawauliza kama wamewahi kufika Dar es Salaam wakasema hapana, sasa sijui waliwapataje wale mawakili,” alisema na kuongeza:
“Wote hawa  wanakuwa ni watu wanaotumiwa. Mwaka huu kati ya wabunge wote 25  Chadema tulioshinda, 14 tulifunguliwa kesi na kati ya hizi 12 zimefunguliwa na watu wanaojiita wananchi, hii ni kutumiwa,” alisema.
Alisema mara baada ya uchaguzi mwaka 2010 aliyekuwa Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba, aliandika waraka kuwataka makatibu wa chama hicho kufungua kesi kwa majimbo yote ambayo chama hicho kiliangushwa jambo alilosema ndilo liliwasukuma kuwatumia wananchi.
Kuhusu hoja kuwa mahakama hiyo ya rufani imeingilia kazi ya kutunga sheria badala ya kuzitafsiri na kuwa imepingana na sheria ya Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Chediel Mgonja ya mwaka 1980, Lissu alisema hazina mashiko.
“Hiyo ni hoja ya kipuuzi. Hiyo sheria ya kuwa mwananchi yeyote ana haki ya kufungua kesi kuwa imetenguliwa na Mahakama ya Rufani, hata mwanafunzi wa mwaka wa kwanza wa sheria ukimuuliza atakwambia kuwa, amri ya Mahakama Kuu wala ya Mahakama ya Rufani yenyewe haiwezi kuizuia mahakama hiyo ya juu kabisa nchini kufanya uamuzi wake,” alisema.
Akizungumzia hoja ya Stolla kwamba mahakama iliibua jambo jipya la kuhoji kama wajibu rufani walikuwa wapiga kura ama la, alisema Rais wake huyo hana hoja, kwani wakili wa walalamikaji aliibua hoja kama hiyo na alipoulizwa na mmoja wa majaji kuwa “Hata sisi hatuwezi kulizungumzia suala hili, alishindwa kujibu akawa anajikanyaga tu,” alisema.
Aliongeza: “Kwenye rufaa ya kwanza mahakama inaruhusiwa kuibua chochote, sasa hizo ni hoja zinazotolewa na watu ambao marafiki zao wa CCM wameshindwa sasa wanavaa joho la utaalamu kutoa hoja kama hizi zisizo na mashiko.”
Shivji na Stolla
Profesa Shivji kwa upande wake alieleza kushangazwa na maelezo ya Mahakama ya Rufani kuwa mpiga kura hana haki ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi na kusema hiyo ni sawa na kutunga sheria mpya na si kutafsiri zilizopo.
“Sheria ya Bunge na Mahakama Kuu katika kesi ya Mgonja (Chediel ya mwaka 1980), vinampa haki mpiga kura kufungua kesi mahakamani kupinga matokeo. Sijaona hoja nzito ya Mahakama ya kufuta haki hiyo ya mpiga kura,” alisema Profesa Shivji.
Kwa upande wake, Stolla alisema: “Nimesikiliza hata maoni ya wanasheria mbalimbali wakizungumzia kutopendezwa na tafsiri ya Mahakama ya Rufani kuhusu haki ya mpiga kura ‘ku-challenge’ (kupinga) matokeo ya uchaguzi mahakamani.
Aliongeza: “Katika uamuzi wa kisheria, inaonekana Mahakama imetunga sheria mpya na wengi tunajiuliza kama siyo, ni sababu gani nyingine inampa haki mpiga kura kupinga matokeo?”
Stolla alisema Sheria ya Bunge ya Uchaguzi ya tangu mwaka 1985, ambayo ilifanyiwa marekebisho mwaka 2002, kabla ya kutungwa upya mwaka 2005, inampa haki mpiga kura kupinga matokeo ya uchaguzi mahakamani.

Kesi ya Lema
Lema alivuliwa ubunge na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Aprili 5, mwaka huu kutokana na kesi iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, wakipinga ushindi wake.
Walikuwa wakidai kuwa katika kampeni zake alikuwa akitumia lugha ya matusi, kejeli na ubaguzi wa kijinsia dhidi ya aliyekuwa mgombea wa wadhifa huo kwa tiketi ya CCM, Dk Batilda Buriani.

Mahakama Kuu katika hukumu yake iliyotolewa na Jaji Gabriel Rwakibarila ilimtia hatiani kwa kutumia lugha ya matusi na kutengua matokeo yaliyompa ushindi.

Hata hivyo, alikata rufaa Mahakama ya Rufani kupitia kwa mawakili wake, Method Kimomogoro na Tundu Lissu ambayo Desemba 21, mwaka huu ilimrejesha tena bungeni baada ya kukubali rufaa yake.

Katika uamuzi wake, Mahakama hiyo ilisema kwa kuwa kisheria hayo ni masilahi ya umma kufikishwa mahakamani chini ya Ibara ya 26 (2) ya Katiba na kwamba mlalamikaji anapaswa kuonyesha haki zake au masilahi ambayo yameingiliwa na athari alizozipata.

source: mwananchi

No comments:

Post a Comment